Kitaifa
Hofu ya uchaguzi inavyotia ‘ndimu’ mijadala bungeni
Dodoma. Mkutano wa 13 wa Bunge uliomalizika Ijumaa wiki iliyopita unaelezwa kurejesha historia ya mabunge ya 2012 na 2013 ambapo wabunge walitishia na hata kuwang’oa baadhi ya mawaziri kwa sababu mbalimbali, safari hii pia wakitaka wawajibike kwa kutapanya rasilimali za Taifa.
Mvutano mkali uliibuka zaidi wakati wabunge wakichangia taarifa tatu za Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC), Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) na Serikali za Mitaa (LAAC) huku mawaziri wakipambana kujibu mapigo.
Taarifa hizo zilitokana na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) inayoishia Juni 30, 2023 iliyoonyesha ubadhirifu katika maeneo mengi.
Mjadala huo ulihitimishwa kwa maazimio ya Bunge yaliyowataka mawaziri, makatibu wakuu na watendaji wengine wa Serikali waliotajwa katika ubadhirifu na wizi huo kujitathimini kabla mamlaka za uteuzi hazijachukua hatua dhidi yao.
Mengine ‘yaliyoutia ndimu’ mjadala ni suala la Kampuni ya Uendelezaji na Uendeshaji Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro (Kadco), ambalo wabunge wakishikilia msimami wao wa mwaka jana kuwa urejeshwe chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), suala ambalo limefanyika bila kusitasita tena.
Pia wabunge walikosoa ufujaji wa mapato, kutaifishwa kwa mifugo inayodaiwa kuingia ndani ya Hifadhi za Taifa na mapori ya akiba, wakati wa mjadala Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2024/25 na mwongozo wa mwelekeo wa bajeti ijayo.
Kutokana na mijadala ilivyokuwa ikisisitiza uwajibikaji, wasomi na wachambuzi waliozungumza na gazeti hili wamesema kauli za wabunge hao hazikutokana na utashi wao, isipokuwa kwa msukumo wa nje ya Bunge, ikiwemo hofu ya kuhojiwa na wananchi mwaka 2025 wakati wa uchaguzi na mitandao ya kijamii.
Wachambuzi hao wamesema misukumo hiyo inawafanya wabunge waamke na hasa kipindi hiki ambacho wanaelekea mwishoni mwa uhai wa Bunge la 12 na kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za mitaa mwakani na Uchaguzi Mkuu 2025.
Wanashambuliwa mno
Akizungumzia ukali huo wa wabunge, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Loisulie alisema ilikuwa ni haki yao kuja juu kwa namna yoyote kwa kuwa wamekuwa wakishambuliwa zaidi kupitia mitandao ya kijamii, kwamba “Bunge halina meno”.
Dk Loisulie alisema wananchi wameonyesha kama vile wabunge hawafanyi kitu katika kukabiliana na ubadhirifu, hivyo sauti walizozitoa zinamaanisha na huenda Watanzania wategemee watunga sheria hao kuwa wakali zaidi ya hapo.
“Ni kama wanajibu mapigo ya wale wanaowakosoa. Ikumbukwe watu wana hisia kwamba awamu ya sita haipambani na rushwa ukilinganisha na awamu ya tano ambayo mitazamo ya wengi wanaona ilikuwa na nguvu ya kukemea vitendo hivyo,” alisema.
Mhadhiri huyo alisema awamu ya sita inakosolewa pia kwamba ni Bunge la chama kimoja (CCM) na ndiyo maana wameamka kwa kusimama katika nafasi zao ili wakipe heshima chama chao, lakini nao waonekane wanaweza watakaposimama mbele ya watu kipindi cha uchaguzi mkuu.
Sambamba na hayo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Ruaha (Rucu), Dk Kaijage Rwezaula alisema kinachofanyika ndani ya Bunge hakiwezi kutofautishwa na uchaguzi mkuu ujao.
Dk Rwezaula alisema habari kwamba wabunge wameamka si sahihi, kwani waliamka tangu walipochaguliwa, lakini cha ajabu ni kama muda wote ni kama walikuwa usingizini.
“Tatizo liko kwetu wanazuoni na waandishi wa habari, hawa watu walijisahau nasi tukakaa kimya. Wana meno hawayatumii, sasa jua lipo kwenye machweo ndipo wanaamka usingizini, huu ni uchaguzi si kingine,” alisema Dk Rwezaula.
Hata hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St John’s cha Dodoma, Dk Shadidu Ndosa alisema hakuna jipya kwa wabunge, bali unafika wakati wanajisahau kwenye majukumu yao.
Dk Ndosa alisema hata nyakati za nyuma wabunge wa CCM walikuwa moto hata kama hakuna uchaguzi na walikuwa wanafanya vizuri na kusikilizwa na watu kwa kila hoja waliyoibuka nayo, akitolea mfano aliyekuwa mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe kabla hajawa waziri.
“Dk Mwakyembe alikuwa anatoka CCM na alikuwa moto sana kabla hajapewa jukumu la kuwa waziri. Kwa hiyo mimi kusema ni homa ya uchaguzi sikubaliani, lakini naunga mkono kuwa wanatimiza wajibu wao kuunga mkono juhudi za CAG, ambaye anafanya kazi kwa weledi na uzalendo mkubwa, lakini anapotoa ripoti yake watu hawachukuliwi hatua, inatuumiza hata sisi wa nje,” alisema Dk Ndosa.
Aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalumu na Jimbo la Kavuu, Dk Pudenciana Kikwembe alisema ni jambo la kawaida kwa wabunge kuwa wakali, hasa inapofika “kipindi cha lala salama.”
Alisema ni lazima wawe wakali kwani wanatoka halmashauri ambako kumejaa madudu na baadhi ya watendaji huwa wamenyanyua vichwa kwa kutafuna mali ya umma na “ukimya wa mwakilishi ni kitanzi kwake mbele ya waajiri wake siku ya kura.”