Connect with us

Makala

Wanawake masikini, wasiosoma wanamiliki zaidi nyumba, ardhi

Dar es Salaam. Umiliki wa nyumba na ardhi kwa mwanamke mmoja mmoja au kwa mashirikiano ni mkubwa karibu mara mbili na zaidi kwa wasiokuwa na elimu na vipato vya chini, kuliko wenye elimu na vipato vya juu.

Pia umiliki huo ni mkubwa zaidi kwa wanawake wanaoishi vijijini kuliko wanaoishi mijini. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria (TDHS) wa mwaka 2022 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Hali hiyo inatajwa kuchangiwa na mila na desturi, huku vipaumbele vikitajwa kuweka utofauti kati ya wanawake waliosoma na wasiosoma.

Ripoti hiyo iliyozinduliwa hivi karibuni inaeleza, asilimia 24 ya wanawake walio na elimu ya sekondari na zaidi na kipato cha juu ndio wanamiliki nyumba na asilimia 13 wakimiliki ardhi.

Kwa upande wa wanawake wasiokuwa na elimu, umiliki wao wa nyumba ni kwa asilimia 53, huku umiliki wa ardhi ukiwa asilimia 38.

Hiyo ikiwa na maana kuwa umiliki wa wale wasiokuwa na elimu na wenye kipato kidogo ni karibu mara tatu zaidi ya ule wa waliosoma na wenye kipato.

Wataja sababu

Oscar Mkude, mtaalamu wa uchumi alisema umiliki wa ardhi unaweza kuwa mkubwa katika maeneo ya vijijini kwa sababu ndiyo chanzo cha kwanza cha mapato.

Hiyo ni kutokana na kile alichoeleza, wanawake wa vijijini wamekuwa wakitumia ardhi wanayomiliki katika kilimo, ufugaji na baadaye huanzisha makazi tofauti na wanawake waliosoma ambao chanzo chao cha kwanza huwa shughuli nyingine kama vile biashara.

“Huyu aliyesoma na anaishi mjini anaponunua ardhi maana yake anataka kufanya uendelezaji kwa ajili ya kujiingizia kipato,” alisema Mkude. Alisema pia wanawake waliosoma na kuolewa hupenda kuacha baadhi ya shughuli kwa wenza wao.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Beldina Msese, mkazi wa Sinza aliyesema: “Ni kawaida kukuta mtu ana maduka matatu hadi manne lakini hana nyumba wala kiwanja, anaishi nyumba ya kupanga, huenda kutokana na viwanja kuwa mbali na sehemu zao za biashara, hivyo wanaona ni bora kupanga karibu,” alisema Beldina.

Lazaro Jackson, alisema ni ngumu kukuta mwanamke aliyesoma na anaishi mjini akiwaza kuanza kununua kiwanja au kujenga kabla ya kumiliki biashara ili kumuingizia kipato. “Wengi wanaanzia kwenye kuwekeza, wakati huo ndiyo hukutana na wenza wao wanaanza maisha, hivyo si rahisi kwao kumiliki mali hizo ila ukisema ufanye sensa ya biashara utawakuta wengi huenda kuliko wanaume,” alisema Jackson.

Akizungumzia suala hilo, Bernard Baha, ambaye ni Mratibu wa Jukwaa la Ardhi Tanzania (Tala), alisema si kila aliyesoma anaweza kupinga mila na desturi, akieleza ni wachache wanaoweza kusimama na kusema sheria inasimamia haki fulani.

Takwimu zaidi

Ripoti inaonyesha umiliki wa ardhi na nyumba huongezeka kadiri umri unavyokua. Ni asilimia tano ya wanawake walio na umri wa kati ya miaka 15 hadi 19 ndio wanamiliki nyumba, huku asilimia nne wakimiliki ardhi.

Hiyo ni tofauti na wanawake walio na umri wa miaka 45 hadi 49 ambapo asilimia 72 wanamiliki nyumba na asilimia 52 wanamiliki ardhi.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi