Kitaifa
Mbinu kuepuka maradhi ya moyo
Dar es Salaam. Wakati takwimu zikionyesha ongezeko la wagonjwa wa moyo kutoka milioni 2.5 mwaka 2017 hadi milioni 3.5 mwaka 2022, wataalamu wa afya wameshauri namna ya kujilinda na maradhi hayo.
Wameshauri umuhimu wa kufanya mazoezi, kuzingatia lishe bora kwa kula matunda, mboga za majani, vyakula vyenye madini ya potasiamu na kupunguza kula vyakula vyenye kiasi kikubwa cha mafuta, chumvi na sukari.
Pia walishauri watu kuepuka uvutaji sigara na unywaji pombe uliokithiri, kutambua kiwango cha sukari katika mwili, msukumo wa damu na kiwango cha mafuta mwilini.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, akizungumza jana wakati wa maadhimisho ya siku ya moyo duniani, yaliyofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) tawi la Dar Group, jijini Dar es Salaam, alisema kuna haja ya watu kubadilika kwa sababu kasi ya magonjwa hayo ni kubwa.
“Niwasisitize Watanzania wakati umefika kila mtu katika nafasi yake kuchukua hatua, kuzingatia ulaji wa vyakula vinavyofaa, kikubwa ni kupunguza matumizi ya chumvi kupita kiasi, sukari na mafuta pamoja na kufanya mazoezi. Hivi ukivishinda umedhibiti magonjwa ya moyo.
“Tumeangalia magonjwa yasiyo ya kuambukiza mfano kisukari, shinikizo la juu la damu, yameongezeka kutoka asilimia moja mwaka 1980 hadi asilimia tisa mwaka 2020,” alisema Waziri Ummy.
Alisema hayo yamebainika kupitia utafiti uliofanywa na Step Survey hivi karibuni kwa Watanzania wenye miaka 15 na kuendelea na kubainika kwa kila watu 100, 12 wana kisukari na 25 wana shinikizo la juu la damu.
Waziri Ummy alisema shinikizo la juu la damu na kisukari ndicho chanzo kikuu cha magonjwa ya moyo, figo na kiharusi.
Alisisitiza watu wenye shinikizo la juu la damu, kisukari na wapo kwenye matumizi ya dawa, wasiache tiba kwa kuwa wanaangukia kupata matatizo ya moyo, kiharusi na figo.
Mboga na mazoezi
Waziri Ummy alisema takwimu alizonazo, zinaonyesha Watanzania hawali mboga za majani, ikiwa ni asilimia tatu pekee wanaokula kwa usahihi.
“Ndugu zangu kuleni mboga za majani bila kuandikiwa na daktari. Wataalamu mtoe elimu, Watanzania tunapika mboga lakini tunaivisha, ukikutana na Waswahili wa Dar es Salaam wanapenda vitu shatashata wanamwaga mchuzi wa mboga wanatia nazi,” alisema.
Kuhusu ulaji wa matunda, alisema wapo wanaotengeneza juisi kwa matunda zaidi ya matatu, jambo alilosema si sahihi. Aliagiza wataalamu wa lishe kutoa elimu.
Waziri alishauri watu kufanya mazoezi, kwa wastani wa dakika 150 kwa wiki kama inavyoshauriwa na wataalamu.
Aliwapongeza wazee kwa kuwa na mwamko wa kufanya mazoezi, akisema changamoto kubwa ni vijana kutoyafanya.
“Sasa hivi ukipita barabarani utakuta watu wazima wakitembea, nitoe wito kwa watu wazima kufanya mazoezi hakuhitaji kukimbia,” alisema.
Alisema changamoto ambayo amekwishaiwasilisha kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ni Watanzania kupata ajali wakifanya mazoezi kwa kugongwa na pikipiki.
“Tumezindua mpango kwa kushirikiana na sekta mbalimbali kuzuia magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kwa hiyo tumeliwasilisha kwa Waziri Mkuu ili awaelekeze wanaohusika na miundombinu ya barabara kuhakikisha ni rafiki kwa watu kufanya mazoezi,” alisema.
Wataalamu wa afya
Kaimu Mkurugenzi wa JKCI, Dk Angela Mhozya alisema kila kundi kwenye jamii, linasumbuliwa na maradhi ya moyo kulingana na umri, akitoa mfano wenye miaka 15 hadi 45 husumbuliwa zaidi na shida ya mishipa ya moyo.
“Kwa wale waliogundulika kuwa na matatizo ya moyo, wanatakiwa kupima afya kila baada ya miezi sita na wale ambao bado wanashauriwa kupima kila mwaka,” alisema.
Dk Angela alisema matatizo ya moyo yanaongezeka kwa asilimia 25 kwa mwezi kwenye taasisi hiyo, huku asilimia 25 hadi 30 ya wanaofanyiwa uchunguzi wakibainika kuwa na maradhi hayo.
Rais wa chama cha madaktari wa moyo (TCS), Dk Robert Mvungi alisema asilimia 13 ya vifo vinavyotokea nchini, vinachangiwa na matatizo ya moyo.
Kwa duniani, alisema watu milioni 20 hupoteza maisha kutokana na matatizo ya moyo.
Shinikizo la damu
Wakati wagonjwa wanaougua shinikizo la damu wakitajwa kuongezeka nchini, takwimu za JKCI zinaonyesha ongezeko hilo kuwapo kwa vijana kuanzia umri wa miaka 20 mpaka 40.
Takwimu zinaonyesha kuna ongezeko la watu 890,788 sawa na asilimia 3.8 ikilinganishwa na asilimia 3.6 mwaka 2021/22.
Kwa wagonjwa wanaotibiwa JKCI kati ya wagonjwa 83,356 waliotibiwa mwaka 2022 asilimia 66.8 (sawa na watu 59,022) walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu.
Mkuu wa kitengo cha utafiti na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo JKCI, Pedro Palangyo, alisema tafiti za hivi karibuni zimebaini licha ya vyanzo vikuu vitano, uchafuzi wa hewa ni chanzo kikuu cha magonjwa ya moyo.
“Tunapovuta hewa isiyo safi tafsiri yake ina kemikali kadhaa na hizo zinajumuisha hewa ukaa, salfa dayoksaidi na nitrojeni dayoksaidi, ambazo zinaweza kuharibu moja kwa moja mfumo wa damu, moyo na mishipa ya moyo.
“Kwanza inakwenda kufanya mishipa ya moyo inakazika, inapoteza uwezo wake wa kusinyaa na kutanuka ili iweze kusukuma damu. Kemikali zikiharibu mishipa inaifanya kuanza kuziba kwa kujaa taka na mafuta na matokeo yake kupunguza upenyo wa damu kupita, hivyo tunaanza kupata vifo vya ghafla na kuziba kwa mishipa ya damu,” alisema.
Dk Pedro alisema kwa sehemu kubwa suala la uchafuzi wa hewa linahusishwa mtu unapovuta kwa njia ya hewa, gesi ambazo zina sumu au kemikali.
“Sasa kwa kuwa hewa iliyovutwa siyo safi, hizo seli zitapokea kemikali moja kwa moja kupitia damu kwa kuwa inakwenda kwenye mishipa ya damu na moyo wenyewe, hivyo inapunguza upenyo na inafanya mishipa kuwa migumu na ikiharibika magonjwa makuu matano ya moyo yanajitokeza,” alisema.
Daktari mshauri mwandamizi wa magonjwa ya ndani na moyo wa JKCI, Profesa Harun Nyagori alisema asilimia kubwa ya wagonjwa hawana dalili, ambao ni asilimia 60, huku asilimia 40 wakipata dalili za miguu kuvimba, kifua kuuma, kushindwa kupumua, moyo kwenda mbio, kizunguzungu na uchovu anapotembea.
Akitaja gharama za kutibu magonjwa ya moyo, mkuu wa Idara ya ukusanyaji mapato wodini JKCI, Joyce Mgaya alisema kwa kawaida wagonjwa wa rufaa wamekuwa wakilipiwa na Serikali asilimia 70 ya gharama na wao wamekuwa wakiwajibika kulipia asilimia 30.
Alisema gharama hizo ni katika vipimo, kumuona daktari, kitanda iwapo atalazwa lakini pia matibabu mengine ya mwendelezo ikiwamo gharama za upasuaji.
“Gharama zinatofautiana lakini hata wagonjwa wa rufaa na msamaha lazima walipie asilimia 30 ya gharama na upasuaji zinazoanzia Sh2 milioni mpaka Sh29.2 ikiwa moyo wako utashindwa kufanya kazi. Matibabu ya mwisho ni kuwekewa betri ya moyo inayogharimu Sh29 milioni ndani ya nchi,” alisema.
Walichosema wadau
Chama cha ACT- Wazalendo katika kusherekea siku ya moyo duniani, kiliishauri Serikali kuhakikisha kila Mtanzania anapata matibabu bila kikwazo chochote, kupitia bima ya afya inayotokana na hifadhi ya jamii.
“Serikali iimarishe huduma za afya ya msingi kwa watu wenye magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yasiyoambukiza, kwa kuweka kipaumbele kwenya matatizo ya upungufu wa miundombinu, ukosefu wa dawa, upungufu wa wafanyakazi wa afya katika ngazi ya afya ya msingi, yaani zahanati na vituo vya afya, wenye mafunzo ya kuzuia, kutambua, na kuwasaidia watu wenye magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yasiyoambukiza,” inaeleza taarifa kwa umma iliyotolewa na chama hicho.
Radhia Jumanne, aliyejitokeza kupima afya, alisema alibainika kuwa na shinikizo la damu bila kufahamu.
“Nimepima nikaambiwa nina shinikizo la juu la damu na hii ni kutokana na namna ninavyokula. Nimeambiwa nipunguze matumizi ya mafuta na chumvi kwa wingi, tayari nimeanza matibabu,” alisema.