Connect with us

Makala

Wataka kibano walimu wanaoendekeza viboko

Simiyu. Serikali imeshauriwa kuwaondoa katika nafasi zao walimu wakuu wa shule za msingi na wakuu wa shule za sekondari, watakaoshindwa kusimamia utaratibu,kanuni na miongozo ya utoaji wa adhabu ya viboko kwa wanafunzi katika shule zao na kusababisha madhara kwa wanafunzi.

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,  ilitoa Waraka wa Elimu Na.24 kuhusu adhabu ya viboko ukielekeza utaratibu mahususi wa adhabu ya viboko.

Katika mwongozo huo, walimu wanaelekezwa kutoa adhabu isiyozidi viboko vinne kwa Mara moja, kwa makosa makubwa ya kinidhamu au yale ya jinai yanayotendeka shuleni au nje ya shule.

Adhabu hiyo itatolewa na mwalimu mkuu au mwalimu mwingine aliyekasimishwa, baada ya kuzingatia ukubwa wa kosa, umri wa mwanafunzi na afya yake.

 

Wadau Simiyu wataka hatua

Wakizungumza na Mwananchi Jumapili Machi 9,2025,  wadau wa elimu katika Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, wameshauri Serikali kuachana na walimu wanaoshindwa kusimamia waraka huo.

Ni ushauri walioutoa kufuatia kuongezeka kwa matendo ya wanafunzi kuathiriwa kwa adhabu ya viboko kwa  kujeruhiwa na hata kusababisha vifo.

Tukio la hivi karibuni ni la mwanafunzi, Mhoja Maduhu ambaye alifariki kutokana na kipigo cha mwalimu katika Shule ya Sekondari Mwasamba wilayani Busega mkoani hapa.

Mhoja inadaiwa alipigwa viboko 10 sambamba na kukanyagwa kichwani Na mwalimu wake, na baadaye kufariki dunia.

Licha ya kuwapo kwa mwongozo, cha kushangaza utolewaji wa adhabu hizo haufuati utaratibu husika kwa mujibu wa waraka.

Slivester Lugembe, mkazi wa Wilaya ya Maswa amesema kuwa kwa sasa kumekuwa na wimbi la baadhi ya walimu wa shule hizo katika wilaya hiyo

kutoa adhabu ya viboko kwa wanafunzi bila kufuata utaratibu,  huku viongozi hao wa shule wakiwepo na kushindwa kuchukua hatua.

Amesema kuwa wanafunzi wengi wamekuwa wakiumizwa kwa kupigwa na viboko, jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu, huku  matukio hayo yakizua uadui kati ya walimu,  wanafunzi pamoja na wazazi.

“Binafsi adhabu ya viboko naiunga mkono kwani inasaidia kurejesha nidhamu ya mwanafunzi, lakini itumike kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na siyo kumchapa mwanafunzi sehemu mbalimbali za mwili na

kumsababishia maumivu makali na wengine hupelekwa hospitali kulazwa. Na unaweza kukuta kosa lenyewe labda kachelewa kufika shuleni…” amesema na kuongeza:

‘Ni vizuri kabla ya kutoa adhabu hizo mwalimu ajaribu kumhoji mwanafunzi sababu ya kufanya kosa hilo. Unaweza kugundua jambo na ukamsaidia na huenda ukafahamu tatizo liko kwa mzazi na wala si kwa mwanafunzi, hivyo kumuadhibu ni kumuonea. Ni vizuri walimu wakuu na wakuu wa shule wakasimamia utoaji wa adhabu hizo katika shule zao.”

Naye Mary Samson mkazi wa mjini Malampaka wilayani humo,  amesema kuwa adhabu hiyo imekuwa ikilaumiwa na wananchi wengi hapa nchini kwani kwa sasa walimu hawachapi tu  viboko bali ni kutoa vipigo kwa wanafunzi ambavyo ni ngumi na mateke.

“Kinachofanyika shuleni walimu wanakiuka taratibu zilizowekwa na Serikali juu ya utoaji wa adhabu hiyo. Wanapiga viboko visivyo na idadi na mbaya zaidi wamegeuza vipigo vya ngumi na mateke. Walimu wa kiume wanawachapa wanafunzi wa kike kinyume cha utaratibu, walimu waliopewa dhamana ya kusimamia shule wameshindwa kazi ya uongozi,”ameeleza.

Ni kinyume cha sheria

Basila Bruno, ni Ofisa Maendeleo ya Jamii wilayani humo,  anayesema kuwa sheria ya mtoto ya mwaka 2009 chini ya kifungu cha 13(1), inakataza mtu kumsababishia mtoto mateso au aina yoyote ya ukatili, kumpa adhabu zisizo za kibinadamu au kumdhahlilisha mtoto.

“Adhabu ya viboko kwa wanafunzi shuleni inatamka wazi kuwa ni viboko vinne tu vinavyoruhusiwa kwa wanafunzi wavulana kuchapwa kwenye makalio na wasichana mikononi na mwalimu akitoa adhabu hiyo anaagizwa aandike kitabuni kuonesha tarehe na idadi ya viboko na aliyeadhibiwa lazima asaini kitabuni humo lakini haya yote hayafanyiki,”amefafanua.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Wilaya ya Maswa, Athuman Kalaghe, amesema adhabu hiyo iliwekwa ili kutunza nidhamu kwa wanafunzi shuleni na wanaoadhibiwa ni wale waliofanya makosa makubwa.

Amesema kuwa utaratibu unamtaka mwalimu mkuu kutoa adhabu ya viboko au kukasimisha mamlaka yake kwa umakini mkubwa kwa mwalimu yeyote kutoa adhabu hiyo, na mwalimu anayechaguliwa kutoa adhabu atakuwa na mamlaka ya kutoa adhabu pale tu atakapopata idhini ya mwalimu mkuu katika tukio husika..

“Adhabu ya viboko bado ina umuhimu na inatumika katika shule za msingi na sekondari hapa nchini. Hata hivyo, adhabu hiyo inapaswa kutolewa kwa mwanafunzi ambaye amefanya makosa makubwa shuleni,” anasema.

Sheria ya Elimu Sura ya 353 marejeo ya mwaka 2002` Kifungu cha 61(1)(v) kinampa mamlaka Waziri Mwenye dhamana ya elimu, kutunga kanuni za masuala mbalimbali yatakayokidhi utekelezaji wa masuala ya sheria hiyo.

Kupitia mamlaka hiyo, moja ya kanuni zilizotungwa ni  mwongozo wa kutoa adhabu ya viboko, ikielezea wakati wa kutoa adhabu pamoja na kiwango cha adhabu hiyo kwa mwanafunzi.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi