Connect with us

Kitaifa

Panga pangua vigogo Dart, Udart yawaibua wadau

Dar es Salaam. Licha ya kupatikana kwa uongozi mpya wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart) na Wakala wake (Dart), wadau wameonyesha shaka, wakieleza uwezekano wa utenguzi wa mabosi hao kuendelea kutokana na uhalisia wa huduma.

Wadau hao wamesema kuendelea kwa utenguzi na uteuzi mpya wa mabosi wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart) na Udart, kutatokana na mzigo mkubwa ambao taasisi hizo zimejitwisha.

Kauli hizo za wadau wa usafirishaji zinakuja siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya mabadiliko ya Mkurugenzi Mkuu wa Udart ikiwa ni miezi sita tangu alipofanya mabadiliko kama hayo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka aliyoitoa leo Jumamosi, Machi 9, 2024 mabadiliko hayo yanahusisha uteuzi wa Waziri Kindamba kuwa Mkurugenzi wa Udart akichukua nafasi ya Gilliard Ngewe atakayepagiwa kazi nyingine.

Hata hivyo, miezi mitatu iliyopita Januari 15, 2024, Rais Samia alifanya mabadiliko ya uongozi Dart akimteuwa Dk Athuman Kihamia kuwa Mtendaji Mkuu, akimrithi Dk Edwin Mhede. Wote waliwekwa kando ilielezwa watapangiwa kazi zingine.

Viongozi hao wapya wa Dart na Dart wanaingia kipindi ambacho kuna wingi wa malalamiko yanayohusu huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka, Dar es Salaam hasa kutokana na uhaba wa mabasi.

Kulingana na wadau sio kwamba waliowahi kuteuliwa hawana uwezo, bali wamezitwisha taasisi hizo mzigo ulio nje ya uwezo wake.

Mradi wa mabasi Mbagala miundombinu ya vituo na barabara umekwisha kamilika lakini huduma hazijaanza zaidi ya miezi mitatu.

Mabadiliko mabosi Dart, Udart

Oktoba 24, mwaka jana, Gilliard Ngewe alitambulishwa kuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Udart), akichukua nafasi ya John Nguya aliyekuwa Mkurugenzi wa pili tangu kampuni hiyo ilipoanzishwa mwaka 2016. Wa kwanza alikuwa Charles Newe.

Kwa jumla Ngewe amehudumu nafasi ya ukurugenzi wa Udart kwa miezi sita hadi leo Jumamosi, Rais Samia alipomteuwa Waziri Kindamba kuwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo.

Kindamba anaukwaa wadhifa huo, akitokea kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, nafasi aliyohudumu kwa mwaka mmoja, tangu Februari 26, mwaka jana.

 Kindamba amewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).

Kwa upande wa Dart, aliyeanza kuwa Mkurugenzi ni Ronald Rwakatare tangu mwaka 2016, miaka mitano baadaye Mei 15, 2021 nafasi yake ilirithiwa na Dk Edwin Mhede.

Dk Mhede alihudumu katika wadhifa huo hadi Januari 15, mwaka huu pale mamlaka ya uteuzi ilipokabidhi mikoba ya bosi wa Dart kwa Dk Athuman Kihamia.

Kwa maneno mengine kampuni na wakala huo kwa sasa zipo chini ya viongozi wapya, walioteuliwa wakipishana miezi mitatu.

Dk Kihamia aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) aliteuliwa Januari 15, mwaka huu kuwa Mkurugenzi mpya wa Dart na Kindamba aliteuliwa jana kuwa mkuu wa Udart.

Uongozi mpya utakuwa suluhu?

Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (Darcoboa), Shifwaya Lema amesema licha ya mabadiliko ya viongozi hao, kuna uwezekano utenguzi ukaendelea kushuhudiwa.

Ameeleza hilo litatokea iwapo wateule wapya katika taasisi hizo, hawatajifunza kutoka kwenye makosa ya watangulizi wao.

Kwa mtazamo wa Lema, kinachosababisha mdororo wa huduma katika usafiri huo ni mzigo mkubwa ambao Dart na Udart zimejitwisha.

Mzigo huo unatokana na kile alichoeleza, taasisi hizo zimekiuka utaratibu kwa kuanzisha huduma katika maeneo mengine, ilhali yake zinayopaswa kuyahudumia hazijakidhi haja.

“Shida wanakiuka utaratibu, walipaswa kutoa huduma Kimara, Morocco, Gerezani, Kivukoni lakini wameanza kwenda Mbezi hatimaye Kibaha ilhali bado kwenye maeneo hayo hawajakidhi,” amesema.

Kufanya hivyo, amesema ni sawa na kujitwisha mzigo usioweza kuubeba na kwamba hapo ndipo shida inapoanzia.

Ameeleza huduma za mabasi hayo kutokana na uhalisia wa miundombinu na uwezo wa Taasisi hizo, zilipaswa kuishia kwenye maeneo waliyopaswa kabla ya kuamua kwenda kwingineko.

“Naamini tutaendelea kuona wakitenguliwa kama hawatajifunza kutoka kwa wale waliotangulia. Mabasi yenyewe mengi yameharibika unapoongeza eneo la kuhudumia hutaweza,” amesisitiza.

Hata hivyo, ameeleza hakukuwa na haja ya kuongeza maeneo hayo ilhali kuna daladala za kutosha kuendelea kusogeza abiria hadi vilipo vituo vya Mwendokasi.

Mtazamo kama huo, alikuwa nao Mwenyekiti wa Madereva wa Mabasi Tanzania (Uwamada), Majura Kafumu aliyesema mabadilimo ya uongozi hayatakuwa chochote kama wateuliwa hawatabadili maono.

Hadi unafikiwa uamuzi wa kutenguliwa, amesema maana yake mkuu wa nchi hakuridhishwa na utendaji.

Lakini, ameeleza Dart na Udart zimeshindwa kukidhi huduma za usafirishaji katika ngazi zote.

“Wamefeli kwanza wakati wanajenga awamu ya kwanza, wanatengeneza boksi ambalo gari ya mbele ikiharibika za nyuma zinashindwa kupita. Angalau hilo wamerekebisha.

“Katika uteuzi huu tuwaombee wawe na maono mbadala yatakayosaidia usafiri wa mwendokasi ufanye kazi katika ufanisi,” amesema Kafumu.

Amesema kwa sasa mradi huo unahodhi barabara za mjini na Daladala zimeminywa kuingia huko.

“Unahodhi vipi maeneo ilhali haukidhi huduma, hawa wanashida sana,” alisema.

Ili kupata suluhu, alisema kampuni hizo zinapaswa kushirikisha wadau kwenye uamuzi wowote, badala ya kufanya kazi kama watawala.

“Lazima wawashirikishe walaji. Lakini kama tunataka kupata suluhu ya msongamano wa magari ni kupanua barabara, tuache mfumo wa njia mbili zianzie nne,” alisema.

Malalamiko ya huduma

Mzizi wa kuanzishwa kwa Dart na Udart ni kusimamia na kutoa huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka katika Jiji la Dar es Salaam.

Lakini shabaha kuu ya huduma hiyo ni kupunguza msongamano wa daladala katika Jiji hilo, kadhalika kurahisisha usafirishaji wa abiria.

Tangu kuanzishwa kwake, huduma za usafiri huo zimegubikwa na malalamiko kutoka kwa abiria na uhaba wa mabasi ndilo lililokuwa lalamiko kubwa zaidi.

Msingi wa malalamiko yao, ilikuwa ni kusongamana kwa abiria muda mrefu vituoni bila kupata huduma hususan nyakati za asubuhi na jioni, kadhalika baadhi ya mabasi yalionekana wakishusha abiria na kuondoka bila kupakia wengine.

Oktoba 10, mwaka 2018 aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo aliweka wazi juu ya utendaji usioridhisha ndani ya Dart.

“Jambo hili katika ofisi yangu halitutii amani kabisa. Kutokana na hilo, Rais Magufuli ameridhia kutenguliwa kwa Mtendaji Mkuu wa Dart, Ronald Rwakatare na nafasi yake itachukuliwa na Leonard Kapongo,” alisema Jafo.

Hata hivyo, dakika 10 baadaye Jafo alitangaza mabadiliko katika uamuzi huo, akisema Rwakatare ataendelea na wadhifa wake lakini ajitathmini.

Hata, Mohammed Mchengerwa naye katika uongozi wake ndani ya Tamisemi, alionyesha kusikia malalamiko dhidi ya mradi huo.

Katika maelekezo yake Oktoba 25, mwaka jana, alisema: “Sitaki nisikie kuna mabasi yametelekezwa, yarekebishwe mabasi yote yaingie kutoa huduma.

“Ndoto za Rais, Watanzania wawe na furaha, watumiaji mwendo kasi wawe na furaha wasibugudhiwe.

“Msimamie mtoa huduma Udart kelele zimekua nyingi hatutaki watu wababaishaji, hawafuati ratiba na kusababisha mrundikano vituoni Mwendokasi iwe chini ya nusu saa,” alisema.

Mabosi hao ni kina nani?

Wawili hao si mara ya kwanza kutokeza katika nafasi za uteuzi, wote wamewahi kushika nafasi mbalimbali katika awamu tofauti za uongozi.

Kindamba kwa mara ya kwanza alichomoza katika nafasi za uteuzi, Septemba 23, mwaka 2016 Rais wa wakati huo, John Magufuli alipomteuwa kukaimu wadhifa wa Mkurugenzi wa Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL).

Baadaye Julai 6, 2017 aliteuliwa kushika wadhifa huo, badala ya kukaimu na alihudumu kwa miaka takriban saba hadi Machi 14, mwaka 2022 alipompisha Peter Ulanga.

Baada ya TTCL, Kindamba akateuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe na baadaye kuhamisha Tanga.

Dk Kihamia naye hakuanzia Dart. Kabla ya hapo alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha tangu Mei 30, 2021.

Si wadhifa huo tu, Dk Kihamia aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, lakini kubwa zaidi aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuanzia Julai 10, 2018.

Wadhifa wake ndani ya NEC ulikoma baada ya kuhudumu kwa siku 457 hadi Oktoba 1, 2019 aliporithiwa na Dk Charles Mahela.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi