Connect with us

Kitaifa

Mbunge akerwa maudhui ya filamu, muziki ndani ya mabasi

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Najma Giga amesema mavazi ya nusu utupu na maudhui ya filamu na muziki yanayoonyeshwa ndani ya mabasi yaendayo mikoani yanakiuka maadili ya Kitanzania.

Amehoji iwapo Serikali haioni suala hilo ni kinyume cha sheria na tabia mbaya inayoporomosha maadili ya Kitanzania.

Katika swali la nyongeza bungeni leo Mei 21, 2024, Najma amesema kuna baadhi ya filamu ambazo watoto wa kiume wanaigiza kama vile wa kike.

“Basata (Baraza la Sanaa la Taifa) na Serikali hawaoni kwamba hilo linaweza kuchochea watoto wa kiume kuona kuwa wa kike ni jambo la kawaida,” amehoji Najma.

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma amesema kazi ya wasanii pamoja na mambo mengine ni kuburudisha na kwamba, wanaweza kuvaa uhusika wa namna yoyote.

Amesema wapo wasanii wameimba nyimbo na kuigiza ni madaktari na waganga wa kienyeji ili kuvaa uhusika.

Mwinjuma amesema suala la uhusika limekaa kimtego wa namna ya Serikali kulishughulikia.

“Tunaangalia tu kama litakuwa limezidi au linaakisi kulisukuma Taifa kufanya vitendo visivyofaa hapo tutachukua hatua,” amesema.

Amesema wanaendelea kufuatilia suala hilo kupitia Basata ili kuhakikisha maudhui yaliyo katika filamu na muziki hayakiuki maadili ya Mtanzania.

Mwinjuma amesema Serikali inachukua hatua kila wakati na kuelimisha.

Kuhusu swali kwamba tamaduni za kigeni zimetawala zaidi kwenye sanaa wakati jukumu la Basata ni kuhimiza na kukuza utamaduni wa Kitanzania, Naibu Waziri Mwinjuma amesema utandawazi na ukuaji wa teknolojia ni chanzo.

“Haya yamesababisha dunia kuwa kijiji hali inayotoa fursa kwa wasanii kupitia majukwaa ya kidijitali kuona mambo mbalimbali yanayofanyika duniani na kuyaiga, hivyo kuathiri sanaa ya Kitanzania,” amesema.

Amesema Basata linafanya kazi ya kufufua, kukuza na kuendeleza sanaa zenye asili ya Kitanzania kupitia programu mbalimbali zikiwamo sanaa mtaa kwa mtaa na Basata Vibes.

Pia kutoa elimu kwa wasanii kuhusu umuhimu wa kuzienzi tamaduni za Kitanzania kupitia kazi za sanaa, kushirikiana na wadau wa sanaa kuandaa matamasha yanayolenga kutangaza utamaduni.

Hata hivyo, amesema Basata linaendelea kuwachukulia hatua za kisheria wadau wa sanaa wanaokiuka kanuni za maadili.

Amesema Basata kwa kushirikiana na kamati maalumu, imetengeneza kivunge cha mtozi (Producers Kit) chenye vionjo zaidi ya 400 vya midundo ya makabila ya Kitanzania vitakavyowezesha wasanii kuvitumia.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi