Connect with us

Kitaifa

Rais Samia amweka Bashe mtegoni

Dar/Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan amemweka mtegoni Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akisema hatavumilia matumizi mabaya ya fedha za mpango wa kilimo katika mashamba makubwa ya pamoja.

Rais Samia alitoa kauli hiyo jana Chamwino jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango unaojulikana kama Building Better Tomorrow (Kujenga Kesho Njema-BBT) utakaotekelezwa katika hekta 317,000 maeneo mbalimbali nchini.

Pia, Rais Samia alitumia hafla hiyo kuzindua mkakati wa ufufuaji mabonde, ndege zisizo na rubani na magari 83 ya wahandisi umwagiliaji kwenye miradi hiyo ya kimkakati.

Pia aliwataka wakandarasi wazawa kuacha kumchezea katika utekelezaji wa miradi.

BBT ni mpango wa Wizara ya Kilimo unaolenga kuwawezesha vijana kumiliki mashamba makubwa na kupewa hati huku Serikali ikiwawezesha miundombinu yote muhimu.

Ni sehemu ya mkakati uliowekwa na Serikali na kutengewa sehemu kubwa ya fedha katika bajeti ya mwaka 2022/23, ili kufanikisha uwekezaji mkubwa kwenye kilimo na kuongeza ajira kwa vijana na wanawake.

‘Sitavumilia’

Kutokana na kipaumbele kinachotolewa kwa mpango huo, Rais Samia alionya: “Nataka kuwaambia nimekusudia kwenye hili na sitavumilia. Bashe na wenzio pale nitakapotoa fedha za wavuja jasho wa Tanzania ziende kwenye matumizi ya kilimo zikazalishe na fedha zile zikachezewe, sitavumilia.”

Alisema amedhamiria kuona kinachofanyika kinatimia na kwamba hilo alilianza kwa kupandisha bajeti ya kilimo na ataendelea kufanya hivyo katika miaka ijayo.

Kwa mujibu wa Rais Samia, anachotaka kuona ni kila fedha zitakazotumika zikazalishe karibu mara mbili hadi tatu.

“Mmetaka vifaa nimewapa, mmetaka ajira nimewapa, mmekuja na wazo nimesema zuri sana endeleeni, fedha nimetoa sioni mtashindwa wapi, mtashindwa ikiwa hamna dhamira, lakini kama mna dhamira, sioni mtashindwa wapi,” alisema Rais Samia.

Hata hivyo, alisema si Wizara ya Kilimo pekee bali jambo hilo linapaswa kusimamiwa na wizara zenye sekta zote zinazogusa kilimo kama Ardhi, Maji na Mazingira.

Katika hilo, alitaka mawaziri wa sekta hizo waunde kamati ya kushughulikia utekelezaji wa mpango huo.

“Sitaki kusikia tumeshindwa. Hakuna kushindwa, lazima twende na lazima tufanikiwe,” alisema.

Alisema baada ya kutangaza mpango huo takriban vijana 20,000 wameomba na kwamba imebainika wengine tayari wapo mashambani wanafanya shughuli za kilimo.

Aliwataka vijana waliopata nafasi ya kuchaguliwa wakahakikishe wanafanya kazi iliyokusudiwa, huku akiwaahidi kuwapatia kila alichowaahidi.

“Tutataka mkazalishe chakula na mazao ya biashara ambayo yatatuletea faida nchini na bahati nzuri mazao yote leo ni kilimo cha biashara,” alisema.

Hata hivyo, mkuu huyo wa nchi aliwageukia wakandarasi wa ndani waliopata nafasi ya kutekeleza mpango huo, kuhakikisha wanatekeleza kama ilivyokusudiwa.

“Kama umepita njia zako na ukapata kazi hii si kwa nia ya kufanya kilichokusudiwa, basi jipange kwamba umesajili mapambano na mama.

“Na mama huwa hapambani, mama amewazaa wote huwa hapambani, anaadhibu tu na akikuadhibu huwezi kupambana naye,” alisema.

Alisema kwa sasa Serikali imegharimia ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji na kwamba baadaye vikundi vyao ndivyo vitakavyojichangisha kuwezesha utunzaji wake.

Mpango wenyewe

Awali, Waziri Bashe alisema safari ya mafanikio katika kilimo ni ngumu, lakini kwa namna yoyote lazima Watanzania watafika.

Bashe alisema pamoja na magumu wanayopitia, hakuna namna lazima mabilionea wanaotokana na kilimo wazalishwe na alimwahidi Rais kuwa atamkabidhi matajiri kutoka katika kilimo mwishoni mwa mwaka 2027.

Alisema vijana wanaopata ardhi, wanapewa hati za kumiliki maeneo hayo kwa miaka 66 na aliwaonya ambao hawako tayari waeleze mapema, ili wapewe nauli za kurudi makwao.

Mpaka jana wizara ilishapokea vijana 812 wa mwanzo na wameshaanza mafunzo ya miezi minne kabla ya kwenda kukabidhiwa mashamba kuanza shughuli za kilimo.

Waziri alisema katika mataifa mengine duniani, Serikali ndiyo inayowajenga matajiri na mabilionea na hiyo ndiyo ndoto yao ndani ya Wizara ya Kilimo.

“Lakini nataka mtambue kuwa, kilimo si kubeti, kilimo ni mfumo endelevu unaohitaji uvumilivu wa hali ya juu, watu wasitegemee kuanza leo halafu mwezi Agosti wawe wamefanikiwa, haiwezekani,” alisema Bashe.

Kwa mujibu wa Bashe, kwa miaka yote kumekuwa na maelezo kuwa ziko hekta 712 zinazofaa kwa kilimo, lakini ukweli si hivyo, kwani hiyo ilikuwa ni mifereji tu ambayo inatumika kwa msimu wa mvua pekee.

Katika hatua nyingine, Bashe alisema wamejidhatiti kusimamia mkakati wa kuhakikisha mwaka 2027 korosho ya Tanzania haisafirishwi ikiwa ghafi kwa kuwa mchakato yote ya ujenzi wa kiwanda cha kubangua zimekamilika.

Patrick Kasare, mmoja wa wakandarasi watano walisaini mikataba alisema agizo la Rais litawapa hamasa ya kufanya kazi kwa kujituma zaidi.

Meneja masoko wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi alisema benki yao imetenga Sh20 bilioni kwa ajili ya kusaidia shughuli za kilimo kwa kuwa wamejiridhisha kuwa mpango huo unakwenda kuzaa matunda.

Mponzi alisema wamekaa na vijana 812 wa awamu ya kwanza na kuwafundisha njia za kibiashara ambazo wanaamini zitawapelekea kwenye faida na tayari wamewafungulia akaunti za benki.

Spika wa Bunge Dk Tulia Akson alisema ili kufanikiwa kwenye mpango wa kilimo, lazima wizara ziunganishe nguvu ya pamoja ambayo itafanya kuwepo na mnyororo wa thamani kwani bila kufanya hivyo kutakuwa na ugumu kwenye utekelezaji.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi