Kitaifa
Bei ya Petroli Zanzibar yashuka
Unguja. Wakati bei ya Petroli Tanzania Bara ikifikia Sh3, 213 kwa lita moja,hali ni tofauti visiwani Zanzibar ambapo Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura), imetangaza bei mpya za mafuta huku bei ya Petroliikishuka kutoka Sh2,970 hadi Sh2,950.
Kuipitia taarifa ya mamlaka hiyo iliyotolewa kwa umma leo Ijumaa Septemba 8, 2023, Zura imesema mafuta ya ndege na yale ya dizeli ndio pekee bai zake zimepanda.
Kulingana na taarifa hiyo, bei ya diseli imepanda kutoka Sh2, 843 kwa mwezi Agosti hadi kufikia Sh3, 012 kwa mwezi Septemba, huku bei ya mafuta ya taa yakibaki Sh2, 921 kama ilivyokuwa mwezi Agosti.
Kwa bei ya mafuta ya ndege lita itauzwa kwa Sh2, 448 kwa mwezi Septemba tofauti na Sh2, 365 iliyouzwa mwezi Agosti.
“Sababu ya kuongezeka kwa bei ya diseli na mafuta ya ndege ni kuongezeka kwa bei katika soko la dunia kwa asilimia 21, gharama za bima na usafirishaji kwa asilimia 62 ikilinganishwa na mwezi Agosti,” iliandikwa kwenye taarifa hiyo.
Kufuatia ongezeko hilo la bei ya mafuta ya ndege na yale ya diseli, Zura imewasisitiza wananchi kuhakikisha wananunua mafuta katika vituo halali na kudai risiti za kieletroniki.
Hali ikiwa hivyo Zanzibar, hivi karibuni Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) ilitangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli Tanzania bara kufikia Sh3,213 kwa Petroli, huku dizeli ikiwa ni Sh3,259; na mafuta ya taa bei yake kuwa Sh2,943 kwa mafuta ya taa.
Kwa taarifa za Ewura mabadiliko hayo yanatokana na kupanda kwa gharama za mafuta katika soko la dunia kwa hadi asilimia 21, gharama za uagizaji wa mafuta hadi asilimia 62 na maamuzi ya kisiasa katika nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi (OPEC+).