Connect with us

Kitaifa

Trump ajitangazia ushindi, kura zaendelea kuhesabiwa

Florida. Mgombea urais wa Republican, Donald Trump amejitangazia ushindi katika uchaguzi wa Marekani alipokuwa akiwahutubia wafuasi wake waliojawa furaha huko Florida wakati kura katika majimbo muhimu zikiwa bado zinahesabiwa.

Hadi sasa, Trump amepata kura za majimbo 267 huku mpinzani wake, Kamala Harris akipata kura 224. Mshindi wa uchaguzi huo anatakiwa kupata kura 270, hivyo, Trump amebakisha kura tatu pekee za majimbo kuwa mshindi wa urais.

Kutokana na wingi wa kura hizo, Trump amewatangazia wafuasi wake ushindi huku akiongoza pia kwa kura za wananchi ambapo amepata kura 70,030,433 sawa na asilimia 51.21 wakati Harris akiwa amepata kura 64,712,777 sawa na asilimia 47.32.

Akizungumza huko West Palm Beach, Florida, ameuambia umati wa watu: “Angalia kilichotokea, inashangaza?” akiongeza: “Nataka kuwashukuru watu wa Marekani kwa heshima kubwa ya kuchaguliwa kuwa rais wenu wa 47.

“Nitawapigania nyinyi na familia zenu na mustakabali wenu, kila siku nitakuwa nawapigania kwa kila pumzi mwilini mwangu.”

Ameuambia umati huo kwamba ulikuwa “Ushindi wa ajabu kwa watu wa Marekani” huku akidai pia alikuwa ameshinda kura za wananchi, jambo ambalo alishindwa kulifikia wakati wa jitihada zake za urais mwaka 2016 na 2020.

“Kushinda kura za wananchi ilikuwa nzuri sana, ni hisia kubwa ya upendo,” alisema.

Matokeo ya mwisho ya uchaguzi bado hayajathibitishwa kwani majimbo tofauti bado hayajatangaza matokeo ya uchaguzi huo.

Wakati ushindi wa chama cha Republican katika Bunge la Seneti umethibitishwa, bado haujathibitishwa katika Bunge la Kitaifa licha ya kufanya vizuri.

Trump mwenye umri wa miaka 78 pia aliwaambia wafuasi wake kwamba “hii itakuwa kweli enzi ya dhahabu ya Marekani”.

Trump ameshinda katika majimbo muhimu ya Georgia, Pennsylvania na North Carolina – na anaongoza katika majimbo mengine kadhaa – akipunguza uhakika wa ushindi wa Kamala Harris kwa kiasi kikubwa.

“Tulishinda vizuizi ambavyo hakuna mtu aliyefikiria tungeweza,” Trump amesema wakati familia, ikiwa ni pamoja na mke wake, Melania na watoto wake, wakisimama karibu naye.

“Tutaisaidia nchi yetu ipone, tuna nchi inayohitaji msaada na inahitaji msaada mkubwa sana,” amesema huku akiongeza maradufu ahadi yake ya kukabiliana na wahamiaji haramu.

Trump basi amerejea jaribio la kuuawa kwenye mkutano huko Pennsylvania Julai 2024 akisema: “Watu wengi wameniambia kuwa Mungu ameokoa maisha yangu kwa sababu na sababu hiyo ilikuwa kuokoa nchi yetu na kuirejesha Marekani katika ukuu na sasa tutaenda kutimiza wajibu huo pamoja.”

Wakati huohuo, Kamala Harris sasa hatahutubia wafuasi wake hadi baadaye leo Jumatano, mwenyekiti wake wa kampeni amesema.

Makamu huyo wa Rais alikuwa anatarajiwa kutoa hotuba katika Chuo Kikuu cha Howard baada ya uchaguzi kufungwa, lakini hali ilizidi kuwa mbaya wakati matokeo yalipoanza kuingia.

Cedric Richmond, mwenyekiti mwenza wa kampeni ya Harris, ameuambia umati katika chuo hicho: “Tutaendelea usiku kucha kupigana ili kuhakikisha, kila kura inahesabiwa, kwamba kila sauti imezungumza.

“Kwa hiyo hautamsikia Makamu wa Rais usiku wa leo lakini kesho utamsikia. Atarudi hapa kesho.”

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi