Connect with us

Makala

Pombe janga jipya kwa afya ya akili nchini

Dar es Salaam. Kama wewe ni mnywaji wa pombe, sasa kaa mkao wa tahadhari!

Kama hukuwa unajua hili, leo ndio siku yako ya kubaini kuwa kinywaji unachokunywa ni sawa na dawa yoyote ile ya kulevya.

Kwa mujibu wa mtaalamu bingwa wa saikolojia na afya ya akili kutoka Hospitali ya Afya ya Akili Mirembe, Dk Japheth Swai, kinachoifanya pombe iwe sehemu ya kundi hilo ni tabia zake inapotumika katika mwili wa binadamu.

“Pombe inalevya, pombe inafubaza, pombe inakujengea uraibu na pombe inakufanya ufanye kitu kinyume na uhalisia wako, inakupa ujasiri wa uongo, hivi ni vitu vinavyofanywa na dawa za kulevya,’’ anasema na kuongeza:

“Dawa ya kulevya ni dawa yoyote utakayoitumia ikakufanya uwe katika hali ya ulevi au kufanya ubongo wako usifanye kazi kama ilivyo kawaida,” anasema.

Hata hivyo, mtaalamu huyo anasema hatari ya pombe ni kubwa zaidi ukilinganisha na dawa nyingine za kulevya.

Hilo linatokana na kile anachofafanua kuwa pombe ndiyo mlango wa matumizi ya dawa nyingine zote za kulevya.

Matumizi ya pombe, kulingana na Dk Swai huathiri ubongo na kwa sababu akili huutumia ubongo kufanya kazi, ukiharibiwa hautatumika tena na hapo ndipo tatizo la afya ya akili huanzia.

Hata hivyo, anaeleza kuwa, kinachotofautisha pombe na dawa nyingine za kulevya, anasema ni uhalali wa kisheria ilionao wa kutumika nchini, lakini nayo ni dawa ya kulevya.

Unywaji pombe na athari kwenye ubongo

Wataalamu wamebainisha kuna athari za kiafya kwa watumiaji wa aina hiyo ya vinywaji.

Wataalamu wameenda mbali zaidi wakisema kuwa ubongo unaokua wa kijana aliyebaleghe huwa katika hatari kubwa ya kudhurika na sumu ya pombe, kwa kuwa pamoja na kupita maeneo mengine mwilini, inakwenda moja kwa moja katika ubongo.

Takwimu zilizotolewa Oktoba mwaka huu na Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha wakati pombe ikikadiriwa kuua watu milioni tatu kila mwaka, wastani wa un ywaji wa pombe nchini, unaonyesha Mtanzania hunywa lita 10.4 za pombe kwa mwaka.

Dk Japheth Swai anasema unapokunywa pombe pamoja na kupita katika maeneo mengine ya mwili, lakini uelekeo wake ni kwenye ubongo na kwenda kuuathiri.

Anaendelea kusema kwa kuwa akili inafanya kazi kwa kushirikiana na ubongo, ukiathirika maana yake uhusiano wa akili na ubongo hautakuwa sawa.

“Hapo sasa mtu atapoteza ule uwezo wake wa kufanya maamuzi kwa busara, kwa sababu pombe inakwenda kushambulia lile eneo ambalo lingetumika kutekeleza maamuzi ya busara,” anasema.

Hatari zaidi, anasema inakuja pale ambapo pombe itatumika kwa muda mrefu, kwani inamfanya mtu aitegemee na kukosa uwezo wa kufanya lolote bila usaidizi wa kilevi hicho.

“Mtu anaanza kuwa tegemezi anakuwa hawezi kumudu lolote hadi atumie kilevi. Ikishafikia hatua hiyo ndipo ambapo mtu awe amekunywa au hajanywa hawezi kuwa sawasawa,” anasema.

Kipindi hicho, anasema ndicho ambacho ugonjwa wa akili huanza kushika kasi.

“Unakuta mtu anakuwa tayari achukue fedha ya ada ya mwanawe akanunue pombe anywe, anakosa maamuzi ya busara hilo tayari ni tatizo la akili,” anasema.

Pombe na msongo wa mawazo

Kuna wanaodai kuwa pombe inapunguza mawazo. Iko hivi, ukinywa kinywaji hicho utendaji wa baadhi ya viungo vyako vya mwili hupungua tofauti na uhalisia wake, kama inavyofafanuliwa na Dk Godwin Mwisomba, ambaye ni mwanasaikolojia kutoka Hospitali ya Mirembe.

“Kwa mfano ukiwa na mawazo kwa kawaida moyo unaenda mbio na hata shinikizo la damu linakuwa juu, sasa ukinywa pombe mapigo ya moyo yanapungua kabisa na hata shinikizo la damu linapungua,” anasema.

Hata ubongo, anasema unapokunywa pombe unapunguza uwezo wa kufikiri na hapo ndipo ambapo wengi huona mawazo yamepungua.

Kawaida ya pombe, anasema unapokunywa inasababisha ubongo utoe homoni za furaha na ndizo zinazomfanya mtu ahisi vizuri baada ya kunywa.

“Lakini homoni za furaha zinapatikana kwa njia ya kawaida, mfano ukiwa na kiu halafu ukanywa maji au ukiwa na njaa ukala chakula,” anasema.

Anaeleza ukitumia pombe kujipa furaha, unatengeneza njia bandia ya kutafuta furaha ilhali zipo njia za asili zinazopaswa kutumika.

“Ukinywa pombe, ukivuta bangi unatengeneza njia bandia ya kujiletea furaha ilhali ipo njia asili,” anasema.

Hatari zaidi ni pale anaposema, kadri unavyokunywa pombe ubongo unajifunza kwamba furaha yako inatokana na kunywa na si vinginevyo.

Kuanzia hapo, anasema mwili na ubongo vinatengeneza tabia ya utegemezi wa pombe kama chanzo cha furaha na hapo ndipo uraibu huanzia.

“Leo utakunywa moja itakupa furaha, kesho utakunywa moja itakupa furaha keshokutwa haitakupa itakutaka uongeze kiwango ili ikupe furaha, hivyo hivyo hadi unafika wakati mtu anakunywa kreti nzima, hii ndiyo tabia ya pombe,” anasema.

Katika hatua hiyo, Dk Mwisomba anasema pombe inatengeneza mazingira ya kuudhibiti mwili, badala ya mtu kujidhibiti.

“Uwezo wa kujisimamia unapungua, unafika wakati unakwenda baa kunywa chupa moja lakini unajikuta unakunywa zaidi, kwamba tayari pombe inakudhibiti wewe badala ya kujidhibiti au kuidhibiti, hii ndiyo tabia ya pombe,” anasema.

Ukifikia hatua hiyo, anasema mabadiliko ya tabia za mwili hutokea, kama uwezo wa asili wa kufanya kazi, kufikiri na mambo mengine hupungua.

Katika hatua hiyo, anasema mwili na akili zote zinakuwa chini ya utawala wa pombe, badala ya yenyewe kutawaliwa na akili na mwili.

“Hapo anakuwa na uraibu wa hali ya juu na madhara mengine ya mwili hutokea Kwa sababu ukinywa pombe inavutwa na kuingiza kwenye mfumo wa damu,” anasema.

Baada ya kuingia kwenye mfumo wa damu, anasema ini ndilo huchakata huku likiathiriwa.

Katika matibabu ya mraibu wa pombe, anasema wanaanza na hatua ya kujua kilichomsababisha huyo mtu kunywa.

Anasisitiza tabia ya pombe katika mwili wa binadamu ni kuufubaza kwa maana kuufanya ufanye kazi taratibu ukilinganisha na uhalisia wake.

“Ukinywa pombe mapigo ya moyo yanapungua, shinikizo la damu linapungua, unaweza ukajisikia kulala,” anasema.

Mhadhiri wa Saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Mabula Nkuba anasema pombe inasimama kama dalili ya changamoto katika afya ya akili ya mtu.

Anaeleza wapo wanaokunywa pombe kama sehemu ya burudani kwao, akifafanua kundi hili hunywa kwa kiasi na unywaji wao haushinikizwi na jambo lolote.

Hatari, anasema ni kwa wale wanaokunywa pombe kama sehemu ya kupunguza mawazo au kujisahaulisha matatizo waliyonayo wakati huo.

“Pombe ukiitumia kawaida bila kushinikizwa na msongo, itabaki kama kinywaji ingawa ukiitumia kwa muda mrefu utapata madhara ya kiafya, lakini wanaoitumia kama kichaka cha msongo ndiyo wanaoathirika zaidi,” anasema.

Hata hivyo, anasema anayetumia pombe kusaka furaha wakati wa huzuni anajulikana kwani, mara nyingi hujitenga hata anapokuwa baa.

“Kawaida wanaokunywa pombe wanakuwa pamoja wananunuliana, lakini ukiona mtu amejitenga anakunywa akiwa peke yake, huwa ni wale walioshinikizwa na msongo,” anasema.

Kulingana na Dk Nkuba, wenye msongo hujikuta wakitumia pombe zaidi ya kawaida, kwa sababu ndiyo kitu wanachokifanya kama kisaidizi cha changamoto zao.

“Ukifanya hivi inakufanya uitegemee na ikitengeneza utegemezi huo maana yake inatengeneza kitu kwamba bila pombe mtu hawezi kufanya kazi vizuri,” anasema.

Hata ulevi wa kupindukia, anasema ni moja ya dalili ya matatizo katika afya ya akili.

Mwenye msongo, anasema anaonekana anakunywa zaidi pombe si kwa sababu anaipenda ni kwa kuwa kuna msongo alioshindwa kuuhimili kwa nguvu zake na akachagua pombe kumsaidia.

“Mara nyingi hawa ni watu ambao hawafunguki, hawaongei sana na hata ukiwakuta kwenye maeneo ya unywaji wanajitenga hawakai na wengine, hiyo ni dalili ya tatizo la afya ya akili,” anasema.

Takwimu za matatizo ya akili

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (Unicef) takriban asilimia 20 ya vijana kote duniani wanakabiliwa na matatizo ya akili na kujiua ambayo ni sababu ya pili kuu ya vifo miongoni mwa vijana wa umri wa kati ya miaka 15- 19 kote ulimwenguni.

Inasadikiwa kuwa mtoto mmoja kati ya sita walio na umri wa chini ya miaka 18, ana uwezekano wa kuwa na tatizo la afya ya akili hata hivyo asilimia 75 ya watu hao hawapati huduma ya afya wanayohitaji.

Akisoma hotuba ya bajeti ya Afya kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022 ilihudumia jumla ya wagonjwa 28,325 kati yao 26,761 ni wagonjwa wa akili wa nje (OPD) na wagonjwa wa akili wa ndani (IPD) 1,564.

Aidha, wagonjwa wa msamaha waliopewa huduma walikuwa 3,985 ambao waliigharimu hospitali kiasi cha Sh60.2 milioni katika kipindi hicho.

Jumla ya wagonjwa 123, walipata huduma za kibingwa za saikolojia na wagonjwa 443 wa Neuro-psychiatry na wagonjwa wapatao 123 walifanyiwa uchunguzi na kuandikiwa taarifa za kisheria. Vilevile, katika kliniki ya afya ya akili kwa watoto na vijana wagonjwa 1,121 63 walihudumiwa. “Mirembe ilipokea wagonjwa wapya 225 wenye matatizo ya utumiaji wa dawa za kulevya na hivyo kufanya jumla ya waraibu wanaohudumiwa na kituo cha Itega kufikia 548 tangu kilipoanza kutoa huduma mwaka 2020,” alisema Waziri Ummy.

Mkuu wa Idara ya Afya na Magonjwa ya Akili Hospitali ya Bugando, Dk Catherine Magwiza anasema mtu kuhisi kukataliwa au kuwa na hatia na wakati mwingine kuhisi maisha yake hayana thamani, ni dalili mojawapo kwani wakati mwingine anaweza kuwa na mawazo ya kutaka kujidhuru.

“Mara nyingi tunasema mpaka condition (hali) iitwe ugonjwa lazima iwe imemsababishia kushindwa kufanya shughuli zake za kila siku, kushindwa kuhusiana na jamii yake, kuchangamana na watu na imemfanya amekosa utambuzi hivyo kuna hatua ikifika ndiyo tunasema ugonjwa wa akili,” anasema Dk Magwiza.

Sababu wanaume kuongoza kuwa na matatizo ya akili

Wataalamu wa afya ya akili na wanasaikolojia wanasema sababu wanaume kuongoza kuwa ni pamoja na kuzongwa na majukumu, ugumu wa maisha, utafutaji, malezi, usiri, kukua kwa teknolojia, matarajio ya maisha, sonona, matukio ya nyuma na matumizi ya mihadarati na unywaji wa pombe kupindukia.

Mtaalamu wa afya ya akili na mwanasaikolojia kutoka Taasisi ya Mental Health Tanzania, Dk Philimina Scarion, anasema wanaume hupata msongo wa mawazo ambao mwishowe hufikia sonona na kujikuta wakipata tatizo la afya ya akili.

Anataja usiri kuwa sababu nyingin… “Dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii ni kuwa mwanaume ni mtu mwenye nguvu, hivyo hapaswi kuonyesha udhaifu iwe ameumizwa kihisia na vinginevyo, hivyo wanabaki kuwa wasiri, wanajiuliza maswali na kujijibu wenyewe, mwishowe wanachanganyikiwa,” anasema Dk Philimina.

Anasema wengi hudhani anapoomba msaada wa mawazo au kuweka hisia zake wazi, ni kuonyesha udhaifu tofauti na wanawake, wengi wao huongea na marafiki au kupiga umbea hii inawasaidia mno.

“Wengine wanaathirika na matukio ya nyuma aliyoyafanya hawezi kuongea na mkewe, wengi mwishowe huchanganyikiwa,” anasema.

Mtaalamu wa saikolojia, Dk Saldin Kimangale anasema ongezeko la wanaume pia linakuzwa na matumizi ya dawa za kulevya na ulevi kupindukia.

“Hilo linachochea wao kupata magonjwa ya matumizi ya dawa za kulevya ambapo pia huchochea kupata magonjwa mengine kama ‘bipolar’, ‘schizophrenia’ na magonjwa ya wasiwasi.”

Naye mtaalamu wa saikolojia, Josephine Tesha anasema: “Tusiwaambie watoto wa kiume ‘Jikaze wewe ni mwanaume’ wanaiweka akilini na ina athari kwao baadaye.”

Mkuu wa Kitengo cha magonjwa ya afya ya akili, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk Frank Massao anasema:

“Mara nyingi wanaume wanakumbwa zaidi na tatizo la afya ya akili kuliko wanawake, lakini pia kuna ongezeko kubwa la kasi ya maradhi ya akili.”

Takwimu za Muhimbili zinaonyesha wanaume wakikabiliwa zaidi na tatizo hilo ikilinganishwa na wanawake kwa kipindi cha mwaka 2020/2021.

Kati ya wagonjwa wa nje 24,014 walioonwa mwaka huu, wanaume walikuwa 15,205 ikilinganishwa na wanawake 8,809 ambao ni ongezeko la asilimia 17.

Mwaka 2019/20, wagonjwa walikuwa 20,571 (wanaume 11,560, na wanawake 9011).

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi