Kitaifa
Siri wengi kutaka mabosi wanaume maeneo ya kazi
Dar es Salaam. Ripoti mpya iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha kuwa, waajiriwa wengi wanapenda kuwa na viongozi wanaume kuliko wanawake.
Ripoti hiyo iliyopewa jina la Social Institution and Gender Index (Sigi Tanzania) ya mwaka 2021 inaonyesha, asilimia 32.9 ya watu wanapenda kuongozwa na mwanaume, huku asilimia 23.9 wakipenda mabosi wanawake.
Miongoni mwa sababu zilizotajwa katika utafiti huo zinazofanya mwanaume kupewa nafasi kubwa ni kujiamini, kuwa na uongozi na usimamizi bora.
Hata hivyo, wadau wanaeleza kuwa, tatizo kubwa linaloonekana ni mitazamo hasi ya jamii juu ya kuongozwa na wanawake, huku wengine wakieleza kuwa mfumo dume bado umetawala.
Aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Kijo Bisimba alisema kinachochangia hali hiyo ni mitazamo ambayo bado iko miongoni mwa jamii na kuamini katika mfumo dume ambayo inapaswa kushughulikiwa.
Hiyo ni kutokana na kule alichoeleza kuwa wapo wanawake wenye uwezo wa kuongoza na kufanya vizuri lakini baadhi ya watu wameshatishwa kuwa ni ngumu kufanya kazi na jinsi hiyo jambo ambalo si la kweli.
“Wakati nakua Mkurugenzi nilihangaika sana kupata katibu muhtasi, nilipompata na kufanya naye kazi kwa muda alikuja kuniambia alitishwa kuwa kufanya kazi na mwanamke ni ngumu jambo ambalo si la kweli.
“Watu wanazungumza kwa mitazamo zaidi kuliko uhalisia, inabidi kupambana na mfumo huu ndani ya jamii kuanzia ngazi ya familia kwa kufundisha watoto wanatakiwa kuishi vipi,” alisema Dk Bisimba.
Mkurugenzi wa Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA), Tike Mwambikile alisema kwa kawaida, jamii bado inamtambua mwanaume kama kiongozi kuliko mwanamke.
“Hivyo namba hii inaonyesha kuwa jamii imeanza kumtambua mwanamke kuwa anaweza kuongoza, tuendelee kuonyesha uzuri wa wanawake viongozi na kuonyesha kuwa wanaweza kuwa bora na kufanya kazi kubwa.
“Bado changamoto zitakuwepo ambazo haziwezi kuepukika kwani wanaume wamekuwa viongozi kwa muda mrefu na wanajua vitu vingi,” alisema.
Alisema kinachoonekana sasa ni kiashiria cha kupiga hatua kwa kile alichokieleza kuwa kuna wakati ambao wanawake viongozi hawakuwapo kabisa lakini akisema kilichopo sasa ni mwelekeo mzuri
Akizungumzia utafiti huo, mhadhiri wa elimu maalumu na saikolojia kutoka Chuo Kikuu Huria (OUT), Dk Cosmas Mnyanyi alisema kiongozi bora huweza kumfanya mfanyakazi afanye kazi kwa ari na kuchukulia kile anachokifanya ni ‘chetu’.
Alisema kiongozi akijenga mazingira bora kwa wafanyakazi bora nao hawatakuwa tayari kumuangusha yeye wala taasisi wanayoitumikia.
“Hili linaanzia katika ustawi mara nyingi katika sehemu ambayo ustawi uko chini ufanisi unakuwa mdogo. Kama kiongozi anatakiwa kutambua changamoto iliyopo na ashirikishe wafanyakazi ili wachangie mawazo na kutatua,” alisema.
Methodolojia
Ripoti hiyo imefanyika chini ya NBS, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS) kupitia usaidizi wa UN Women Tanzania na Organisation for Economic Co-operation and Development (OECD) Development Centre.
Jumla ya watu 7,068 walio na miaka 15 na kuendelea walitumika kufanya utafiti huu ambapo kati yake 3,848 ni wanawake na 3,220 ni wanaume. Asilimia 97 ya waliohojiwa walitoka Tanzania Bara na asilimia watatu walitokea Zanzibar.
Hata hivyo, wakati mchanganuo wa watumishi waliochagua jinsi ipi wanapendezwa kuongozwa nayo, asilimia 40 ya watu nchini walionyesha kuwa tayari kufanya kazi na bosi wa jinsi yoyote.
Wakati takwimu zikionyesha kuwa kila jinsi inajipendelea katika uongozi, wanaume wanaongoza kwa kuhitaji kuongozwa na wanaume wenzao kuliko wanawake.
Asilimia 41 ya wanaume walio na umri wa kuanzia miaka 15 na kuendelea, wanapendelea kufanya kazi na wanaume wenzao, huku asilimia 15 wakitamani kufanya kazi na wanawake.
Wakati kwa upande wa wanawake, asilimia 33.5 walio katika umri sawa na wanaume, ndiyo wanapenda kuwa na mabosi wanawake huku asilimia 25 wakiwapa wanaume.
Utafiti huo unaonyesha kuwa asilimia 70 ya watu waliochagua kuongozwa na mabosi wanaume wametaja sifa kuwa wanaume ni viongozi bora na wana usimamizi mzuri.
Katika upande wa waliochagua wanawake viongozi, walisema wanawake pia wana uongozi bora na usimamizi, huku matumizi bora ya pesa pia yakitajwa kwa kiasi kidogo.
Matokeo ya ripoti hiyo ya ‘Sigi Tanzania’ yanaendana na hali halisi ambayo ipo katika maisha ya kawaida kwenye jamii ambapo wanaume wanatawala katika ngazi za maamuzi na uongozi kuliko wanawake.
Takwimu za ripoti ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) inayoitwa ‘Uwakilishi wa Wanawake katika Uongozi na Nafasi za Kufanya Maamuzi Tanzania, 2005-2020’ zinazoonyesha bado wanawake wanazidi kuwa wachache katika nafasi za uongozi na kufanya maamuzi.
Ripoti hiyo imeonyesha nafasi ndogo ya wanawake kwenye idara zinazosimamiwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kuanzia mwaka 2007 hadi 2019, ambapo katika nafasi za utendaji wanawake walikuwa asilimia 29 ikilinganishwa na wanaume asilimia 71, wakuu wa idara wanawake walikuwa asilimia 17 huku wanaume wakiwa asilimia 83 na wakuu wasaidizi wa idara, uwakilishi wa wanawake ulikuwa asilimia 23 huku wa wanaume ukiwa asilimia 77.
Kwa upande wa wakuu wa mikoa, ripoti hiyo ya TGNP inaonyesha, mwaka 2015 asilimia 37 ya wakuu wa mikoa walikuwa wanawake na kuanzia mwaka 2016 hadi 2020 kiwango hicho kilishuka hadi asilimia 19.
Hali inazidi kuwa mbaya zaidi katika upande wa mahakama ambapo majaji wanawake wa Mahakama Kuu wanazidi kupungua kadri miaka inavyoenda.
“Mwaka 2016 majaji wanawake walikuwa asilimia 47, mwaka 2017 ilipungua kidogo hadi asilimia 44, mwaka 2018 idadi ilizidi kupungua na kufika asilimia 35 kabla ya kushuka tena hadi asilimia 29 kwa kipindi cha miaka miwili (2019 hadi 2020),”ilisema sehemu ya ripoti hiyo.
Wasemavyo wadau
Joel Peter ambaye ni bodaboda alisema kwa upande wake kufanya kazi na mwanaume mwenzake kunampa uhuru zaidi wa kuomba usaidizi inapotokea kuliko mwanamke.
“Mwanaume ni rahisi sana kukuelewa ukimuambia kitu, kama nina tatizo naweza kumfuta na kumuambia tofauti na mwanamke, kwanza mpaka umzoee kiasi cha kumuambia matatizo yako ni ngumu,’’ alisema.
Janeth Kimaro ambaye ni mfanyakazi wa ofisini alisema mabosi wanawake mara nyingi wamekuwa hawataki kuona wafanyakazi hususani wa kike walio chini yao wanasifiwa au kufanikiwa.
“Kuna ile wanawake kutopendana, unaweza kudhani inasemwa tu lakini kiuhalisia ipo, hatupendi kuona mwenzako anasifiwa wakati yuko chini yako kwa hiyo inakuwa ngumu,” alisema Janeth.
Maoni yake hayatofautiani na ya Prisca Pishon ambaye anasema wakati mwingine wanawake wanashindwa kutofautisha karaha za nyumbani na kazi jambo ambalo huweza kuathiri utendaji.
“Mtu akikwazwa nyumbani anakuja na hasira zake hadi kazini, au anaweza kuamka hajisikii kuongea na mtu, hapo hamuwezi kufanya kazi,” alisema Prisca.
Maoni hayo yalienda mbali hadi kwa walimu ambapo walidai kuwa na mkuu wa shule mwanaume ni vyema kuliko mwanamke huku wakieleza kuwa si watu wa kuchimbua vitu na wanaelewa kwa haraka.
Hata katika sehemu za huduma kama baa, wanawake wengi wanapenda kuhudumiwa na wanaume huku wanaume wakihitaji huduma za wanawake.
Utawala Tanzania
Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi, sasa Tanzania inaongozwa na Rais mwanamke, Samia Suluhu Hassan na mhimili wa Bunge nao unaongozwa na Spika, Dk Tulia Ackson.
Mbali na wao, pia idadi ya wakuu wa mikoa wanawake imeongezeka kutoka asilimia 10 mwaka 2005 hadi asilimia 23 mwaka 2022, huku wakuu wa wilaya wakiongezeka kutoka asilimia 19 hadi asilimia 25 huo huo.
Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu aliposhiriki kongamano la nne la Wanawake Vijana wa Mtandao wa Viongozi Afrika lililofanyika visiwani Zanzibar, Desemba mwaka jana.
“Idadi ya wanawake katika vyombo vya maamuzi imeongezeka na inakaribia kufikia nusu wabunge Tanzania [wabunge wanawake] wameongezeka kutoka asilimia 21.5 mwaka 2005 hadi asilimia 37 mwaka 2022,” alisema Samia.
Alisema anataka kuona wanawake wakiingia kwenye masoko ya kikanda na kuyatumia masoko hayo kama hatua ya kwenda mbali zaidi hadi kwenye masoko ya nje.
Lakini wakati matamanio yake ni kuona idadi ya wanawake katika uongozi ikikua, kwa wananchi bado ni tofauti hasa inapofika wakati wa kuchagua wawakilishi bungeni.
Kwa mujibu wa kitabu cha kumbukumbu ya wabunge toleo la sita kilicotolewa Februari, 2022, idadi wa wabunge waliopo ni 392 huku wale wa majimbo (kuchaguliwa) wakiwa ni 264.
Kati ya wabunge hao, majimbo 27 pekee ndiyo yanayoongozwa na wanawake huku mengine yakiongozwa na wanaume.
Idadi ya wanawake bungeni inaongezwa zaidi na viti maalumu ambao wapo 113 kutoka vyama tofauti nchini.
Lakini hali hii huenda ikawa bado ni hatua za awali za kuisogelea 50 kwa 50 kwani kuongozwa na wanaume ni kitu ambacho kimekuwapo tangu enzi na enzi.
Kabla ya kuwapo na serikali, jamii za Tanzania kupitia makabila tofauti zilikuwa zikiongozwa na machifu ambao walikuwa ni wanaume.
Wanaume pia katika ngazi ya familia bado wanaonekana kupewa nafasi kubwa ya uongozi kama kichwa cha familia, huku mama akiwa msaidizi wake jambo ambalo limeendelea kurithishwa vizazi na vizazi.
Sheikh Ponda Issa Ponda alisema kwa mtazamo wa dini, baadhi ya watu walipewa uwezo wa kuelewa mambo zaidi ya wengine huku akitaja jinsia kuwa na mchango mkubwa.
“Haimaanishi kubagua au kukandamiza watu, kuna nafasi ambazo zinaweza kushikwa na wanawake, wakati mwingine wanaweza kuzishika hata kwa dharula na wakafanya vizuri lakini mwanaume bado anapewa nafasi kubwa,’’ alisema.
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Dk Charles Kitima, alisema kinachotegemewa ni uwezo wa mtu wa kufanya kazi za uongozi husika, huku akiwa ametayarishwa kitaaluma na ukomavu wa kuonyesha watu dira kufikia malengo ya taasisi husika. Alisema mila na desturi za kidunia na utawala katika ngazi za juu zamani ulikuwa ukitegemea sana majeshi katika kuundwa kwake ndiyo maana wanaume walipewa jukumu kubwa.
“Kinamama wana uwezo mkubwa wa kiuongozi, katika historia duniani kinamama wachache sana waliokuwa wanaongoza nchi ndiyo wameingia katika matatizo ya kuvuruga amani lakini mara zote wamekuwa wapatanishi, watafuta amani na watu wanaohubiri mshikamano,’’ alisema.