Connect with us

Kitaifa

Polisi waimarisha ulinzi Dar, wafanya doria kila kona

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi linafanya doria jijini Dar es Salaam na viunga vyake kuanzia jana Septemba 20, 2024 askari wenye silaha wakiwa kwenye magari wakizunguka huku na kule.

Mbali ya magari yenye askari wakiwamo wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), pia kwenye baadhi ya maeneo wanazunguka na gari la maji maarufu washawasha.

Mwananchi leo Septemba 21, 2024 imeshuhudia katika maeneo mbalimbali kukiwa na doria, baadhi ya wananchi wakishangaa kuona hali hiyo inayohusishwa na maandamano yaliyotangazwa kufanyika Septemba 23, 2024 na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

 

Chadema ilitangaza maandamano hayo Septemba 12 kulaani matukio ya watu kutekwa na mauaji yakiwamo ya makada wake.

Licha ya polisi kuzuia maandamano hayo, Chadema imekuwa ikisisitiza kuwa yatafanyika.

Chadema Kanda ya Pwani kupitia ofisa habari wake, Gerva Lyenda imetangaza kuwa imeshawasilisha barua kulitaarifu Jeshi la Polisi kuhusu maandamano hayo.

Miongoni mwa maeneo ambayo Polisi wameweka doria ni Daraja la Juu la Kijazi, Ubungo ambako askari wapo tangu asubuhi.

Polisi wamekuwa wakifanya doria hadi eneo la Mbezi, Stendi ya Mabasi ya Magufuli, baadhi yakizunguka katika Barabara ya Mandela kwenda Buguruni na kurudi Ubungo. Polisi pia wameonekana wakifanya doria maeneo ya Mbagala.

Kauli ya Muliro

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alipoulizwa kuhusu doria hiyo ambayo imewaogopesha baadhi ya wananchi amesema:

“Labda wahalifu ndio wanaogopa, watu wema wanaogopa Polisi? Mbona mimi simu nyingi nilizopata za wananchi wanafurahi sana? Hao wanaoogopa ni kina nani? Mimi masomo yangu ya criminology (elimu ya jinai), mtu anayeogopa ni mhalifu,” amesema.

Kamanda Muliro amesema hali hiyo ni ya kawaida ya masuala ya kiusalama na wanataka waende nayo kwenye mfumo wa kata.

“Ni mfumo wa Jeshi kupeleka usalama mpaka kwenye kata,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu uendelevu wa doria hiyo, Kamanda Muliro amesema:

“Ni jambo la kawaida, watu wamekuwa wakipongeza karibu wiki mbili huko nyuma. Hii kazi imekuwa ikiendelea vizuri na tunataka tufike kwenye kata kule. Kata nyingi zimepata huduma, baadhi ya wapo polisi, baadhi yao wana pikipiki, lakini magari yakifika inakuwa vizuri zaidi.”

Kamanda Muliro alipoulizwa iwapo doria hiyo ni maandalizi ya kukabiliana na maandamano ya Chadema amesema:

“Tangu walipotangaza msimamo wa Jeshi la Polisi ulishatoka, tuna msemaji wetu wa Jeshi alisema maandamano yamepigwa marufuku.”

Akizungumzia msimamo wa Chadema wa kusisitiza maandamano hayo, Kamanda Muliro amesema:

“Sisi hatubishani kwa maneno, taasisi ya kijeshi ilishatoa msimamo wake na wao kama wana msimamo wao, hilo ni jambo lingine. Kikubwa ni kwamba hali ya usalama imekuwa ikiimarishwa siyo kwa sababu yao, ila watu wema lazima waendelee kuwa salama na wengine wote wenye shughuli halali lazima waendelee. Sasa tunafanyaje, tunaimarisha usalama.”

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi