Connect with us

Makala

Sababu wanaofariki wakiongezwa makalio zatajwa

kurekebisha maumbile nchini, wametaja sababu tatu zinazoweza kusababisha anayepatiwa huduma ya kuongeza shepu na makalio kufariki dunia.

Sababu hizo zimetajwa kuwa ni hali ya kiafya ya mteja husika, utaalamu wa watoa huduma na mazingira yaliyopo wakati na baada ya upasuaji.

Wataalamu hao wamesema hayo jana Alhamisi, Novemba 2023 ikiwa ni siku chache tangu kutolewa taarifa kuhusu watu wengi wanaokwenda nchini Uturuki kuongeza makalio na shepu kufariki dunia wakipatiwa huduma au baada.

Ripoti ya upasuaji wa kurekebisha maumbile ya mwaka 2023 iliyofanywa nchini Marekani na tovuti ya ‘Research and Market’ inaonyesha asilimia 42.7 ya waliofanyiwa upasuaji huo walipata madhara ikiwamo kifo.

Takwimu hizi zinaonyesha takribani nusu ya wote waliofanyiwa upasuaji wa kurekebisha maumbile hupata madhara hasi.

Daktari bingwa wa upasuaji wa kurekebisha maumbile wa Hospitali ya Aga Khan, Aidan Njau akizungumza na Mwananchi Digital amesema mgonjwa mwenyewe namna anavyochagua akapate huduma wapi, anayetakiwa kumfanyia huduma na baada ya upasuaji ni vitu vya msingi kabla ya kufanya uamuzi.

“Ukiangalia soko la huduma hiyo kwa sasa linahamia Uturuki ukilinganisha na sehemu nyingine kama India na kwingineko, inaelezwa gharama ni za chini zaidi, utalaamu na mazingira,” anasema na kuongeza:

“Lakini sasa mtu ana hali gani kiafya? anaweza kuwa na matatizo ya moyo, figo, magonjwa mengine ambayo sawa hayana mahusiano ya karibu na kile alichokifuata, maana amekwenda pale kutaka kurekebisha maumbile yake, lakini anaweza kuwa na umri mkubwa, kisukari, presha na magonjwa kama hayo.”

Dk Njau amesema anapofanyiwa upasuaji na tayari ana matatizo mengine hawezi kuangaliwa kwa maana wao wanaangalia kipato kwa kile alichokifuata.

“Hospitali inaingiza kipato, nchi pia inaingiza kipato sababu ni utalii wa matibabu. Huduma hiyo ni ndefu, ikileta changamoto hasa kwa matatizo mengine, nafasi ya kusogelea kifo inakua kubwa zaidi,” amesema.

Dk Njau amesisitiza utaalamu ni kitu cha pili muhimu zaidi katika huduma za urekebishaji maumbile. Amesema kwa mzoefu anafanya vizuri zaidi tofauti na wanaojifunza mitandaoni au hawana utaalamu husika, bali wanatafuta fedha.

“Ni mbaya, ni ukweli lazima tuseme, wengi sasa hivi wanatafuta mtandaoni watu hawajui bila kujua mitandao inaweka kila kitu anaingia huko na kuanza kuwasiliana na watu asiowajua, wala utaalamu walionao, wala uzoefu,” amesema.

Anasema upasuaji huo unahitaji mtu anayejua nini anafanya na ana uzoefu mkubwa.

“Anaweza kukosea yakatokea makosa ya kibinadamu yakasababisha kifo au madhara pamoja na kwamba teknolojia ipo juu kuliko sisi, lakini bado kuna suala la utaalamu, vifaa, dawa na vingine,” amesema.

Ameeleza suala la mazingira mtu anapokwenda nchi za watu wengine kufuata huduma mara nyingi hufikia hotelini na hana ndugu wala watu wa karibu, jambo linalochangia wengi kupata maambukizi.

“Wengi hukwepa gharama, kuna watu wanakuwa kama mawakala wanawapeleka kule wanawekwa kwenye hoteli au nyumba moja wanawekewa mpishi. Sasa kuna huduma zinahitajika kuangalia kidonda kuhakikisha unapata dawa inavyohitajika,” amesema na kuongeza:

“Mazingira yanatakiwa kuwa masafi, sasa kutokana na foleni na gharama unakaa siku mbili au moja hospitali unarudi hotelini kule huna mwangalizi, mazingira mabovu, nafasi ya kupata maambukizi ni kubwa ikitokea shida ni ngumu kulalamika, wao ni wahudumu wa hoteli tu,” amesema.

Dk Njau amesema gharama za upasuaji huo nje ya nchi ni kubwa kwa kuanzia nauli ya ndege, kulala hotelini, mizunguko na gharama za huduma, mtu wa kuongozana naye au kutokuwa na ndugu na bado wakirudi wanapata changamoto.

Anasema, “Wanaporudi wengi wanapata athari, wanakuja Aga Khan wana vidonda ambavyo vimeharibika na vingine vinakuwa na usaha inabidi turudie upya na wengine vinavilia damu, inahatarisha maisha yake na ile shepu ambayo alikuwa anaihitaji haipati tena.”

“Hawa wengi wakimpigia daktari wake hawapati mawasiliano na wakati mwingine daktari anamkimbia, kurudi kule hawezi anapata wapi tena Sh20 milioni ya kurudi,” anahoji.

Daktari bingwa wa kurekebisha maumbile katika Hospitali ya Muhimbili-Upanga, Dk Lauren Rwanyuma amesema wakati mwingine upasuaji unaweza kuwa ndivyo sivyo na matokeo yaliyotarajiwa yasipatikane.

“Akiwa na bahati matokeo yake shepu ya mwili ikawa kubwa au ndogo tofauti na matarajio, lakini kama ana bahati mbaya anapoteza maisha na hii sababu kubwa ni utaalamu duni. Kuna wengine nyama zinagoma kuungana na kukaa katika hali ya kawaida na nzuri, hivyo kuwalazimu kufanya upasuaji mwingine, hali hiyo inaweza kuchangiwa na umri,” amesema.

Dk Rwanyuma amesema ni vyema mhusika akawa makini kufuatilia kwa kina hospitali au mtaalamu anayekwenda kumfanyia huduma hiyo, kwa maana kama atafanyiwa na mtu asiye mzoefu madhara ni makubwa.

Licha ya uwapo wa madhara ambayo wataalamu wa afya huyasema, bado soko la upasuaji wa kurekebisha maumbile linazidi kushika hatamu duniani, wastani wa ongezeko la utolewaji wa huduma hiyo ni asilimia 9.2 kila mwaka.

“Soko la kimataifa la upasuaji wa kurekebisha maumbile lilikua kutoka Dola za Marekani bilioni 42.55 (Sh106.2 trilioni) mwaka 2022 hadi makadirio ya Dola bilioni 46.45 (Sh116.16 trilioni) mwishoni mwa mwaka 2023,” imesema ripoti ya upasuaji wa kurekebisha maumbile ya mwaka 2023.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi