Connect with us

Makala

Miti ilivyozalisha majina ya maeneo maarufu

Dar es Salaam. Miti ina faida chekwa. Kama ulidhani miti inatupatia kivuli, matunda na hata dawa pekee, utakuwa umekosea sana.

Miti ni zaidi ya hayo. Tanzania ina utamaduni wa kipekee hasa katika utoaji wa majina ya maeneo.

Utamaduni huu ni wa kutumia majina ya miti kuwakilisha maeneo. Ndio maana unaposikia maneno kama Mnazi Mmoja, Mkwajuni, Mwembeni, Mfenesini na mengineyo, jua asili ya eneo hilo ni kuwapo kwa miti aina aina hiyo.

Lakini pia kulikuwa na utamaduni wa kuinasibisha miti hiyo na kile kilichokuwa kikifanyika chini ya miti hiyo.

Kwa mfano, Mwembetogwa (sasa Faya katika jiji la  Dar es Salaam, chini ya mwembe huo eneo hilo kulikuwa na mtu akiuza togwa.Vile vile Magomeni Mwembe chai, kulikuwa na mtu akiuza chai chini ya mwembe huo.

Leo tunaangazia baadhi ya maeneo maarufu nchini ambayo asili ya majina yanayotaambulisha, imetokana na miti iliyokuwapo maeneo husika.

Mnazi Moja (Dar es Salaam)

Eneo hili maarufu kama viwanja vya Mnazi Mmoja lipo katikati ya Jiji la Dar es Salaam, lina historia ya aina yake kabla   na baada ya uhuru.

Ndilo eneo ambalo mkutano wa kwanza wa TANU ulifanyika hapo mwaka 1954.

Jina hilo lilitokana na mti wa mnazi uliobaki baada ya shamba la minazi la Mwarabu aliyeitwa Suleiman bin Ahmed lililokuwa eneo hilo kuungua moto na kubaki mnazi mmoja. Awali eneo hilo kabla ya kupandwa minazi, lilikuwa shamba la mpunga na mihogo likimilikiwa na bwenyenye aliyejulikana kwa jina la Mwinyi Gogo.

Mbuyuni (Dar es Salaam)

Huwezi kujisifu umefika Dar hasa Wilaya Kinondoni kama hujafika eneo liitwalo Mbuyuni. Tofauti na maeneo mengi ambayo yamechukua majina ya miti ambayo leo imepotea, eneo hilo  limechukua jina la mti wa mbuyu ambao  mpaka sasa bado upo.

Hata kulipotokea taarifa kuwa mti huo uliopo Barabara ya Ali Hassan Mwinyi ungekatwa kupisha barabara ya mabasi ya mwendo kasi, mjadala wake haukuwa mdogo kwenye mitandao ya kijamii.

Taarifa njema ni pale mamlaka husika zilipojitokeza na kueleza kuwa mti huo wenye alama ya kipekee katika eneo hilo, hautokatwa na ndivyo ilivyokuwa. Hatujui mabadiliko ya siku zijazo kama mti huo nao utakuja kuwa historia kwa kupigwa panga ama la.

Mijohoroni   (Kilimanjaro)  

Eneo hili lilijulikana zaidi kitaifa kufuatia sakata la kesi ya  mauaji ya mfanyabiashara wa madini, bilionea Erasto Msuya.

Ilielezwa kuwa bilionea Msuya aliuawa kwa risasi katika eneo hilo ambalo asili yake ni kuwepo kwa miti aina ya mijohoro.

Ni miti tiba inayotajwa kutibu maradhi kama vile homa za mara kwa mara.

Ni mti mzuri unaotajwa kuwa na kivuli na maeneo mengi hupandwa shuleni.

Mwembe Chai (Dar es Salaam)

Eneo jingine maarufu jijini Dar es Salaam ni Mwembechai lililopo Magomeni. Kwa mujibu wa mwenyeji wa Magomeni, Khamis Mnuta, anasema eneo hilo lilikuwa na mwembe na chini yake kulikuwa na mzee aliyekuwa akiuza chai chini ya mti.

Eneo hilo zamani anasema palikuwapo na kituo kikubwa cha mabasi yanayokwenda nje ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Ubungo

Ni moja ya wilaya tano za Mkoa wa Dar es Salaam, iliyoanzishwa kisheria mwaka 2015 baada ya kumegwa  maeneo ya Wilaya ya Kinondoni.

Historia inaonyesha katika eneo hili kulikuwa na pori lenye miti mingi ya jamii ya mibungo, hivyo kusababisha wenyeji kupaita Ubungo.

Mabungo ni aina ya matunda madogo ambayo kwa sasa ni nadra sana kupatikana kwani ni sehemu ya matunda pori.

Aghalabu ni matunda yenye uchachu hali inayofanya walaji wengi wayatumie sambamba na chumvi.

Utamaduni wa kutumia miti kuyapa majina maeneo, ni utamaduni wa maeneo mengi nchini, ndio maana kuna majina kama Mnazi Mmoja, Mwembeni, Mbuyuni na  Mkuyuni, yanapatikana katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Zanzibar kinara wa majina ya miti

Kama kuna eneo nchini lenye maeneo hususan mitaa inayotambulika kwa majina ya miti, kisiwa cha Unguja kinaweza kuongoza.

Unapozunguka karibu kila kona ya kisiwa hicho majina yaliyotamalaki yanatokana na miti.

Unguja imejaa majina kama Mfenesini, Mkunguni, Miembeni, Kikwajuni, Mtundani,  Michenzani, Migombani, Mtendeni, Misufini, Mkunazini, mbuyuni na mengineyo.

Zaidi ya hilo wenyeji wa Zanzibar wameonyesha utundu wa hali ya juu wa kuipa miti hiyo majina ya nyongeza, hali inayozidi kuyapa majina hayo mvuto.

Kwa mfano, majina kama Mwembeshauri, Mwembatanga, Mwembenjugu, Mwembebeni, Mwembeladu, Mwembe kisonge, Mwembe mchomeke, Mwembemimba, Mwembe makumbi, Mwembe matarumbeta; ni kiashiria tosha cha utunzi uliotukuka wa majina kwa wenyeji wa kisiwa hicho.

Miti mingine

Katika Jiji la Dar es Salaam na mingineyo majina ya maeneo yatokanayo na miti yamejaa.

Mathalani majina kama mikoroshini, mzambarauni, mkuyuni, mwembeni ni maarufu sana katika maeneo mbalimbali.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi