Connect with us

Kitaifa

Bei za mafuta ya petrol, dizel zaongezeka Dar

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei mpya za mafuta zitakazotumika kuanzia leo Jumatano Machi 1, 2023 huku bei ya petrol na dizeli zikipaa ikilinganishwa na Februari.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Mwainyekule imeonyesha kuwa katika jiji la Dar es Salaam bei ya mafuta ya Petroli itauzwa Sh2,960 mwezi huu ikilinganishwa na Sh2,819 ya Februari.

Hali kadhalika, bei ya dizeli imeongezeka kidogo kutoka Sh3,105 Februari hadi Sh3,130 mwezi huu sawa na ongezeko la Sh25.

Wakati bei hizo zikipaa katika jiji la Dar es Salaam, hali ni tofauti kwa mikoa ya kaskazini ikijumuisha Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara ambao mafuta ya dizeli yamepungua kwa Sh64 kwa lita kutoka Sh2,967 Februari hadi Sh2,903 mwezi huu.

Huku kwa upande wa dizeli kwenye mikoa hiyo imeshuka kwa Sh209 kutoka Sh3,340 Februari hadi Sh3,131 mwezi huu.

Utofauti wa bei katika mikoa inasababishwa na umbali wa usafirishaji wa mafuta kutoka bandarini na bandari ambayo mkoa husika unachukua mafuta hayo.

Kwa upande wa mafuta yanayoingia kupitia bandari ya Mtwara ambayo inahusisha mikoa ya kusini (Mtwara, Lindi na Ruvuma) bei ya mafuta ya petroli itaongezeka kwa Sh138 na ya dizeli itapungua kwa Sh68.

Bei hii inakuja baada ya Serikali kuondoa ruzuku ya mafuta ambayo ilikuwa inapunguza ukali wa bei hizo takribani miezi miwili iliyopita.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi