Connect with us

Kitaifa

Rais Samia atoa maagizo ucheleweshaji vifaa vya miradi bandarini

Dar/mikoani. Rais Samia Suluhu Hassan ameziagiza mamlaka zote zinazohusika na miradi zinazohusisha uagizaji wa vifaa nje ya nchi, kujipanga ili vifaa vinapofika kusiwe na ucheleweshwaji na miradi itekelezwe kwa haraka.

Amesema miongoni mwa changamoto alizobaini wakati wa utekelezaji wa miradi, ni ucheleweshaji wa misamaha ya kodi, vibali vya baadhi ya wafanyakazi na kuchelewa kwa vifaa kuondolewa bandarini.

Rais Samia aliyasema hayo leo Jumanne, Oktoba 17, 2023, wakati akipokea taarifaa ya mradi wa umeme vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) awamu ya tatu mzunguko wa pili wilayani Iramba mkoani Singida.

“Nilipokuwa India kwa ziara maalumu, nilipata nafasi ya kunong’ona na mkandarasi na washauri wakanieleza changamoto wakati wa utekelezaji wa mradi huu ikiwemo kuchelewa kwa  misamaha ya kodi, vibali vya wafanyakazi, mkandarasi na mtaalamu mshauri na ucheleweshaji wa kutoa vifaa bandarini.

Changamoto zote hizi ni za kutengenezwa na taasisi zetu, kwa maneno mengine Serikali inajichelewesha yenyewe na huu ndio ugonjwa ninaoutaja kila mara wa kukosekana kwa uratibu ndani ya taasisi zetu,” amesema

Kuhusu mradi wa maji uliogharimu Sh24.47 bilioni aliouzindua wilayani hapo, Rais Samia amesema kukamilika kwake kazi kubwa iliyobaki ni usambazaji kwenye vitongoji na vijiji.

Amesema hakutakuwa na maana wananchi kuona maji kwenye mabomba bila kupata.

“Hapa niseme kidogo kuhusu bei ya kuwaunganishia maji watu nyumbani na uwekaji wa mita, kulikuwa na malalamiko makubwa ya ubambikaji wa bili za maji, malalamiko haya yataondoshwa kwa kutumia teknolojia,” amesema.

Iwapo mita hizo zitafungwa kwenye nyumba za wananchi alisema zitaondoa kero kwani malipo yatakuwa kabla ya matumizi.

Akiwa wilayani Igunga, Mkoa wa Tabaora kuendelea na ziara mkoani humo akitokea Singida, Rais Samia amewahakikishia wakulima wa eneo hilo soko la mazao yao hata itakapotokea changamoto katika masoko ya kimataifa.

Kulingana na mkuu huyo wa nchi, itakapotokea changamoto katika masoko hayo, Serikali imejipanga kununua mazao yote na kuyahifadhi hadi itakapopata soko.

“Patakapokuwa na changamoto katika masoko ya nje, Serikali imejiandaa kununua mazao hayo tutahifadhi na tutauza pale masoko yatakapopatikana,” amesema

Katika wilaya hiyo, amezindua Chuo cha Ufundi stadi Veta, akisema ni mwendelezo wa juhudi za Serikali kuhakikisha vijana wanapata elimu ya amali na ufundi.

“Tumeamua Wilaya zote kuwe na vyuo vya aina hii na kila Mkoa kiwe na chuo cha Mkoa na shabaha yetu ni kujenga vyuo vitakavyofundisha vijana elimu ya amali,” amesema

Ameeleza uamuzi huo unalenga kuzalisha wataalamu wa ndani watakaokuwa na uwezo wa kutumika katika miradi, badala ya nafasi hizo kuchukuliwa na wageni.

Kwa mujibu wa Rais Samia, vyuo hivyo vinajengwa vikihusianishwa na mpango wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) inayohusu kilimo na mifugo.

Akihutubia wananchi wa Nzega mkoani humo, Rais Samia amesema mkakati wa Serikali kwa sasa ni kuzalisha yenyewe mbegu kwa ajili ya wakulima.

Mkakati huo, unatokana na kile alichoeleza, kumekuwa na changamoto ya bei ya bidhaa hiyo, kadhalika malalamiko ya ubora wake.

“Nimeongea na wakala wa uzalishaji mbegu (ASA) wamenambia wameongeza mashamba, tumedhamiria kuzalisha wenyewe mbegu,” amesema.

Hata hivyo, ametaka uzalishaji wa mbegu hizo uende sambamba na usambazaji wake, kama inavyofanyika katika usambazaji wa pembejeo.

Rais Samia amewasisitiza wakazi wa eneo hilo kuongeza juhudi katika shughuli za kilimo kwani Serikali inafanya kila namna kuhakikisha inawawekea mazingira bora.

Lakini ametaka juhudi hizo, ziende sambamba na uongezaji thamani na masoko ili kuwa na tija.

Katika hotuba yake hiyo, ameeleza kusikitishwa na vijana wa Nzega wanaojihusisha na dawa za kulevya badala ya shughuli za maendeleo.

Ametaka Serikali ya mkoa huo kuhakikisha inadhibiti hilo.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa amesema wapo baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya wasiotekeleza majukumu yao, badala yake wamejikita kutafuta majimbo.

“Hawa wanapokea fedha za miradi ya maendeleo lakini wanafanya kazi za siasa kutafuta majimbo badala ya kusimamia maendeleo,” amesema

Ameahidi kupeleka majina yao kwa Rais Samia ili nafasi hizo wapewe watakaokuwa na uwezo wa kusimamia miradi ya maendeleo.

“Upeleke watu ambao watasaidia kusimamia miradi ya maendeleo, kwa sababu fedha unazopeleka kwenye halmashauri na Mikoa ni nyingi,” amesema

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameeleza umuhimu wa vyuo hivyo ni kumwezesha muhitimu kuwa na uwezo wa kujiajiri.

“Vyuo hivi ni muhimu kwani vinamwezesha mtu mwenye elimu kuanzia darasa la saba hadi chuo kikuu kuwa na ujuzi utakaomwezesha kuendesha maisha yake,” alisema.

Naye Mbunge wa Iramba Magharibi ambaye ni Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amemsifu Rais Samia kwa kuwaunganisha Watanzania pamoja na vyama vya siasa’

“Ulichokifanya si kila mtu anaweza kukifanya, wewe umekuja na R4 maridhiano, ustahimilivu, mageuzi, wewe ni mama wa vyama vyote unavyovifanya si kila mtu anaweza kufanya,” amesema Dk Mwigulu na kuongeza:

“Fuatilia wale wanaopatana na Serikali na chama tawala wakiomba tuvumiliane, fuatilia wao kwenye vyama vyao wameweza kupatana kiasi gani wanapotofautiana.”

Kwa upande wake, Naibu waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Serikali inaendelea kusimamia mradi wa Julius Nyerere kwa kiwango cha juu na tayari wamefikia asilimia 92.74, hadi Januari wataanza majaribio.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi