Kitaifa
Kamari janga hatari vyuoni
Michezo ya kamari kwa kawaida huwa ni chungu na tamu kwa wachezaji wake, lakini kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kwao imekuwa ni shubiri.
Michezo hii ambayo kwa sasa inatajwa kuteka watu wa rika, jinsi na jinsia mbalimbali, imekuwa maarufu nchini kiasi cha kuwaibua baadhi ya watu hasa viongozi wa kidini kukemea michezo hiyo, ambayo hata hivyo, inatajwa kuwa chanzo cha mapato kwa Serikali.
Katika siku za hivi karibuni kumeibuka kundi la wanafunzi wa vyuo vikuu kuzama kwenye michezo hiyo, ambayo imetajwa kuwa mojawapo ya vyanzo vya baadhi yao kukatisha masomo yao kwa kukosa fedha za ada na hata za kujikimu.
Licha ya Serikali kuruhusu michezo hiyo na kuwatoza kodi wachezeshaji, kwa upande wa pili ni michezo inayowaumiza zaidi washiriki wake, kusababisha kuyumba kwa uchumi wa watu binafsi na hata jamii.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini baadhi ya wanafunzi wamekuwa washiriki wazuri wa kamari kwa aina zake mbalimbali ikiwamo kubashiri (kubeti) matokeo ya michezo hususan soka, kucheza kwa kutumia mashine maarufu ‘mchina’ na hata kwa kutumia mchezo wa ‘pool table.
Ushuhuda
Mhitimu katika Chuo cha Biashara cha jijini Dar es Salaam, Elikana Hoya anasema katika aina hizo tatu za kamari, mchezo wa mashine ndiyo unaopendelewa zaidi na vijana, huku ukiwaacha na maumivu.
“Mimi ni miongoni mwa waliokuwa wanacheza nikiwa chuo,nasema kweli kuna siku nililiwa fedha nikatamani kutembea kutoka Dar es Salaam kuja Bahi (Dodoma),’’ anasema.
Kwa mujibu wa Hoya, kuna wakati alicheza Sh50,000 akapata Sh170,000 lakini kila siku alikuwa akicheza mwisho Sh10,000 na kuliwa na kwa mara ya mwisho akiwa mwaka wa mwisho, alicheza Sh400,000 za matumizi ya muhula wote na fedha hizo aliliwa ndani ya dakika 20.
Hali hiyo anasema ikamlazimu kuishi Kimara ambako kila siku jioni alikuwa akilazimika kufanya kibarua cha kusomba mchanga na kuuza ili kukwepa kurudi nyumbani.
Ukiondoa kamari ya kwenye mashine, anasema mchezo mwingine ni ubashiri kwa timu za mpira ambao anataja kuwa gharama yake huwa siyo kubwa, licha ya kuwa wachezaji wake wanaliwa.
Ushuhuda mwingine ni wa mwanafunzi wa Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST), Kelvin Isote, anayesema anao mfano kwani jambo hilo kwani lilishampata rafiki yake wa karibu.
“Rafiki yangu tulikuwa wote ngazi ya diploma, kila wakati alikuwa ni mtu wa kubeti, yaani hakuwa anasikia chochote kutoka kwa mtu yeyote zaidi ya kuwaza kubeti, matokeo yake yalimkuta ya kumkuta na masomo ikawa ndiyo basi,” anasema Isote.
Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, rafiki yake alikuwa akitumia fedha nyingi na mara chache aliweza kubeti na kupatia lakini anazoliwa zilikuwa nyingi zaidi ya zile alizokuwa akizipata hivyo kusababisha maisha yake kwa ujumla kuwa mabaya.
Kamari tangu sekondari
Wakati hawa wakieleza hayo, Ibrahim Andrew ana simulizi nyingine ya mtoto wa mama yake mdogo aliyeanza uraibu wa kamari tangu akiwa sekondari. Akafika chuo akashindwa kumaliza kwa sababu ya ‘kutafuna’ fedha yote kwenye kamari.
“Huyu mdogo wangu (anamtaja jina) ana miaka zaidi ya saba ameshindwa kumaliza chuo licha ya kupata mkopo asilimia 100 enzi za utawala wa (Jakaka) Kikwete, hela alikuwa akichukua anakwenda kuicheza kamari,” anasema.
Anaongeza: “Ilifika wakati anaicheza kamari hela yote na kumfanya kushindwa kuwa na hela za kujikimu, anarudi nyumbani kwa mama mdogo anakwapua vitu ndani na kwenda kucheza kamari.”
Andrew anasema mdogo wake huyo alianza kucheza kamari tangu akisoma sekondari jijini Dar es Salaam. Alipofika chuo, alikokuwa anasomea uhandisi wa umeme, alipewa mkopo wa asilimia 100 ambao ndio uliomchanganya akili.
‘’ Mpaka sasa ameshindwa kuendelea kwani darasani alikuwa haingii, anafeli ovyo na mwisho akajifukuza kwenyewe kwa kutokwenda chuo,’’ anaeleza.
Andrew anasema kamari imekuwa tatizo kubwa na kama isingekuwa hivyo mdogo wake angekuwa amemaliza chuo lakini sasa imemfanya asiwe na mbele wala nyuma.
‘’Amesababisha hasara kwani kuna kipindi alianza kuiba na kukamatwa na kuwekwa polisi, ili kumtoa, mama mdogo alilazimika kuuza mashamba. Unajua baba mdogo alikwishafariki, kwa hiyo mama mdogo ndio anawasimamia na wako watoto wanne, lakini huyu amekuwa msumbufu na kama mateso kwenye familia. Asingekuwa najihusisha na kamari si ajabu angekuwa amemaliza hata chuo na kumsaidia mama mdogo,” anasema
Wasemacho walezi vyuoni
Walezi wa wanafunzi wa baadhi ya vyuo vikuu jijini Dodoma, wanakiri kuwa michezo hiyo imepoteza ndoto za vijana wengi na kuwafanya kuwa watumwa huku wengine wakifikia hatua ya kukacha masomo yao.
Baadhi ya wanafunzi nao wanakiri kuwa kamari ni changamoto kwa maisha ya wanavyuo hasa kundi la wanaume. Ni changamoto nyingine baada ya ile ya miaka nenda rudi ya baadhi ya vijana wa kiume kike kuingia kwenye uhusiano na kuishi kama mke na mume wakiwa masomoni.
Kuhusu hilo la uhusiano, kijana wa kiume analazimika kuwa kama baba wa familia na kijana wa kike analazimika kuwa kama mke kamili. Unaweza kuona namna gani uhusiano huu unavyoweza kuwa na athari katika masomo yao. Lakini hilo mosi, pili ni hili janga jipya la wanafunzi kuanzisha uhusiano na uchezaji kamari, ambao ni hatari zaidi.
Akizungumza katika kongamano la mapambano dhidi ya rushwa llilofanyika hivi karibuni jijini Arusha,Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Lughano Kusiluka alisema kamari imekuwa ni tatizo sugu kwa vijana vyuoni.
Profesa Kusiluka alisema kundi kubwa la wanafunzi linamaliza hela ya ada kwenye kamari na kusababisha waanze kuhangaika kwenye kulipa ada hadi wiki ya mwisho ya mitihani ambapo kisheria wanapaswa kufukuzwa.
Makamu huyo alisema kuwa wanafunzi wengi wanaonekana kuonewa vyuoni wanapobanwa kuhusu ada, lakini kiuhalisia pesa wanazitumia kwenye kamari na starehe nyingine na zikishamalizika wanatafuta namna ya kuonekana hawana hatia.
Profesa Kusiluka ambaye ni kiongozi wa wakuu wa vyuo vikuu upande wa malezi ya wanafunzi, alieleza kuwa wanaokumbwa na kadhia hiyo siyo vijana wanaotegemea wazazi wao pekee, lakini hata wanaopata mikopo ya Serikali.
“Mwanafunzi anapewa mkopo na Serikali, akipokea anakwenda kubeti, anafanya starehe mbalimbali, hela ikianza kuisha utaona anapika bwenini na wanajua tumekataza kupika bwenini. Pesa ikiisha anakuja ofisini na kuanza kulia akisema ni mtoto wa mkulima. Kumbuka huyu anayejiita mtoto wa mkulima amepewa hela na Serikali ya kujikimu,’’ alisema Profesa Kusiluka
Alisema kuwa wengine wanapokwenda ofisini kwake huwa analazimika kupiga simu kwa wazazi wa watoto, ili ajiridhishe na ndipo hugundua kuwa walipewa ada ya kulipa lakini hawajalipa.
“Ukichukua hatua ya kumpigia mzazi anakwambia nimempa ada, sasa changamoto mimi pale nipo makao makuu, wabunge na viongozi wengine wako pale, unaweza ukasikia wanafunzi kadhaa wakataliwa kufanya mtithani lakini hawajui nyuma ya pazia nini kimetokea. Mwanafunzi huyo huyo akiona ubao umeharibika anaanza kuitisha maandamano, ‘’ aliongeza Profesa Kusiluka.
Makamu huyo anasema mambo hayo yanasabisha wanafunzi wengi kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa hasa watoto wa kike kujihusisha na rushwa ya ngono ili waweze kupata ada na mahitaji mengine.
Mlezi wa wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha St John’s Johaiven Bikongolo anakiri kuwapo kwa matatizo makubwa wanayokutana nayo wanafunzi mojawapo likiwa hilo la kushiriki michezo ya kubashiri.
Bikongolo anasema tatizo hilo halihitaji dawa ya namna nyingine isipokuwa ni kupelekea elimu inayofaa kwa vijana ili kusudi waweze kubadilika na kujua madhara ya kamari.
“Mimi hapa kwangu (St John’s) tatizo siyo kubwa kama ambavyo linaweza kuwa katika maeneo mengine, sisi tuna wanafunzi wachache wanaopata mkopo ambao hawazidi 2,000 walio wengi wanalipiwa ada na wazazi wao, lakini kweli wapo wenye tabia hizo,” anasema Bikongolo.
Anabainisha kuwa, fedha nyingi vijana wanaliwa kwenye kubashiri michezo ya mpira ambako wanaona kama vile wanaweza kupata faida lakini matokeo yake huwa ni mabaya kwao.
Akizungumzi namna ya kuwasaidia wanafunzi kuepukana na jambo hilo, anasema wanacho chama chao ambacho kinahusika na ushauri na malezi kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu (TACOGA), ambacho mlezi wake ni Profesa Kusiluka ndicho kimekuwa na kazi kubwa ya kuwakumbusha vijana namna ya kuishi.
Kwa upande wake mlezi wa wanafunzi katika Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP) Jane Mchakama, alisema hali ya maisha kwa baadhi ya wanafunzi inatia huruma kutokana na kumaliza fedha za mahitaji kwenye Kamari.
Mchakama alisema idara yake imekuwa na kazi kubwa ya kuwapa elimu wanafunzi kuanzia mwaka wa kwanza pindi wanaporipoti chuoni hapo ili watambue madhara wanayoweza kuyapata kwenye michezo hiyo.
Anakiri kuwa, kubeti kumesababisha baadhi ya wanafunzi kufikia hatua ya kuchukia maisha na kuona si kitu kwani wanajikuta kwenye wakati mgumu zaidi kuliko walivyodhani.
Licha ya kutokuwa na takwimu sahihi za wangapi wameacha masomo na ambao wanaishi maisha madumu kutokana na kuendekeza michezo hiyo, anasema siyo kwa vyuo vya mbali, bali hata kwake tatizo lipo.
Kwa upande wake, mlezi wa wanafunzi Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino cha Mwanza, Liberatus Ndegeulaya, anakiri kuwepo kwa tatizo katika chuo hicho kinachomilikiwa na taasisi ya dini.
Anasema baadhi ya vijana wanajikuta kwenye wakati mgumu kimaisha kutokana na kutumia pesa zao vibaya kwenye michezo hiyo.
“Hapa Mwanza kuna tatizo, vijana wakipata mkopo wanaelekeza kwenye michezo ya kubashiri na hasa mpira wa miguu,wanaliwa sana na wengine kwenye michezo ya mashine, baada siku mbili huwa wamechacha hivyo kuyafanya maisha yao kuwa ya tabu hadi mkopo mwingine unapokuja,” anasema Ndegeulaya.
Mmoja wa wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Nelson Mandela cha Arusha alisema kwao tatizo hilo lipo ingawa siyo kwa ukubwa kwa alichoeleza kuwa wengi wanasoma hapo wakitokea kazini.
“Tatizo kweli lipo, ninachokiona ni kwenye michezo hii ya kutumbukiza pesa yaani wanaliwa sana na hasa vijana wa kiume, ingawa kusema kweli naona wengi wanajitambua, au kwa sababu wanatoka kazini,” alisema huku akiomba jina lake kuhifadhiwa.
Aliyekuwa Rais wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe George Lubeleje alisema katika mazingira ya vyuo kuna mambo mengi lakini tatizo ni namna ya watu wanavyobadili mitindo ya maisha.
Lubeleje alisema suala la kubeti ni kubwa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kuliko hata linavyotazamwa kwa sasa, kwani linasababisha hata viwango vya ufaulu kwa wanafunzi kushuka kutokana na kutumia muda mwingi kwenye kamari hizo.
“Kitu wasichokijua watu ni kwamba, kumekuwa na shida kubwa kwa sababu ya mapenzi ya mipira. Watu wanashinda kwenye kubeti na kweli siyo kupoteza fedha lakini hata muda wao unapotea sana mwishowe anakuja kusoma kwa mtindo wa zimamoto,” alisema Lubeleje.
Wazazi nao
Hosea Mhechela ambaye ni mzazi wa mwanafunzi anayesoma Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, alisema maisha ya vijana wanapokuwa mbali na wazazi wao yamekuwa na shida kwani wanabadili mitindo ya kuishi.
Mzazi huyo alipendekeza kuwa, ufike wakati Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) liongezewe bajeti ili kusudi wawe wanawaweka muda mrefu vijana waliomaliza kidato cha sita, kwani wanaotoka huko baadhi wamekuwa na mabadiliko kwa kujitambua.