Connect with us

Kitaifa

Samia ataja fursa kwa wahitimu JKT

Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza Programu ya Kujenga Kesho kwa Vijana (BBT) iunganishwe na shughuli za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili vijana wanaomaliza mafunzo ya JKT na kukosa ajira, wapate mahali pa kwenda.

Hivi sasa vijana wa BBT wanapatikana kupitia kujaza fomu zinazopatikana katika tovuti inayoendeshwa na Wizara ya Kilimo.

Hata hivyo, utaratibu huo unalalamikiwa na wananchi na wabunge wakidai wanaochukuliwa si walengwa wa mpango bad ala yake wakitaka vijana wa vijijini wanaojishughulisha na kilimo ndio wachukuliwe kwenye mpango huo.

Akizungumza jana katika kilele cha maadhimisho ya miaka 60 tangu JKT iasisiwe, Rais Samia alisema lengo la programu hiyo ambayo iko chini ya Wizara ya Kilimo, ni kuwawezesha vijana kufanya kazi za kilimo, ufugaji, uvuvi na uchumi wa bluu.

Alisema lengo la Serikali la kuunganisha shughuli zinazofanywa na JKT na zile za BBT ni kutaka kupata matokeo katika miradi hiyo.

“Tunataka kuwajengea kesho nzuri vijana na wanapotoka pale (JKT), wajue wanakwenda wapi na wanakwenda kufanya nini. Sasa hivi wakihitimu hapa kama hawakupata nafasi za ajira, wanazubaa mitaani. Tunakwenda kuunganisha mpango wa BBT na kinachofanyika JKT ili vijana wawe na mwelekeo mzuri,” alisema Rais.

Aliagiza Wizara ya Ulinzi na JKT kuandaa mpango mkakati wa kurekebisha kambi za JKT na kuwataka kuanza na upande wa malezi ya vijana ili Serikali nayo ijielekeza huko.

Akizungumzia Shirika la Suma JKT, Samia alisema Serikali italiwezesha kupata mikopo itakayotumika kuongeza uzalishaji na kujenga uwezo kulipa.

“Dhamira ya Serikali ni kuliwezesha jeshi hili liwe la kisasa zaidi na litimize majukumu yake kwa ufanisi wa hali ya juu,” alisema.

Waziri wa Ulinzi na JKT, Innocent Bashungwa alimshukuru Rais Samia kwa kuongeza bajeti iliyoongeza vijana wanaojiunga na JKT kwa mujibu wa sheria kutoka 30,000 mwaka jana hadi kufikia 52,000 mwaka huu.

Alisema maelekezo ya Rais ni kuhakikisha kuwa vijana wote wanaomaliza kidato cha sita wanapitia mafunzo hayo kwa mujibu wa sheria na mwaka huu kuna vijana 117,000 walihitimu kidato cha sita na wanaendelea na mafunzo hayo.

Awali, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda alisema JKT inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa raslimali watu na fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu itakayosaidia kufanikisha malengo yake.

“Niwatake sasa JKT kuzifanya changamoto hizo kuwa fursa ya kufanya ubunifu na kuweka mikakati itakayowawezesha kutekeleza majukumu yenu kwa ufanisi stahiki,” alisema jenerali Mkunda.

Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele alisema mafunzo hayo yalianza na vijana 11, lakini hivi sasa vijana walioko kambini kwenye mafunzo hayo ni 52,000.

Viongozi wapewa tuzo

Katika kilele hicho, Rais Samia alikabidhiwa tuzo ya heshima na Bashungwa huku yeye (Rais) akikabidhi tuzo kwa familia za waasisi wa JKT ambao ni Rais wa awamu ya kwanza, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Serikali ya Zanzibar Hayati Abeid Amani Karume.

Tuzo ya Mwalimu Nyerere ilikabidhiwa kwa mtoto wake, Makongoro Nyerere ambaye ni mkuu wa Mkoa wa Rukwa.

Tuzo ua familia ya Karume ilipokelewa na mkuu wa Brigedi ya Zanzibar, Brigedia Jenerali Said Hamis Said kwa niaba ya familia.

Hayati Karume na Nyerere wameacha wajane na watoto ambao mara nyingi kwenye matukio ya kukabidhiwa huwawakilisha.

Wadau wazungumza

Akizungumzia agizo la Rais Samia juu ya miradi ya BBT, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda alisema agizo la Rais kuunganisha JKT na mpango wa BBT linaweza kuwa na maana lakini kwa namna nyingine bado kuna tatizo.

Dk Mbunda alisema hata kabla ya kuunganishwa na JKT, mpango wa BBT bado umekuwa na mashaka makubwa kwani unahitaji kufanyiwa utafiti.

Alisema katika suala linalohusu vijana, lilipaswa kusimamiwa kwa kufanya utafiti wa kina kuhusu nani achukuliwe au nani aachwe lakini kwa namna ilivyo ni kama limechukuliwa kinadharia zaidi.

“Sina uhakika hata namna walivyochukuliwa wale wa awali, hivi unawezaje kuwachukua watu na kuanzisha mpango ambao hujaufanyia utafiti, mimi sina mawazo tofauti ikiwa wamefanya utafiti wa kisomi maana lazima tuchukue vijana wenye idea (ufahamu) ya kilimo,” alisema Dk Mbunda.

Ofisa kilimo wa mkoa wa Dodoma, Bernard Abraham alisema mpango wa Rais wa kuunganisha JKT na BBT unaweza kuwa na maana kubwa kwani wengi watakaochukuliwa watakuwa ni vijana wenye wito na mambo ya kilimo.

Abraham alisema vijana wanaotoka JKT wanakuwa majasiri na wenye uzalendo na wanakuwa wameshafundishwa kazi, yakiwemo mambo ya kilimo, ambayo hayatakuwa mageni kwao.

“Kutoka JKT wanaweza kupatikana vijana waliotoka shule za kilimo na wakiunganisha na uzalendo na kuwa anuani zao za makazi zinafahamika vema, nafikiri tunakwenda kutimiza lengo letu,” alisema Abraham.

Hata hivyo, alipendekeza uchaguzi wa vijana wanaokwenda kujiunga na BBT uangaliwe kwa mapana na vigezo viwekwe, kubwa ikiwa ni uhiyari wa wahusika.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi