Kitaifa
Rais Samia akemea viongozi wanaosubiri maelekezo kutoka ‘juu’
Dar es Salaam. Ule mtindo wa viongozi wa umma, kutekeleza majukumu kwa kusubiri maelekezo kutoka juu huenda unakwenda kukoma, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwapa uhuru wa kufanya kazi kwa kufuata mipango na mikakati yao na kukemea kuogopa kutoa maamuzi hadi maelekezo kutoka ‘juu’.
Licha ya kuwapa uhuru huo, Mkuu huyo wa nchi, amewataka mipango yao isiende kinyume na sheria, kanuni na taratibu za Serikali Kuu.
Rais Samia ametoa ruhusa hiyo leo, Jumapili Agosti 27, 2023 alipohutubia hafla ya kufunga mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa, yaliyofanyika katika Taasisi ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.
Amesema katika uongozi wake hatashusha maelekezo kwa viongozi hao kuhusu nini wanapaswa kufanya, badala yake anataka kuwaona wanakuwa na ndoto kulingana na mipango ya Serikali.
“Usisubiri Rais aseme Mkuu wa Mkoa fanya hili huko, ile ilikuwa zamani, enzi za Mwanri (Mkuu wa Mkoa wa zamani wa Tabora) mimi napenda kuona mtu anajituma, anajielewa anajua nini anafanya,” amesema.
Hata hivyo, ametaka kwenye ndoto zao hizo wasiyumbishwe huku akiwasihi kuwa na jawabu iwapo wanachokifanya kitahojiwa.
Lakini, amewataka kusimamia maamuzi yao, huku akionya hilo lisiwafanye kutokubali ushauri wa wengine.
“Naposema kusimama kwenye maamuzi yako sio muende huko kichwa ngumu mnachotaka ndo hicho hicho, hapana, unaangalia mazingira yaliyopo na unafanya kulingana na miongozo ya kisheria,” amesema.