Connect with us

Kitaifa

Mahakama yazuia shughuli za Chadema kwa muda

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam imezuia kwa muda shughuli zote za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katibu mkuu, mawakala na wafuasi wa chama hicho kushiriki kwa namna yoyote shuguli zote za kisiasa hadi pale kesi ya msingi itakaposikilizwa.

Pia imeagiza mali zote za Chadema zisitumike mpaka pale kesi ya msingi itakaposikilizwa.

Kesi ya msingi kuhusu mgawanyo wa rasilimali za chama hicho imepangwa kuanza kusikilizwa Juni 24, 2025.

Kesi hiyo imefunguliwa na Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Zanzibar na wenzake wawili, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, ambao ni wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutokea Zanzibar.

Wadaiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema, ikiwa mdaiwa wa kwanza na Katibu Mkuu wa Chadema, akiwa mdaiwa wa pili.

Awali, Mahakama hiyo ilitupilia mbali pingamizi la Chadema kuhusu kesi hiyo lililokuwa na sababu tisa za kutaka kesi itupwe bila kusikilizwa madai ya msingi ya wadai.

Katika sababu hizo Chadema kilidai wadai hawajaonyesha kiwango cha fedha kinachodaiwa, wadai kutokutumia taratibu za ndani ya chama kabla ya kwenda mahakamani na viapo vya mdai wa pili na wa tatu kutokuambatanishwa kwenye hati ya madai.

 

Sababu nyingine ni wadai kutokuwa na mamlaka ya kumshtaki mdaiwa wa kwanza (Bodi ya Wadhamini) kwa madai kuwa nao ni sehemu ya bodi ya wadhamini.

Vilevile walidai wadai hawana haki ya kisheria kufungua kesi hiyo mahakamani, Pia hawana mamlaka ya kumshtaki mdaiwa wa pili, Katibu Mkuu wa Chadema na mwisho kesi kufunguliwa bila kutaja kifungu cha sheria kinachoipa Mahakama mamlaka kusikiliza kesi hiyo.

Pingamizi hilo lililosikilizwa kwa njia ya maandishi limetolewa uamuzi leo Jumanne, Juni 10, 2025 ambalo Mahakama imelitupilia mbali.

Jaji Mwanga katika uamuzi wake amechambua sababu moja baada ya nyingine, hatimaye akahitimisha kuwa pingamizi la Chadema halina mashiko ya kisheria.

“Kwa kuzingatia uchambuzi huo nimejiridhisha kuwa pingamizi hili halina mashiko na linatupiliwa mbali. Ninaamuru kesi ya msingi itaendelea kusikilizwa Juni 24, 2025,” amesema Jaji Mwanga.

 

Mbali na kesi ya msingi, Chadema kiliweka pingamizi dhidi ya shauri la maombi ya zuio la muda, huku kikitoa sababu kama zilizotolewa dhidi ya kesi ya msingi.

Waombaji (wadai) kwa upande wao waliibua pingamizi la awali dhidi ya kiapo kinzani cha wadaiwa kinachojibu kiapo cha wadai kinachounga mkono maombi ya zuio la muda wakiibua hoja tano, pamoja na mambo mengine kuhusu kasoro za kisheria kwenye hati ya kiapo.

Katika amri yake ya mwisho, Jaji Mwanga alielekeza mapingamizi yote (pingamizi la Chadema dhidi ya maombi ya zuio na pingamizi la wadai dhidi ya kiapo kinzani cha Chadema na shauri la maombi ya zuio) yasikilizwe Juni 10, 2025 kwa mdomo.

Usikilizwaji wa mapingamizi hayo ulitegemea uamuzi wa pingamizi la Chadema dhidi ya kesi ya msingi, iwapo Mahakama ingekubaliana na pingamizi lao, kesi ya msingi ingetupiliwa mbali na huo ungekuwa mwisho wa kila kitu, kwani hata maombi ya zuio la muda yasingeweza kusimamia.

Lakini kwa uamuzi wa Mahakama, kesi ya msingi ipo mahakamani na imeendelea na usikilizwaji pingamizi la Chadema dhidi maombi ya zuio, pingamizi la wadai dhidi ya kiapo cha Chadema na maombi yenyewe ya zuio la muda na kufikia uamuzi wa kuzuia shughuli za chama hicho kwa muda hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na uamuzi kutolewa.

 

Wakili Chadema ajitoa

Shauri la zuio lilisikilizwa upande mmoja wa mdai, baada ya wakili wa mdaiwa (Chadema), Jebra Kambole kuomba kujiengua kuendelea na shauri hilo.

“Siwezi kuendelea na shauri hili, naomba kujiengua ili wateja wangu wapate muda kutafuta wakili mwingine,” amesema.

Baada ya kujiengua, Kambole na wafuasi wa Chadema waliokuwa mahakamani waliondoka na kuacha shauri la zuio likiendelea kusikilizwa upande mmoja.

Katika kesi ya madai namba 8323 ya mwaka 2025, wadai wanaiomba Mahakama itamke na kuamuru wadaiwa wamekiuka sheria zinazohusu vyama vya siasa na Katiba ya chama hicho.

Wameomba amri hizo za mahakama wakidai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.

Pia, wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga Muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa msingi huo, waombaji wanaomba Mahakama itoe hukumu na amri dhidi ya wadaiwa kwamba wamekiuka kifungu cha 6A (1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019.

Pia, wanaiomba Mahakama itamke kwamba ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.

Vilevile wanaiomba Mahakama itamke na kuwaelekeza wadaiwa kuzingatia kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019.

Amri nyingine wanazoomba ni kusitishwa kwa muda kwa shughuli zote za kisiasa hadi hapo kutakapokuwapo utekelezaji wa maagizo ya Mahakama.

Wanaiomba Mahakama itoe amri ya zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi wajibu maombi watakapotekeleza matakwa ya sheria husika.

Mbali na amri hizo, wanaiomba Mahakama iamuru wadaiwa walipe gharama za kesi na itoe nafuu nyingine yoyote ambayo Mahakama itaona inafaa kuzitoa.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi