Kitaifa
Aweso aiagiza Dawasa kuunganisha maji kwa mkopo
Dar es Salaam. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) kuhakikisha wananchi wanaowahudumia wanawezeshwa kupata huduma ya majisafi kwa kupewa utaratibu wa kulipa kidogokidogo kwa mkopo.
Ametoa kauli hiyo jana Novemba 17, 2023 kwenye hafla ya utiaji saini na kumkabidhi mkandarasi M/S SinoHydro kutoka China eneo la Pugu jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa sio wananchi wote wana uwezo wa kulipia gharama ya maunganisho mapya kwa wakati kulingana na utofauti wa kipato, hivyo kwa wale ambao hawawezi wapewe utaratibu wa kulipa kwa njia ya mkopo ili wote wanufaike na huduma ya majisafi.
“Kwa sasa upatikanaji wa maji kwenye maeneo mengi ya huduma umeimarika, hivyo ni vyema kila mwananchi apate huduma kikamilifu ili kufanikisha adhma ya Serikali ya ‘kumtua mama ndoo kichwani,” amesema Aweso.
“Tunapaswa kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa aliyoufanya wa fedha za ukamilishwaji wa miradi hii na usambazaji wa majisafi kwa wananchi kwenye maeneo mengi, hivyo tunapaswa kuhakikisha wananchi wanaona tija ya uwekezaji huu kwa wao kupata maji,” amesisitiza Aweso.
Kuhusu mradi wa maji wa Dar es Salaam ya Kusini, Aweso amesema unatarajiwa kunufaisha wakazi wapatao 450,000 wa majimbo ya Ukonga, Segerea, Ubungo, Kibamba, Ilala na Temeke na sehemu ya wilaya ya Kisarawe.
“Mradi huu ni wa muhimu sana kwa kuwa wananchi wa maeneo haya wamekuwa kwenye changamoto ya maji kwa muda mrefu, hivyo mkandarasi wa mradi ahakikishe anatekeleza mradi huu ndani ya wakati ili ukamilike na wananchi wapate maji,” amesema.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bona Kamoli ameishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza nguvu nyingi katika mradi huo, huku pia akiipongeza Dawasa kwa jitihada za kubuni na kusanifu mradi huo katika jimbo la Segerea.
Kwa upande wake Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Kiula Kingu amesema mradi huo unatekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia wa Sh36.967 bilioni.
“Utekelezaji wa mradi umegawanyika katika awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza utanufaisha Kata za Kwembe, Kitunda, Pugu Stesheni, Kipunguni na Mzinga.
“Awamu ya pili itahudumia wakazi wa Kata kata za Kivule, Kinyerezi, Zingiziwa, Majohe, Charambe, Kwembe, Buza, Msongola, Msigani na Mbezi,” ameeleza Kingu.
Amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa tangi la kuhifadhi na kusambaza maji lenye ukubwa wa lita milioni tisa litakalojengwa eneo la Bangulo, pia kutakuwa na ujenzi wa bomba la kusafirisha maji la ukubwa wa inchi 28 kwa umbali wa kilomita 10.8 pamoja na bomba la kusambaza maji la ukubwa wa inchi 28 na inchi 10 kwa umbali wa kilomita 17.29.
Ameongeza kuwa, Dawasa imetenga Sh500 milioni za utekelezaji wa miradi midogo ukiwamo wa jimbo la Kibamba utakaoufaisha wakazi 12,200 wa maeneo ya Mbezi Makabe, Kitopeni na maeneo ya jirani.
“Kwa Jimbo la Ukonga, Mamlaka imetenga Sh222 milioni kutekeleza mradi utakaonufaisha wananchi 19,144 wa Majohe, Kuchangani, Kivule na Mjimpya.
“Kwa jimbo la Segerea Mamlaka imetenga Sh334 milioni kupeleka huduma maeneo ya Vingunguti, Kipawa, Stakishari na Majimboga itakaonufaisha kaya 1,050.”