Kitaifa
Rais ampa rungu Profesa Kitila
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Mipango na Uwekezaji kutafuta watu wenye uwezo mkubwa wa kufikiri ndani na nje ya nchi ili wasaidie kufikiri na kupanga maendeleo ya Taifa.
Alitoa agizo hilo Julai 14, 2023, wakati akiwaapisha viongozi aliowateua, wakiwemo mawaziri, watendaji wa Serikali na wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Julai 5 mwaka huu, Rais Samia alibadilisha muundo wa wizara mbili; iliyokuwa Wizara ya Fedha na Mipango ambayo sasa ni Wizara ya Fedha na iliyokuwa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ambayo sasa ni Wizara ya Viwanda na Biashara, huku sekta zilizoondolewa zikiwekwa kwenye wizara mpya ya Mipango na Uwekezaji.
Baadhi ya walioapishwa ni Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba na naibu wake, Hamad Chande; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji na naibu wake, Exaud Kigahe na Profesa Kitila Mkumbo, anayekwenda Wizara ya Mipango na Uwekezaji.
Rais Samia alisema Wizara ya Mipango na Uwekezaji ni muhimu kwa sababu ndani yake kuna Msajili wa Hazina, Kituo cha Uwekezaji na Tume ya Mipango.
Aliwataka watafute ‘vichwa vizuri’ vitakavyosaidia kufikiri na kupanga maendeleo ya nchi. Alimtaka Profesa Kitila kwenda kuwa kamisaa na mratibu mzuri, ili maeneo hayo matatu yafanye kazi.
Alisema wanakosolewa mitandaoni baada ya kuamua na kupanga, lakini kama wanaona watu wazuri nje wawachukue, ili wawe sehemu ya Tume ya Mipango, wakafikiri pamoja na kuondoa vuguvugu kwamba wamepanga nini.
Rais alisema wameweka taasisi hizo tatu katika wizara hiyo, ili Serikali isomane na jambo litakalotoka hapo litakuwa limefikiriwa upande wa uwekezaji na Msajili wa Hazina atakuwa ametoa maoni na watu wa mipango watakuwa wamepanga.
“Kukiwa na uratibu mzuri, muungano mzuri kati yenu kwa maeneo matatu hayo, tunategemea maendeleo yetu yatakwenda haraka na itakwenda kwa ufanisi mkubwa na kwa umakini. Hatuendi kufanya try and error (kujaribu na kukosea), tunakwenda kufanya uamuzi kwa umakini.
“Kwa hiyo hongera, lakini kuna kazi kubwa mbele yako na timu yako, Mafuru na wenzie hiyo ndiyo kazi yenu,” alisema.
Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alimpongeza Rais Samia kwa kuirudisha Tume ya Mipango kwa sababu maendeleo endelevu hayatokei ghafla bila kupangwa na kwamba ujenzi wa nchi ni matokeo ya juhudi za kujenga nchi.
Dk Mpango, aliyewahi kufanya kazi Tume ya Mipango, alimpongeza Lawrence Mafuru kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa tume hiyo.
Hata hivyo, alisema ana kazi kubwa tatu ambazo ni kubainisha hali halisi ya maendeleo ya nchi, kubadilisha mwelekeo kimkakati na kuongoza maandalizi ya Dira ya Taifa ya mwaka 2050.
“Ukaongoze ufanyaji wa hizo kazi kwa kushirikiana na wizara zote na kwa msisitizo, ukashirikiane sana na sekta binafsi, lakini pia chama tawala (CCM), Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Benki Kuu ya Tanzania, Wizara ya Fedha na wizara nyingine,” alisema Dk Mpango.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma alisema anaamini kwa ahadi walizozitoa zitabaki ndani ya mioyo yao na watakwenda kuzifanyia kazi.