Kitaifa
Zigo bima ya afya kwa wote kurejea bungeni
Dar es Salaam. Kwa mara nyingine Serikali imepanga kuwasilisha tena muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote katika mkutano wa Bunge utakaoanza wiki ijayo.
Muswada huo kwa sasa umefanyiwa marekebisho baada ya Wizara ya Afya kupokea maoni ya wadau mbalimbali na hivi sasa umepelekwa katika Baraza la Mawaziri kwa uamuzi, imefahamika.
Februari mwaka huu, licha ya kuwekwa katika ratiba ya mkutano wa Bunge kwa ajili ya kusomwa kwa hatua zote tatu za mchakato wa utungwaji wa sheria, uliondolewa kwa kile kilichobainika kutokuwepo kwa chanzo endelevu cha fedha kutekeleza mpango huo.
Huo ulikuwa mkwamo wa pili wa muswada huo tangu usomwe kwa mara ya kwanza katika mkutano wa nane wa Bunge na kupelekwa kwenye Kamati ya Bunge kwa ajili ya kuuchambua.
Katika mkutano wa tisa, muswada huo ulipangwa kujadiliwa kwa siku moja Novemba 12 mwaka jana, lakini pia ulikwama.
Akiuondoa bungeni, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema “Bunge na Serikali tunaendelea na mashauriano juu ya mambo ambayo hatujaafikiana vizuri.”
Bunge lilikuja na hoja hiyo kufuatia takwimu zilizotolewa na Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (Tasaf) kubainisha kuwa asilimia 26 ya Watanzania ndiyo wanaotakiwa kulipiwa huduma ya bima ya afya na mfuko wa Serikali.
Kabla ya kukwama, muswada huo uliosomwa Novemba mwaka jana ulitakiwa kusomwa kwa mara ya pili na kujadili Februari mwaka huu na kupitishwa.
Septemba 25 mwaka huu, akizungumza na vyombo vya habari kuhusu mafanikio ya sekta ya afya nchini, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel alisema Serikali inakusudia kuurudisha bungeni muswada huo.
Japokuwa hakutaja lini utarejeshwa, alisisitiza Serikali haina tatizo, bali wadau ndio wanaoleta ukinzani wa mawazo kwenye mfumo huo.
Jana, jijini Dar es Salaam, akitoa mada kwa vyombo vya habari kuhusu muswada huo, Ofisa Habari Mwandamizi wa Wizara ya Afya, Said Makora alisema tayari wamepokea maoni mbalimbali na kufanya marekebisho, hivyo muswada huo unatarajiwa kusomwa katika mkutano wa Bunge wa Novemba.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu hakupatikana jana kupitia simu yake ili atoe ufafanuzi wa kilichofikiwa mpaka sasa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Stanslaus Nyongo alipoulizwa iwapo yale maoni waliyoyataka yamefanyiwa kazi, alisema “na sisi tunasubiri uletwe ndiyo tutajua.”
Katika mada yake, Makora alisema kilichokwamisha muswada huo ilikuwa ni namna ambavyo wasio na uwezo watapatiwa huduma za matibabu.
“Muswada ulikwamishwa na kundi hili, Bunge waliuliza fedha mtazitoa wapi? Mtuonyeshe mtazitoa kwenye chanzo kipi na hicho kiwepo kwenye sheria, lakini pia walisema hawaridhiki na mfumo wa Tasaf wa kuwatambua watu wanaotoka kwenye kaya maskini.
“Hivyo tunatafuta njia nyingine za kuwatambua, kwa hivi sasa kuna majadiliano ya jinsi ya kulifanya hili jambo, hivyo tukirudi bungeni kwa jinsi tulivyojipanga kulingana na yale waliyotuelekeza kwa namna tulivyoyakamilisha, wataweza kutusikiliza,” alisema.
Licha ya vikwazo vilivyopo, Mtaalamu wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati alisisitiza kuwa suluhisho la changamoto nyingi za huduma za afya ni kupitisha muswada wa sheria ya bima ya afya kwa wote.
“Katika vitu vinavyosubiriwa kwa sasa ni hiki. Suala la bima ya afya kwa wote lilienda bungeni likatolewa na hatujaambiwa sababu, bajeti ya Wizara ya Afya ilipita haikuzungumzia kitu chochote, nafikiri NHIF inajua sababu za ndani kwa sababu Serikali ilitaka kuweka hela ili huduma iweze kuanza,” alisema.
Hoja ya Dk Osati haina tofauti a iliyotolewa na Septemba 8 mwaka huu na Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtoni aliposema, “bima ya afya kwa wote itakuwa suluhu ya kudumu kwa wananchi wote, ikiwemo watoto wasio na wazazi na wasiojiweza ambao awali walikuwa wakilipiwa na wahisani kupitia “Toto Afya Kadi”.
Changamoto za mfumo
Pamoja na jitihada za kupata bima kwa wote, bado kumekuwa na changamoto katika utekelezaji wa mifumo ya ugharamiaji huduma za afya katika utaratibu wa malipo ya papo kwa papo na msamaha na hivyo kusababisha baadhi ya wananchi kukosa huduma kutokana na kukosa fedha za kugharamia huduma za matibabu vituoni.
Makora alisema mpaka sasa bado kuna idadi ndogo ya wananchi katika mfumo wa bima ya afya, waliojiunga kwa hiari ambao ni asilimia 15.3 ya Watanzania wote. Kati ya hao, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) una asilimia 8, CHF asilimia 6, NSSF asilimia 0.3 na bima binafsi ni asilimia 1.
“Hali hii imesababisha wananchi kujiunga wakiwa wagonjwa kinyume na kanuni za bima,” alisema.
Alisema wakati muswada huo unaandaliwa kutimiza wajibu wa Serikali wa kikatiba wa kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya bila vikwazo, asilimia 85 ya Watanzania wapo nje ya mfumo huo.
Kusuasua huko kuliwahi kugusiwa na aliyewahi kuwa Spika Job Ndugai, Novemba mwaka juzi aliposema suala la muswada huo linapaswa kushughulikiwa haraka.
Ndugai wakati huo akiwa Spika alisema hayo baada ya muswada huo uliokuwa umewasilishwa bungeni kukwama.
“Bima inagusa Watanzania wengi, hususan wa kipato cha chini. Huu ni muda mwafaka kwa muswada kufikishwa ili itungwe sheria. Ni muhimu Serikali ikasema kama kuna mkwamo mahali, ili Bunge lisaidie,” alisema Ndugai wakati huo akiwa spika kabla ya kujiuzulu Januari 6, mwaka jana.
Uhai na uendelevu
Katika hatua nyingine, Makora alisema Wizara ya Afya imefanya tathmini mbili za uhai na uendelevu wa mifuko ya bima ya afya ili kubaini gharama za matibabu, kupitia mshauri elekezi wa kimataifa, Muhanna and Co. Ltd, Lebanon, mwaka 2020.
Pia tathmini ya NHIF ilifanyika mwaka 2022 na zote mbili zimeonyesha uhimilivu wa mifuko unategemea idadi kubwa ya wanachama kujiunga na bima na kuwa uhiari wa kujiunga ni changamoto katika utekelezaji wa mfumo huo nchini.
“Wanachama na makundi yote walioingia kwa hiari wametumia huduma zaidi ya michango yao kwa wastani kati ya asilimia 212 kwa mwaka 2020 hadi asilimia 369 kwa mwaka 2021,” alisema.
Katika kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa sheria inayopendekezwa, mikakati na mipango mbalimbali ya utekelezaji kabla na baada ya sheria hiyo kupitishwa, ni mpango endelevu wa utoaji wa elimu kwa umma.
Kumekuwepo na ongezeko la vituo vya kutolea huduma za afya kutoka 8,449 mwaka 2019 hadi 10,067 kwa mwaka 2022 vinavyotoa huduma katika maeneo yote ya mijini na vijijini.
Kufuatia hatua iliyofikiwa, Naibu Msemaji wa sekta ya afya wa Chama cha ACT- Wazalendo, Ruqayya Nassir alisema waliishauri Serikali itenge kila mwaka katika bajeti asilimia 2.5 ya pato la Taifa kama fedha za kuchangia mfumo huo (sawa na Sh3.5 trilioni kwa bajeti ya sasa).
Wakati Tanzania ikiandaa muswada huo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeshauri Serikali kuangalia uwezekano wa kuwa na bima moja ili kuwawezesha wenye uwezo kifedha na wasio na uwezo kuhudumiwa kwa usawa.
Imeelezwa kuwa uwepo wa mifuko mingi ya bima ya afya inaleta mkanganyiko katika utoaji wa huduma hiyo.
Muswada wenyewe
Katika utekelezaji wa Sheria ya bima ya afya kwa wote viwango vilivyopendekezwa katika muswada uliiondolewa ni:
i. Sekta rasmi: Kiwango cha uchangiaji cha asilimia 6 kwa watumishi wa umma na wafanyakazi wa sekta rasmi binafsi.
ii. Wananchi waliojiajiri katika sekta isiyo rasmi kiwango ni Sh340,000 kwa kaya ya watu sita kwa mwaka.
iii. Kiwango kwa mtu mmoja Sh120,000.
iv. Kiwango cha Sh 60,000 kilipendekezwa kwa kaya kwa mwaka kwa wananchi waliopo katika sekta isiyo rasmi, kwenye kitita cha mafao ya huduma za msingi cha jamii.