Kitaifa
Serikali Zanzibar yasitisha bei mpya ushuru za bandarini
Baada ya kuibuka sintofahamu katika Bandari ya Malindi Zanzibar kuhusu mabadiliko ya ushuru, Makamu wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla amefanya ziara maalumu kujionea hali hiyo huku akiwataka wadau wa bandari kukubali mabadiliko.
Tangu Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) lilipokabidhi bandari hiyo kuendeshwa ana mwekezaji Kampuni ya Africa Global Logistics (AGL) ya Ufaransa, Septemba 18, 2023 kumeibuka malalamiko ya kuongezeka kwa ushuru katika bandari hiyo na kusababisha baadhi ya shughuli zisimame.
Wadau wa bandari hususani wa majahazi wanalalamikia kupandishiwa ushuru mara mbili ya bei iliyokuwapo awali, hata hivyo bei hizo zimeelezwa kuwa ndio bei halali kwa mujibu wa kanuni za mwaka 2018 lakini zilikuwa hazifuatwi.
Bila mamlaka kuanisha bei maalumu zilizokuwapo awali kwa madai ya kuwa ni mchanganyiko, baadhi ya wafanyabiashara hao walitolea mfano wa kuingiza gari aina ya kontena kulazimika kulipia zaiid ya Sh100,000 kutoka Sh56,000 ya awali.
Akizungumza na wadau hao leo jioni Septemba 21, 2023 Hemed amesema nia ya Serikali ni njema na imeamua kuweka mwekezaji huyo ili kuleta ufanisi katika bandari hiyo ambayo ilikuwa ikilalamikiwa na wafanyabiashara.
“Baada ya kuona malalamiko haya tumeagiza kwanza bei mpya zitishwe tuendelee na bei zile za awali,” amesema na kuongeza kuwa.
“Mwelekeo wa Serikali ni kusimamia makubaliano ili kuleta ufanisi, lakini niwaombe ndugu zangu lazima tukubali mabadiliko haya masula ya mazoea yanatukwamisha,” amesema
Pia amewataka watu wanaotumia suala hilo kujikuza kisiasa waache maana serikali ndiyo imeamua kusitisha bei hizo mpya bila kupokea maagizo kutoka kwa mtu yeyote.
Ili kuleta ufanisi katika bandari hiyo pia ameagiza kuhakikisha benki zinafanya kazi ndani ya saa 24 badala ya kufunga ofisi saa 11:00 jioni.
Awali Waziri wa Ujenzi, Mawalisiliano na Uchukuzi, Dk Khalid amesema laima utaratibu ubadilishwe lakini jambo kubwa ni uelewa kwa wananchi hao.
Naye Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya amesema kwa sasa mambo yanabadilika huko mbeleni hakuna mambo ya mazoea.
“Haya ndiyo mabadiliko tunayoyasema lazima tukubaliane nayo, katika kukuza uchumi hatuwezi kwenda kwa mazoea,” amesema.
Mwenyekiti wa Wawakala wa Usafirishaji, Omar Makame amesema baada ya kurejesha bei hizo shughuli za kushusha mizigo zimendelea kama kawaida.
Tunashukuru angalau kilio kimesikiaka shghuli zinaendelea lakini kikubwa mambo haya yanatakiwa elimu vinginevyo yanaweza kuleta atahari kubwa baadaye,” amesema.