Kitaifa
Wananchi wasimulia machungu ndugu kuliwa na mamba
Buchosa. Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Izindabo Kata ya Lugata Kisiwa cha Kome wamesimulia machungu ya ndugu kushambuliwa na mamba hadi kupoteza maisha na wengine kupata ulemavu wakudumu matukio hayo yameleta simanzi kubwa Kwa jamii.
Machi 9 mwaka huu Primtiva Mtaloza mkazi wa Kijiji cha Izindabo Kata Lugata alishambuliwa na mamba kisha kupoteza maisha wakati anaoga Ziwa Victoria.
Ndani ya muda mfupi ndani ya mwaka huu takribani watu saba wamepoteza maisha, hivyo wananchi kufikia hatua kuiomba serikali kuwasaidia kuvuna mamba hao wanaohatarisha usalama wao.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Izindabo Stiven Gerevaz ametoa shukrani kwa maofisa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (Tawa) baada ya kufanikiwa kuwavua mamba wawili waliosadikika kuua watu kwenye Kijiji cha Izindabo kata Lugata Wilayani Sengerema mkoa wa Mwanza.
Amesema licha ya mamba hao kuvunwa ametoa wito kwa wananchi wa Kijiji cha Izindabo kuacha mazoea ya kuoga ziwani bali watumie vizimba vilivyojengwa na Serikali Kwa ajili ya kujikinga kushambuliwa na mamba.
Ofisa msaidizi daraja la pili wa Tawa, Mohamed Mpoto amesema licha ya kuwavuna mamba hawa pia wanatoa elimu kwa wananchi juu ya athari zinazosababishwa na wanyama wakali hususani mamba.
Amewataka wananchi kutoa ushirikiano wa dhati katika zoezi hili la kuwasaka mamba ili waweze kuvunwa na wananchi waishi kwa amani.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Lugata Nduhelechi Mwebesa amewapongeza maofisa wanyamapori kufanikiwa kuwavuna mamba hao.
Mwananchi wa Kijiji cha Izindabo, Inosent Majaliwa amesema suluhisho la wananchi kuacha kushambuliwa na mamba ni kupatikana kwa maji ya bomba kwenye kata la Lugata ili wananchi waache kuoga ziwani.
Omari Muhando ni Mhifadhi wa Wanyamapori kitengo cha mahusiano kwa jamii amesema elimu wanayoitoa kwa wananchi juu kuepuka kushambuliwa na mamba itawasaidia wananchi wa Kijiji cha Izindabo.
Ofisa Mtendaji Kata ya Lugata Rafael Jangole amesema wananchi wanatakiwa kuwa waangalifu wakati wanafanya shughuli za kibinadamu ndani ya Ziwa Victoria ili kujiepusha na kushambuliwa na mamba.