Kitaifa
Safari mpya ya mageuzi, siku 1,096 za Samia madarakani
Dar es Salaam.
“Hongera kwa maendeleo ya utawala wako, umekuwa champion (kinara) kwenye mageuzi ya kidemokrasia katika nchi hii na kwa njia hiyo tumeimarisha uhusiano wetu na leo ni sehemu ya kuimarishwa kwa uhusiano baina ya mataifa yetu mawili na chini ya uongozi wako.”
Hayo ni maneno ya Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris alipofanya ziara ya kiserikali nchini Machi 30 mwaka jana na kupokewa na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Kamala alimweleza Rais Samia kwamba anatambua amefungua milango ya kufanya kazi na vyama vya upinzani, ameondoa marufuku ya mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa, ameimarisha uhuru wa vyombo vya habari na amekuwa akishiriki makongamno ya demokrasia.
Maneno hayo yanaakisi namna Rais Samia alivyofanya mageuzi kwenye nyanya za kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutamaduni na maneno ya Kamala yanawakilisha mtazamo wa jumuiya ya kimataifa juu ya utawala wake.
Hapa nchini, wadau wa demokrasia wanachambua uimara na upungufu wa mageuzi yaliyofanywa na Rais Samia ndani ya miaka mitatu ya utawala wake.
Samia ametimiza siku 1096 tangu alipoapishwa kuwa Rais Machi 19, 2021, Ikulu ya Dar es Salaam, baada ya kifo cha mtangulizi wake, John Magufuli.
Mageuzi ya kisiasa
Moja ya mambo aliyoyafanya Rais Samia baada ya kuingia madarakani ni kufanya mageuzi ya kisiasa akilenga kuondoa vikwazo na siasa za chuki na kuingiza maridhiano, licha ya tofauti zao za kiitikadi.
Katika hilo alianzisha mazungumzo na vyama vya siasa nchini kupitia Baraza la Vyama vya Siasa na chama kikuu cha upinzani Chadema na aliunda Kikosi Kazi kilichokusanya maoni ya wananchi na kutoa mapendekezo ya namna ya kutatua changamoto zilizoibuliwa kuhusu demokrasia ya vyama vingi.
Baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa ni kuruhusiwa mikutano ya hadhara, ruzuku igawiwe sawa kwa vyama vyote, marekebisho yafanyike kwenye Tume ya Uchaguzi na mchakato wa kuandika Katiba mpya ukamilishwe.
Sehemu ya mapendekezo hayo yametekelezwa na Serikali ya Rais Samia, kama vile kuruhusu mikutano ya hadhara, maboresho ya Tume ya Uchaguzi, ingawa bado wadau wanadai hayajakidhi haja.
Kutokana na maboresho hayo, mwanazuoni katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST), Profesa Ambrose Kessy anaitafsiri miaka mitatu ya kiongozi huyo kuwa yenye mafanikio zaidi kuliko changamoto.
Profesa Kessy anasema ndani ya kipindi hicho, Rais Samia amerudisha uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa maoni na hata wa kukusanyika kupitia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.
Akitolea mfano, alisema hatua ya Rais Samia kuongoza kwa falsafa ya 4R (maridhiano, mabadiliko, ustahamilivu na kujenga upya) ni moja ya mafanikio ambayo yamewezesha majadiliano katika siasa na hata uchumi.
Profesa Kessy alisema mkuu huyo wa nchi ameonyesha uharaka wa kuchukua hatua dhidi ya mtendaji yeyote anayelalamikiwa na wananchi.
Kwa namna tofauti, hatua hiyo ya nia ya mabadiliko ya sheria inatazamwa na Conrad Masabo, wa idara ya Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwa inaakisi utashi wa kisiasa wa Rais aliyepo madarakani na jambo hilo ni moja ya mafanikio katika utendaji wake wa miaka mitatu.
Marekebisho ya sheria
Ndani ya kipindi hicho, yamefanyika marekebisho ya sheria tatu za uchaguzi, lengo likiwa ni kuweka mazingira mazuri ya kisiasa nchini na kujibu kiu ya wananchi wanaotaka kuona mabadiliko.
Sheria zilizotungwa na Bunge ni pamoja na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sheria ya Tume ya Uchaguzi na Sheria ya Vyama vya Siasa.
Hata hivyo, baadhi ya wadau kikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( Chedema) kuzikosoa wakisema marekebisho hayo hayajagusa msingi wa tatizo.
Chadema Ilianzisha maandamano nchi nzima kupinga sheria hizo ikidai kwamba suluhisho la kuwa na chaguzi huru na za haki ni kuwa na Katiba mpya ya wananchi itakayotoa mazingira ya usawa kwenye chaguzi.
Tayari chama hicho kimefanya maandamano katika majiji makubwa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha na hivi karibuni kimetanga kuanza awamu ya pili ya maandamano katika mikoa mbalimbali.
Abadili uelekeo Uviko-19
Wakati Rais Samia anaingia madarakani, ulimwengu ulikuwa unakabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19 na mataifa mbalimbali duniani yalichukua hatua kadhaa za kujikinga na ugonjwa huo ikiwemo kutangaza karantini na kutoa chanjo ya virusi hivyo.
Mtangulizi wake, Hayati Magufuli alikataa chanjo ya Uviko-19, hivyo hazikuruhusiwa kuingia nchini, hamasa kubwa ikawekwa kwenye matumizi ya dawa za miti shamba na kujifukiza kama njia ya kujitibu maradhi hayo.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya kuingia madarakani, Rais Samia alitangaza kuruhusu chanjo kuingizwa nchini na kuhamasisha wananchi kwenda kuchanja huku yeye mwenyewe akiwa mtu wa kwanza kupata chanjo hiyo.
Kwa hatua hiyo, Rais mteule wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko alisema uongozi wa awamu ya sita ulipoingia madarakani ulichukua matazamo wa kitaalamu, mawazo jumuishi na ushirikiano mpana na mashirika ya kimataifa kuruhusu chanjo na mikakati mtambuka kuelekea kuudhibiti ugonjwa huo.
“Aliendeleza jitihada za utafiti na utengenezaji wa chanjo hapa nchini zilizoasisiwa na mtangulizi wake. Alikabiliana na athari za Uviko-19 kwa hatua madhubuti zilizokubalika na wengi ndani na nje ya Tanzania,” anasema Dk Nkoronko.
Mageuzi ya kiuchumi
Mageuzi ya Samia hayajaishia katika siasa na afya pekee bali katika uchumi wa nchi kwa ujumla ukiangazia hatua za kufungua nchi kibiashara na uwekezaji.
Alisema katika utawala wake mwelekeo utakuwa kurudisha imani kwa wawekezaji na kutoa vivutio kwa wawekezaji mahiri ikiwa ni pamoja na kuwezesha uwekezaji kufanyika kwa haraka
Rais Samia alisema kutakuwa na sifa na matakwa maalumu yatakayowekwa kwa uwazi katika kutambua miradi ya kimkakati itakayostahiki vivutio vya kikodi au vivutio vingine. Suala la upatikanaji wa mitaji nalo halina budi kuangaliwa kwa umakini mkubwa.
Vilevile alisema Serikali yake inakusudia kufanya mageuzi ya kiutendaji kwenye mfumo wa utozaji na ukusanyaji wa kodi, kuweka mfumo utakaorahisisha na kuvutia walipa kodi, na kutengeneza wigo mpana zaidi wa walipa kodi ikilinganishwa na walipa kodi waliopo leo.
“Hivyo basi, kuna kila haja ya kutanua wigo wa walipa kodi, na vilevile, kuweka mifumo rafiki ya ulipaji na ukusanyaji wa kodi. Ningependa kuona wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi wanalipa kodi bila shuruti na matumizi ya nguvu, wakitambua kwamba kodi ni maendeleo yao,” alisema Rais Samia na kauli hiyo ilifurahiwa na jumuiya ya wafanyabiashara.
Ikiwa imepita miezi 16 tangu Novemba 2022, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, Uledi Mussa alisema Vikosi Kazi vilivyokuwa vinatumika kukukusanya kodi kwa mabavu vimeondolewa ili kuhakikisha kunakuwa na haki katika ukusanyaji mapato nchini.
“Kwa sasa tunakusanya mapato bila mabavu. Waachane kabisa kabisa na matumizi ya mabavu. Tunataka walipa kodi wajisikie vizuri kabisa. ,” alisema wakati akizungumza na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).
Aidha akilihutubia Bunge Rais Samia alisema uongozi wake una dhamiria kufanya mapitio na uchambuzi wa kina kwenye uendeshaji wa Mashirika ya Umma, akiwa na lengo la kuyafanya yaweze kujiendesha kwa faida.
Katika kutimiza kusudi hilo Desemba 15, 2023 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo alitangaza kuunganishwa kwa mashirika na taasisi 16 na kufuta mashirika na taasisi za umma nne, ili kuongeza tija katika utendaji kazi.
Kuvutia uwekezaji
Katika kipindi cha Machi 2021 hadi Machi 10, 2024, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi 1,188 sawa na ongezeko la asilimia 63.19 ikilinganishwa miradi 728 iliyosajiliwa katika kipindi kama hicho, Machi 2018 hadi Machi 10, 2021.
Kwa upande wa Ajira zilizozalishwa kutokana na usajili wa miradi kumekuwa na ongezeko la asilimia 231.63 kutoka ajira 104,172 zilizozalishwa kipindi cha miaka mitatu ya kuanzia mwaka 2018 mpaka 2021 mpaka ajira 345,464 zinazotarajiwa katika kipindi cha miaka mitatu ya awamu ya sita kuanzia Machi 2021 mpaka Machi 2024.
Thamani ya mitaji ya miradi ya uwekezaji iliyosajiliwa TIC kuanzia Machi 2021 hadi Machi 2024 ikilinganishwa kipindi kama hicho Machi 2018 hadi Machi 2021, imeongezeka kwa asilimia 137.5 kutoka Dola za Marekani 6.33 bilioni hadi Dola za Marekani 15.04 bilioni.
Akieleza kwa nini imekuwa hivyo, Mkurugenzi wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Adam Mihayo alisema katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan mengi yamefanyika na kwa ujumla wake yamerudisha imani kwa wawekezaji na kukuza biashara.
Mihayo ametoa kauli hiyo wakati akizungumza safari ya uongozi wa Rais Samia iliyoanza Machi 19, 2021 akisema mazingira ya kufanya biashara yameimarika, imani ya wawekezaji imeongezeka jambo ambalo linaonekana kupitia takwimu za uwekezaji nchini
Anasema Rais Samia amefanya kazi kubwa, ikiwa ni pamoja na kudumisha amani ambayo ikikosekana watu hawawezi kufanya shughuli za maendeleo.
“Kuna hatua za makusudi zimechukuliwa na Serikali ili kuhakikisha shughuli za kimaendeleo zinaimarika, bajeti yake katika miaka mitatu imekuwa ikiongezeka, sekta zinazoendesha uchumi zimekuwa zikitengenea fedha zaidi mwaka hadi mwaka,” aliema Mihayo.
Maridhiano yasambae
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza anasema Rais Samia alijitahidi katika hotuba yake ya kwanza, kwa kuanza na kauli za kuliunganisha Taifa, hata hivyo kuna mambo mawili ambayo bado hayako sawa.
Alitaja mambo hayo akisema, mosi, maridhiano ya kitaifa ni zaidi ya vyama kuridhiana, kuna makundi mengi katika utawala uliopita yaliparanganyika na yanahitaji kuridhiana.
“Kulikuwa na uhasama wa walipa kodi na watoza kodi, kulikuwa na uhasama wa wakulima na wafugaji, kuna uhasama kati ya vijana waliokosa ajira na Serikali yao.
Kwa hiyo, kuleta maridhiano ya vyama vya siasa ni sehemu ndogo ya kuliunganisha Taifa na bado kuna kazi ya kufanya na Rais anahitaji msaada,” alisema Askofu Bagonza
Pili, kiongozi huyo alisema, hata katika maridhiano ya kisiasa yamekwama, “pamoja na nia nzuuuuri ya mama, kuleta maridhiano ya kisiasa, bado amekwama na kwa maoni yangu amekwamishwa na mambo makuu mawili.
“Yeye ni chama na yeye ni Serikali, kwa hiyo anashindwa ajigaweje, lini awe chama na lini awe Serilakali, ni kazi kubwa na anahitaji msaada, namshauri asikate tamaa na kurudi mezani,” alisema
Askofu huyo alisema, upatanisho si wa siku moja. Sababu nyingine ni kwa sababu kilichosababisha mpalanganyiko wa kisiasa ni cha kisheria zaidi na Kikatiba kuliko mtu na mtu.
“Huwezi kuyatua matatizo ya kisheria kisiasa na huwezi kuyatatua matatizo ya kisiasa kwa kutumia sheria. Mimi ninachoona wamekwama kwenye eneo la kisheria na Katiba. Rais asaidiwe katika eneo hilo,” anasema.
Achukue hatua
Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashim Rungwe alisema utawala unalega kwenye kudhibiti ubadhilifu na usimamizi wa mali za umma lakini kila uchwao watu wanaiba na haoni hatua zinazochukuliwa.
“Rais Samia kazi yake kila siku kutujulisha watu wanaiba fedha zetu, lakini hakuna hatua anazochukua dhidi yao na utaratibu wao umekuwa wa ovyo tangu awamu zilizopita, tunajua wanakula hela,” anasema.
Anasema watu wanaofuja fedha hizo wamekuwa wakijenga majumba ya kifahari huku wananchi ambao ni wengi wakiambulia shombo kiasi cha kuendelea kujenga chuki.
“Angekuwa anachukua hatua tungeona lakini hakuna mtu hata mmoja aliyewahi kuchukuliwa hatua, amekuwa akiishia kusema wanaofanya hivyo wajitathimini kama wanaweza kuendana na kasi yake,” anasema.
Rungwe anaongeza hata tume zinazoundwa hawataki kushirikisha wadau kutoka vyama vingine, hivyo umekuwa ubaguzi ambao hauvumiliki kwa kushindwa kutambua kama wao ni Watanzania na wana uchungu na raslimali za nchi.
Matumizi makubwa
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Mendeleo (Chadema), John Mnyika alisema Rais Samia kwa muda aliodumu madarakani ameshindwa kuchukua hatua zakisera, kikodi na kiutendaji kubana matumizi ya Serikali ili kupunguza mzigo wa maisha magumu wanayopitia wananchi.
“Matokeo yake bei za bidhaa zimekuwa zikipanda kila mwaka tangu aingie madarakani, jambo linalozidi kuleta hali ngumu ya maisha kwa wananchi ni eneo ambalo anapokenda mbele anapaswa kulitazama,” anasema.
Mnyika anasema eneo la pili ni kasi ya ukuaji wa deni la Taifa ndani ya muda wake imekuwa kubwa, anapaswa kulidhibiti kwa kutokuendelea kukopa mikopo nje ya nchi ya kibiashara.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF)-Bara, Magdalena Sakaya alisema Rais Samia amejitahidi kujenga demokrasia kwa kuleta usawa wa kisiasa ndani ya nchi kwa kuamini hakuna chama chenye hatimiliki ya nchi.
“Ametoa vyama vya siasa kwenye kifungo cha miaka saba na akarejesha mikutano ya hadhara ambayo ni majukwaa ya watu kuzungumza na wamekuwa huru kutoa maoni bila bughudha,” alisema.
Sakaya anataja eneo aliloshindwa kulitendea haki kudhibiti uwajibikaji kwa watendaji wa ofisi za umma, wananchi wamekuwa wakipitia wakati mgumu kupata huduma.
“Ukienda kwenye hospitali, vituo vya afya, ofisi za ardhi hali ni mbaya. Mfano mwenyewe nina miaka minne sasa nafuatilia hati yangu sijapata, unaenda wanakuzungusha kupita maelezo,” anasema.
Anasema watendaji wote wamegeuka machawa kila jambo kusifia na wamekuwa wakinehemeka na mishahara ya bure bila kufanya kazi na kuzidisha hasira kwa wananchi.