Kitaifa
Juhudi za ziada zatakiwa kufikia usawa nchi za SADC
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kokasi ya Wanawake katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Regina Esparon amesema nguvu ya ziada inahitajika kufanya mapinduzi katika usawa wa jinsia kwenye uongozi.
Kauli hiyo ya Regina inatokana na kile alichoeleza kuwa, takwimu za African Barometer zinaonyesha ni asilimia 22 pekee ya wanawake ndiyo wanaoshika nafasi za uongozi katika nchi za Afrika.
Regina ametoa kauli hiyo leo, Julai 3, 2023 katika mkutano wa 53 wa Jukwaa la wabunge wa nchi za SADC uliofanyika jijini Arusha na Rais Samia Suluhu Hassan akiwa mgeni rasmi.
Katika hotuba yake hiyo, amesema pamoja na juhudi zinazofanywa bado nchi za Afrika zinakabiliwa na changamoto ya usawa katika uongozi.
Akirejea takwimu za utafiti wa African Barometer, Regina amesema ni asilimia 22 tu ya wanawake ndiyo wanaoshika nafasi za uongozi katika mabaraza ya mawaziri ya nchi za Afrika.
“Kunahitajika nguvu ya ziada na mbinu za kimapinduzi ili kuwawezesha wanawake na hatimaye waongezeke katika uongozi wa kisiasa,” amesema.
Katika hotuba yake hiyo, ameipongeza Tanzania kwa kuwa mfano wa kuwa na Rais mwanamke, akisema uongozi wake umekuwa kielelezo cha uwezo wa wanawake katika kuongoza.
“Uongozi wake ni kielelezo cha mafanikio ambayo mwanamke akiaminiwa na kupewa nafasi atayafikia mbali na changamoto za jinsia yake,” amesema.
Amesisitiza uwezeshwaji wa wanawake hata katika shughuli za kilimo, akifafanua ndilo kundi linalofanya kazi kubwa, lakini linakabiliwa na changamoto ya uwezeshaji.
Ametaja vikwazo vinavyowakabili wanawake ni umiliki ardhi, elimu ya kilimo na rasilimali nyingine wezeshi kwa uzalishaji.
Kama wanawake, ameeleza wana wajibu wa kuhakikisha vikwazo hivyo vinatatuliwa ili kuwapa nafasi wanawake wawe na mchango katika sekta ya kilimo katika nchi za SADC.
“Kuwawezesha wanawake katika kilimo ni jambo jema litakalokuza usalama wa chakula katika nchi zetu za SADC,” amesema.
Pamoja na kuwahusisha wanawake katika kilimo, amesema ni vyema pia wahusishwe kwenye kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.