Connect with us

Kitaifa

Rais Samia amebisha hodi milango mitano nyeti India

Jumapili (Oktoba 8, 2023), ni saa 11:15 alasiri. Hiyo ni kwa mujibu wa majira ya Delhi, India ambayo ni saa 8:45 mchana, ndege mpya ya Shirika la Air Tanzania, Boeing 737-9 Max (Olduvai Gorge), inatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Indira Gandhi, Delhi. Ni uthibitisho kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amewasili India.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, yupo tayari uwanjani kumlaki Rais Samia. January alitangulia mapema India kwa ajili ya maandalizi ya ziara hiyo.

Mwenye jukumu la kumlaki Rais Samia ni Waziri wa Elimu wa India, Annapurna Devi. Bila shaka, iliwapendeza rais mwanamke apokelewe na kiongozi mwanamama.

Burudani kidogo airport. Akinamama wanacheza dansi asilia ya Kihindi aina ya Koli. Ndivyo wanavyomkaribisha Rais Samia India, kwa kumwonjesha ladha ya utamaduni wao kimuziki na sanaa kwa jumla.

Inakuwa ziara ya kwanza ya Rais Samia India, tangu alipokula kiapo cha kuongoza dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni ziara ya kwanza baada ya miaka nane kwa Rais wa Tanzania kuzuru taifa hilo la Bara la Asia.

Rais wa Nne, Jakaya Kikwete, alikuwa kiongozi wa juu wa Tanzania kufanya ziara ya kikazi India. Ilikuwa Juni 2015, takriban miezi mitano kabla hajakabidhi kijiti kwa Rais wa Tano, John Magufuli.

Uhusiano wa Tanzania na India, umejengwa kutoka mbali. Kabla ya uhuru, kisha Tanganyika ilipopata uhuru, India chini ya Waziri Mkuu wa kwanza, Jawaharlal Nehru, ilifungua ubalozi wake Dar es Salaam, Novemba 1962. Uhusiano ukatanuka baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Misimamo ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Nehru, iliendana katika maeneo mengi, hasa kutenganisha dini na siasa, kupiga vita ubaguzi wa aina yoyote na kupambana na ukoloni.

Mwaka 1971, Mwalimu Nyerere alifanya ziara ya kwanza India. Mwaka 1972, Rais wa India Varahagiri “V.V” Giri, alizuru Tanzania. Mwalimu Nyerere alifanya ziara saba akiwa Rais (mwaka 1971, 1976, 1981, 1982, 1983, 1984 na 1985). Na kila Rais wa Tanzania, alitembelea India, kasoro Magufuli.

Rais Ali Mwinyi alitembelea India mara mbili (mwaka 1989 na 1993). Rais Benjamin Mkapa, mara moja, mwaka 2002. Kikwete mara mbili (mwaka 2008 na 2015).

Viongozi wakuu wa India wamekuwa wakitembelea Tanzania. Baada ya Rais V.V Giri mwaka 1972, Makamu wa Rais wa India G.S. Pathak, alizuru Tanzania mwaka 1974 na aliyemfuatia, D.B. Jatti mwaka 1975.

Waziri Mkuu wa vipindi viwili India, Indira Gandhi, alitembea Tanzania mara mbili, mwaka 1976 na 1980. Waziri Mkuu wa Sita wa India, Rajiv Gandhi (mwaka 1986). Waziri Mkuu wa 12, Inder Gujral (1997). Waziri Mkuu wa 13, Manmohan Singh (Mwaka 2011) na Waziri Mkuu wa 14, ambaye ndiye aliye ofisini hivi sasa, Narendra Modi, mwaka 2016.

Mwaka 1989, Tanzania ilimpokea Rais wa Nane wa India, Ramaswamy Venkataraman na mwaka 2004, Rais wa 11 wa nchi hiyo, Abdul Kalam.

Mwaka 1974, Serikali ya India ilimtunuku Mwalimu Nyerere, Tuzo ya Jawaharlal Nehru ya Uelewa wa Kimataifa. Kisha, mwaka 1995, India walimpa Mwalimu Nyerere, Tuzo ya Amani ya Gandhi kwa kufanikisha uhuru wa Tanganyika bila kumwaga damu.

Inathibitishwa bila kuacha shaka kuwa uhusiano wa Tanzania na India una mizizi ya muda mrefu. Kitendo cha Rais Samia kuzuru India, ni mwendelezo wa undugu ulioasisiwa na Mwalimu Nyerere.

Uhusiano na manufaa

India ina miaka 76 tangu ilipopata uhuru wake kutoka UK, kadhalika Tanzania miaka 62. Asili ya uhusiano uliojengwa na Mwalimu Nyerere pamoja na Nehru ni tofauti kabisa na mazingira ya sasa.

Miaka ya 1960 hadi 1980, India na Tanzania zilijenga uhusiano wa kufaana na kuliwazana dhidi ya ubeberu wa Magharibi. Muongo wa tatu wa Karne ya 21, India ni taifa tajiri na linatarajiwa kuwa kwenye kilele cha dunia miongo mitatu ijayo.

Price Waterhouse Coopers (PwC) ni taasisi ya kimataifa ya mahesabu. Makao yake makuu ni UK. Imo kwenye zile taasisi nne kubwa za utaalamu wa hesabu duniani. Nyingine ni Deloitte, Ernst & Young (EY) na KPMG.

Kwa mujibu wa PwC, matazamio ya kimahesabu ya pato la Taifa (GDP), ifikapo mwaka 2050, nchi za Magharibi zitapigwa mweleka. China itashika nafasi ya kwanza, India itakuwa ya pili kwa uchumi mkubwa duniani.

Tanzania inahitaji kuimarisha uhusiano wake na China, India, Indonesia, Brazil na Mexico, bila kulegeza kwa Marekani, Russia, Japan, Ujerumani na Uingereza. Hayo ni matakwa ya kujenga na kuimarisha uhusiano wenye manufaa, kulingana na uelekeo wa uchumi duniani.

Chenye kupendeza kuhusu India ni jinsi walivyoibeba kwa uzito ziara ya Rais Samia. Hawajajitazama kama wao sasa ni wakubwa na wanazidi kukwea kiuchumi na Tanzania bado inajitafuta, wamempa Rais Samia hadhi stahiki kama mkuu wa nchi rafiki.

Vyombo vya habari India, vimeripoti kwa ukubwa kuwa Rais Samia amezuru India kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Droupadi Murmu. Hicho ni kipimo kwamba Tanzania imo ndani ya kitabu kizuri cha India.

Hodi milango mingine

Ripoti ya Benki ya Dunia imeitaja India kuwa mnunuzi mkubwa wa malighafi, ikishika nafasi ya sita ulimwenguni. Ziara ya Rais Samia inabisha hodi kwenye mlango wa mauziano ya malighafi, hivyo kutoa fursa pana kwa wakulima na wafanyabiashara wa Tanzania.

India ni taifa jabali duniani ambalo linaelekea kupata ushindi mkubwa dhidi ya umaskini. Ripoti ya Tume ya Mipango India, inaonyesha kuwa kasi ya kubadili maisha ya wananchi kutoka umaskini hadi daraja la kati ni kubwa. Na inahitajika miongo michache, hakutakuwa na Mhindi fukara.

India, nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu ulimwenguni. Ikifikisha watu bilioni 1.4 na kuipiku China, Aprili 2023, imekuwa na wastani wa kuwavusha watu milioni 130 kila miaka 10, kutoka umaskini hadi daraja la kati. Wastani wa kuishi wa wananchi wa India ni miaka 70.

Ziara ya Tanzania India bila shaka inabisha hodi kwenye mlango wa maarifa ya mageuzi ya kimaisha ya wananchi. Watanzania wapo milioni 62 tu. Inawezekana kabisa kuushinda umaskini na Tanzania isiwe na raia fukara ndani ya miongo michache kama itasoma mbinu ambazo India watazitumia.

India ni taifa linalotamba kwa ufahari mkubwa kwamba linaongoza kwa demokrasia duniani na limeweza kujenga uchumi mkubwa wakati likijenga na kuimarisha misingi ya kidemokrasia.

Tazama taifa ambalo linapiga hatua kubwa kiuchumi na kuelekea kileleni, likizipiku nchi ambazo zamani ilizinyenyekea, bila kuminya uhuru wa maoni wala kuchomoza makucha ya udikteta, lipo lilipo.

Huu ni mlango mzuri mno ambao Rais Samia amebisha hodi kupitia ziara yake India. Wahindi wamewezaje vita vya kiuchumi bila kuminya demokrasia? Imekuwa fahari kubwa kwao kuwa wamejenga uchumi imara katikati ya misingi thabiti ya kidemokrasia.

Dola ya Shirikisho India inaundwa na Serikali ya Kibunge. Rais Murmu ni mkuu wa nchi, raia namba moja, amiri jeshi mkuu, Waziri Mkuu, Modi, ndiye kiongozi wa serikali.

Ratiba ya Rais Samia India, ilitosheleza mikutano na viongozi wote wakuu India, kuanzia Modi mpaka Murmu yenye kuhusu ushirikiano. Vikao vyote vilifanyika Ikulu ya India, Rashtrapati Bhavan, New Delhi.

Ziara hiyo ilihusisha kusaini na kubadilishana hati za makubaliano katika maeneo mbalimbali ya ushirikiano. Rariba pia ilionesha angehudhuria kongamano la uwekezaji na biashara, New Delhi.

Huo ni mlango wa tano ambao Rais Samia ameubishia hodi India. Kuimarisha uhusiano sio tu na serikali pamoja na mkuu wa nchi, vilevile na wafanyabiashara wa nchi hiyo. Miaka saba iliyopita, wakulima wa mbaazi Tanzania walipitia kipindi kigumu, sababu soko India lilikatishwa ghafla.

Thamani ya kilo moja ya mbaazi ilishuka kutoka Sh2,500 mpaka Sh200. Maumivu yalikuwa makali. Ufumbuzi wa haraka ulikosekana kwa sababu ya kulega kwa uhusiano. India ni mkulima mkubwa wa mbaazi, pia inaongoza kwa uagizaji wa nafaka hizo. Mbaazi za Tanzania kukosa soko India yalikuwa matokeo ya kuzorota kwa uhusiano wa kidiplomasia.

Rais Samia kushiriki kongamano la biashara na uwekezaji India ni karata ya ukaribisho kwa wawekezaji, vilevile kufungua milango ya ushirikiano wa kiteknolojia. India ipo mbali kwenye teknolojia. Tanzania inaweza kunufaika kwa kutumia vizuri fursa.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi