Connect with us

Kitaifa

DC Rufiji aonya wananchi, maji kutoka Bwawa la Nyerere yakiongezeka

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, Meja Edward Gowele amewataka wananchi wilayani humo kuondoka kwenye maeneo yenye mafuriko na kutosogelea maji yanayoendelea kuongezeka kutoka bwawa la mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP).

Akizungumza na Mwananchi Digital kwa simu, Meja Gowele amesema:

“Tangu awali nilisema, watu walio mabondeni waondoke waende kwa ndugu, jamaa na marafiki na wale waliokosa pa kwenda tumewahifadhi shuleni,” amesema na kuongeza:

“Ndiyo maana tumepeleka taarifa Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa ili watupe maturubai ya kuwahifadhi wananchi.”

Hata hivyo, amesema tofauti na mafuriko ya miaka ya nyuma, ya mwaka huu yamedhibitiwa na bwawa la Julius Nyerere, vinginevyo hali ingekuwa mbaya.

“Haya mafuriko yamekuwepo kwa muda mrefu, mwaka 1968, miaka ya 1970 na 1980 na mwaka 2020. Hili bwawa limesaidia kuyapunguza tofauti na zamani,” amesema.

Gowele amesema, “Sisi tunawapa taarifa wananchi kuanzia ngazi ya kata, vijiji na vitongoji ili wahame. Suala la evacuation (uokozi) liko palepale, kipaumbele ni kuokoa maisha ya watu.”

Kwa upande wake, Meneja wa Tanesco Kanda ya Mashariki, Kenneth Boymanda amesema maelezo ya DC Gowele ndiyo mawasiliano waliyotoa.

“Chochote kinachoendelea mawasiliano yanafanyika katika ngazi ya wilaya. Kwa kadiri mvua inavyonyesha ndivyo maji yanavyozidi kuongezeka,” amesema.

Amesema inategemea mvua inavyonyesha kwenye mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ndivyo maji yanavyoshuka kuingia kwenye bwawa.

“Ikinyesha nyingi maji yanaongezeka, ikinyesha kidogo, maji yanapungua. Hata hapa Dar es Salaam jana (Aprili 6, 2024) mvua imenyesha siku nzima,” amesema.

Mhandisi Dismas Ngoto wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutoka bwawa la JNHPP Aprili 5, 2024 alipozungumza katika ziara ya Mkuu wa wilaya, kukagua madhara ya mafuriko katika Kijiji cha Mohoro alisema licha ya kuleta madhara kwa makazi ya watu na mazao, mafuriko ya mwaka huu hayajafikia ya mwaka 2020 kwa kuwa yamedhibitiwa.

Alisema walianza kufungua maji hayo Machi 5, 2024 na wanatarajia kuyafunga Mei 25, 2024.

“Hivi sasa maji yanayokuja katika bwawa la Nyerere ni mita za ujazo 8,300 sawa na lita milioni 8.3 kwa sekunde. Kama tusingeyazuia moja kwa moja madhara yake yangekuwa makubwa mno,” alisema.

Alisema mafuriko yaliyotokea mwaka 2020 yalikuwa mita za ujazo 7,000 sawa na lita milioni 7 kwa sekunde, na yalikuwa yanashuka.

“Maji yale yalileta madhara makubwa japo watu waliokoka. Sasa kama haya yangeachiwa yashuke moja kwa moja, madhara yake yangekuwa makubwa mno,” alisema.

Alisema kwa sasa wanayadhibiti maji hayo kwa kuyaachia mita za ujazo 3,000 hadi 6,000 kwa siku.

“Hii yote ni kutokana na mvua zilizotangazwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwamba zitakuwa kubwa, na si hapa tu, madhara yako nchi nzima. Sisi Tanesco tunasema pole, pole, pole sana,” alisema.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi