Connect with us

Kitaifa

Wabunge wacharuka mfumo uagizaji mafuta

Dodoma. Wakati wabunge wakitaka hatua zichukuliwe ili kukabiliana na uhaba wa mafuta nchini, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ametaka Serikali ifanye tathimini ya mfumo mpya wa uagizaji mafuta.

Dk Tulia alisema hayo Dodoma jana mchana wakati akiahirisha shughuli za Bunge huku akisisitiza hoja iliyoibuliwa asubuhi na mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi alipomuuliza swali Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhusu wananchi kuhangaika kupata mafuta.

Shangazi alisema kumekuwa na sintofahamu kuhusu suala la mafuta kwa kuwa licha ya bei zinazopanda kila wakati mafuta hayo huwa hayapatikani lakini inapofika Jumatano ya kwanza ya mwezi ambayo ni siku ya kutangaza bei upya, huanza kupatikana.

Swali la mbunge huyo limetokana na kile kilichoshuhudiwa wiki iliyopita maeneo mbalimbali nchini wananchi wakihangaika kupata mafuta kutokana na baadhi ya vituo kufungwa kwa madai huduma hiyo ilikuwa haipo.

Hata hivyo, baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya Jumanne usiku huku ikionesha kupanda, huduma hiyo ilirejea kwenye vituo vilivyokuwa haviuzi kwa sababu ya kutokuwa na mafuta.

Shangazi aliibua suala hilo katika kipindi cha maswali na majibu kwa Waziri Mkuu alipohoji Serikali imeweka mikakati gani kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unakuwa mzuri nchini.

Akijibu swali hilo, Majaliwa alikiri uwapo wa changamoto hiyo lakini akasema zipo jitihada zinazochukuliwa na Serikali kuondokana na tatizo hilo kwasababu nishati hiyo ndiyo injini ya uchumi.

Alisema tayari Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Naibu Waziri Mkuu Dk Doto Biteko ambaye ameanza kushughulikia jambo hilo kwa kukaa na wadau mbalimbali.

“Niendelee kumuagiza naibu waziri mkuu aendelee kushughulikia hili ndani ya wiki moja tuwe na majibu na katika hilo wapanue wigo kwa waagiza mafuta ili tuwe na mafuta ya kutosha na suala la bei tutaangalia huko mbele,” alisema.

Spika Tulia alisema ni wakati wa Serikali kufanya tathimini ya Mfumo mpya wa Uagizaji wa Mafuta wa Pamoja (BPS).

Alisema haiwezekani mafuta yakawepo ndani ya wiki mbili za mwanzo wa mwezi lakini baada ya hapo kunakuwa na shida ya upatikanaji wa nishati hiyo.

“Bei ikitangazwa tu mafuta yanaanza kuwepo sasa kama huu mfumo unatupelekea kwenye changamoto nyingi kuliko ule wa kwanza basi tuangalie namna ya kuboresha ule uliokuwepo zamani,” alisema Spika Tulia.

Alisema kama mfumo wa BPS una mianya ambayo imeachiwa basi kufanyike kwa tathimini kuonyesha maeneo ambayo mianya ipo ili iweze kuzibwa kwa kuwa wanaona foleni ya mafuta lakini ghafla inaondoka baada ya bei mpya kutangazwa.

Alisema kufanyika kwa tathimini hiyo kutaisaidia Serikali lakini na wabunge kuona wapi wanaweza kuwasaidia katika jukumu lao la kuisimamia Serikali.

Wakizungumza katika viwanja vya Bunge na gazeti hili, wabunge waliitaka Serikali kuangalia kama bado ni sahihi kwa Serikali kujiondoa katika biashara hiyo ya mafuta.

Mbunge wa Sengerema (CCM), Hamis Tabasamu alitaka kufanyike tathimini kama Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) linapaswa kuendelea kutoagiza mafuta nchini kwa sasa au la.

Tabasamu ambaye pia ni mwenyekiti wa wafanyabiashara wa mafuta wadogo mkoani Geita alisema Serikali inapaswa kuangalia sheria na kanuni zinazohusu uagizaji wa mafuta kama bado zinalifaa Taifa.

“Leseni za biashara ya mafuta zinatolewa na Ewura, sio wizara yetu ya viwanda na biashara ambaye ndiye mwenye dhamana ya utoaji wa leseni za biashara kwa sheria ya mwaka 1972. Tunapaswa kuangalia je ni sahihi kufanya hivyo,” alisema Tabasamu.

Mbunge wa Mpanda Vijijini (CCM), Moshi Kakoso alisema hali ya upatikanaji wa mafuta katika jimbo lake hadi jana ni mbaya na kwamba lita moja ya mafuta ya dizeli ilikuwa ikiuzwa kwa Sh5,000.

Mbunge wa Kigoma Mjini, (CCM), Kilumbe Ng’enda alisema hali ya upatikanaji wa mafuta katika jimbo lake ni nzuri na kwa bei iliyopangwa na Ewura.

 Wakati huohuo, Chama cha Wamiliki wa Malori wa Kati na Wadogo (TAMSTOA) walikutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana na kuitaka Serikali kuja na mwarobaini wa kushusha bei ya mafuta badala ya kujikita kwenye kutafuta ufumbuzi wa upatikanaji wake.

Mwenyekiti wa chama hicho, Chuki Shabani alisema inasikitisha kuona Zambia wanaochukulia mafuta hapa nchini bei yao ya mafuta ni Sh999.

Kama haitoshi visiwani Zanzibar nako bei ya mafuta ipo chini kwa kuwa mpaka kufika jana petroli ilikuwa ikiuzwa Sh2,893 na kuhoji Serikali inakwama wapi kutafuta suluhu ya kupunguza bei ya bidhaa hiyo.

“Leo hii wasafirishaji hatujui bajeti ya kusafirisha mzigo kwa sababu kila leo mafuta yanapanda na haujui yatapanda kwa shilingi ngapi,kwa kweli inatuumiza ukizingatia wengi wanapenda kuweka mafuta yao nchini hata kama wanasafiri kwenda nje ya nchi,”alisema Shabani.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi