Kitaifa
Temeke yatoa mikopo ya Sh4.6 bilioni
Dar es Salaam. Vikundi 185 vya wanawake, wenye ulemavu na vijana kutoka Wilaya ya Temeke leo vimekadhiwa mkopo wa Sh4.6 bilioni ili viweze kuendelea shughuli zao za kiuchumi.
Vikundi hivyo vina jumla ya wananufaika 1,146 ambao wanajishughulisha na vitu mbalimbali ikiwemo usindikaji wa bidhaa, bodaboda, utengenezaji wa Tomato.
Fedha hizo ni sehemu ya asilimia 10 ya mapato ya halmashauri zinazotolewa kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza baada ya kupokea mikopo hiyo, Clara Sanga ambaye ni mmoja wa wanufaika amesema italeta tija kwao katika kukuza uzalishaji na kutanua wigo wa ajira.
“Ajira hazitaishia kwetu sisi, wapo watakaoshiriki katika utekelezaji wa miradi yetu ili iweze kuendelea, kuongeza mzunguko wa fedha, kutatua kero na kutoa huduma katika maeneo tunayotoa na tutakwenda kubadili mawazo ya wasiochangamkia fursa ya mikopo hii,” amesema Clara.
Mkurugenzi wa Temeke, Elihuruma Mabelya amesema utoaji wa mikopo hiyo ni utekeleza wa maagizo ya Serikali ambayo yanalenga kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye walemavu.
“Hadi Februari mwaka huu Sh11.869 bilioni zilikuwa zimetolewa, katika kipindi hiki pia tulipanga kukusanya Sh7.8 bilioni lakini tumekusanya Sh4.6 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 60 ya makusanyo yetu,” amesema Elihuruma.
Ili kuongeza wigo wa ukusanyaji mikopo hiyo wamesema wako mbioni kununua gari ambalo litakuwa likifanya ukaguzi katika miradi ya wajasiriamali hao na kutatua changamoto wanazokutana nazo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla ambaye alikuwa mgeni rasmi katika katika hafla hiyo aliwataka waliokopeshwa kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima ili waweze kurejesha mikopo waliyopewa kwa wakati.
“Kila nguo inayotoka we umo unataka, umepewa mkopo unaenda kununua samani za ndani, hizo samani zitakusaidia kurejesha mikopo, mpunguze matumizi yasiyokuwa ya lazima,” amesema Makalla.
Alitumia nafasi hiyo pia kuzitaka wilaya za mkoa huo kuhakikisha wanatoa mafunzo kwa watengenezaji bidhaa ili waweze kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi ikiwemo kwa kupata namba ya utambulisho wa bidhaa (Barcode).
“Mamlaka husika, mnapoenda kuwakagua hawa kinamama hasa watengenezaji wa bidhaa watieni moyo na si kuwakaripia, we naye kifungashio gani hiki umetumia hata bidhaa hazionekani, mwambie umefanya vizuri ila angefanya hivi ingekuwa bora zaidi, watueni moyo,” emesema Makalla.