Lissu akirejea nasaha za wenyeviti wastaafu wa chama hicho, Bob Makani na Edwin Mtei amesema: “Haijawahi kutokea katika chama chetu kuwa uongozi wa juu umetolewa kama zawadi kwa mtu fulani…Huu ndio urithi tulioachiwa na wazee wetu.”
“Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kumekuwa na majaribio mengi, kutoka kwa baadhi ya wanachama na viongozi wa chama chetu ya kunishawishi kugombea nafasi ya mwenyekiti wa chama chetu,” amesema Lissu.
“Kwa sababu ya ufahamu wao wa historia hii, Mzee Mtei na Mzee Makani hawakutaka kukaa madarakani mpaka watakapolazimishwa kuondoka kwa aibu. Waliandaa utaratibu wa kuondoka madarakani kwa hiari yao na kwa kutumia taratibu za kikatiba.”
Amesema mara kadhaa amekuwa hana nia ya kuwania nafasi hiyo na katika kuonesha hilo Agosti 2024 aliwasilisha barua kwa Katibu Mkuu, John Mnyika kuonesha kusudio la kuwania umakamu mwenyekiti na kugombea urais katika uchaguzi ujao.
Lissu amesema amewasilisha barua kwa Katibu Mkuu ya kuonesha nia ya kuwania nafasi ya uenyekiti na kuondoa barua ya awali ya kuwania umakamu mwenyekiti.
Katika maelezo yake Lissu amesema:”Michuano mikali ambayo tumeishuhudia katika chaguzi za chama zinazoendelea ni ushahidi tosha kwamba chama kimekua. Katika mazingira haya, hatuna budi kurudisha tena utaratibu wa kikatiba wa ukomo wa madaraka katika chama tuliokuwa nao katika miaka ya mwanzo ya chama chetu.”
“Kuweka ukomo wa madaraka katika uongozi wa chama siyo tu utaondoa uwezekano wa viongozi wa chama kung’ang’ania madaraka, bali pia utawezesha kujengeka kwa utamaduni wa kuandaa viongozi wapya wa chama,” amesisitiza.
Huku akishangiliwa mara kadhaa na washiriki wa mkutano huo, Lissu amesema: “Muhimu kusisitiza mabadiliko yote haya ya uongozi wa juu wa chama yalifanyika kwa njia ya uchaguzi kwa mujibu wa katiba ya chama.”
“Haijatokea katika historia yote ya chama chetu kwamba uongozi wa juu wa chama chetu umetolewa kwa mwanachama yeyote kama zawadi au fadhila kutoka kwa kiongozi au viongozi walioko madarakani,” amesema Lissu.
Kwa mujibu wa Lissu, huo ndio urithi wa wazee na waanzilishi wa chama hicho, wanaopaswa kuuenzi na kuuendeleza.
“Kwa sababu hiyo, mwanachama wa Chadema au mtu mwingine yeyote anayeona ajabu au anayechukizwa na uamuzi wangu wa kutangaza nia ya kugombea nafasi ya uenyekiti wa chama chetu, atakuwa ama hajui, au amesahau au hataki kuenzi na kuendeleza urithi tulioachiwa na wazee wetu Edwin Mtei na Bob Makani wa kuachiana madaraka ya uongozi ndani ya chama kwa njia ya uchaguzi huru na wa haki,” amesema.
“Mtu wa aina hiyo anatakiwa kuelimishwa au kukumbushwa juu ya urithi huu, na kwa vyovyote vile asiruhusiwe kutuletea utamaduni tofauti katika kubadilishana madaraka na uongozi katika chama chetu,” amesema Lissu.
“Ukomo wa madaraka utapunguza sana, kama sio kuondoa kabisa, upambe na uchawa unaoshamiri pale viongozi wanapong’ang’ania madaraka katika mazingira yasiyokuwa na ukomo wa madaraka.”
Lissu ambaye kitaaluma ni mwanasheria amesema: “Ukomo wa madaraka kwa wabunge na madiwani wa viti maalum wanaotokana na chama chetu, utapanua fursa kwa wanachama wengi zaidi wa Bawacha kuwa wabunge na madiwani wa viti maalum na hivyo na wao kujengewa uzoefu na uwezo katika shughuli za kibunge na halmashauri za serikali za mitaa.”
Lissu amesema mabadiliko mengine ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi ni Katiba ya chama hicho hususan kwenye kusimamia Katiba ya chama:
“Ili kuweka mifumo mizuri na huru ya uchaguzi,” amesema Lissu.