Connect with us

Kitaifa

Machinga warejea kimyakimya

Dar es Salaam. Vijana wengi wamejikita kufanya ujasiriamali, licha ya kukabiliwa na changamoto lukuki, ikiwamo ukosefu wa maeneo rasmi ya kuendesha shughuli zao.

Kutokana na hali hiyo, baadhi yao hulazimika kufanya shughuli hizo kando mwa barabara na maeneo mengine yasiyopangwa na mamlaka husika licha ya Serikali kuweka katazo.

Maeneo mengine wanakofanyia biashara ni juu ya mitaro na mifereji, barabara za waenda kwa miguu, hifadhi ya barabara na mengine ya taasisi za Serikali na shule, hivyo kuleta usumbufu kwa wananchi na mali zao.

Septemba 2021, Rais Samia Suluhu Hassan aliwaagiza wakuu wa mikoa nchini kuwapanga wajasiriamali hao maarufu kama machinga katika maeneo stahiki bila kusababisha vurugu.

Licha ya utekelezaji wa agizo hilo, sasa wamerejea kwenye maeneo walikoondolewa, huku baadhi ya watu wakijitengenezea mazingira ya kujipatia kipato kutoka kwa wafanyabiashara hao kwa kuwapangisha katika maeneo rasmi na yasiyo rasmi.

Ni kwa vipi hurejea

Baadhi ya machinga walizungumza na Mwananchi wakieleza namna wanavyopata maeneo ya kufanyia biashara na namna wanavyokwepa kukamatwa katika yasiyo rasmi.

Elihuruma Mroso, mjasiriamali anayefanya shughuli zake Kariakoo katika Mtaa wa Kongo, anasema baadhi ya watu wamegeuza maeneo yasiyo rasmi kuwa mtaji wa kujipatia kipato.

“Kuna watu wana nguvu ya kukuruhusu ufanye biashara katika eneo lililokatazwa baada ya kuwapatia kitu kidogo (fedha) ili wakulinde. Kati ya hao wapo viongozi wa chama cha Machinga,” anasema Mroso.

Mfanyabiashara mwingine wa Kariakoo katika mtaa wa Kongo, ambaye hakutaka kutajwa jina anadai ukiwa karibu na mgambo wa jiji unaweza kuendesha biashara maeneo yasiyo rasmi pasipo kubughudhiwa.

“Mgambo wakishabeba bidhaa zako siku ya kwanza, ya pili na ya tatu, unaanza kuwa na urafiki nao. Unachopaswa kufanya ni kutenga fedha za kuwapa kila siku, kwa mwezi unaweza kuwapa kati ya Sh50,000 hadi Sh100,000 kulingana na eneo ulipo. “Hawa husaidia pia wakubwa wao wanapopanga kufanya operesheni za kushtukiza za kukamata watu, huwapigia simu ili waondoke kwa kuwa wanajua wasipofanya hivyo na wao kula yao imeharibika,” anasema.

Hayo yakijitokeza kwa wanaofanya biashara maeneo yaliyozuiwa, baadhi waliokabidhiwa meza maeneo rasmi katika baadhi ya mitaa iliyoko Kariakoo badala ya kuyatumia huyakodisha ili kujiingizia kipato. Meza ya biashara katika maeneo hayo hukodishwa kwa Sh200,000 na utalazimika kulipa kwa miezi mpaka sita, sawa na Sh1.2 milioni. Wakati wa operesheni ya kuwapangia maeneo machinga iliyofanywa na Halmashauri ya Jiji la Ilala, machinga walipatiwa meza hizo kwa Sh85,000.

Machinga wanasemaje?

Mmoja wa wanaofanya udalali wa maeneo anasema huwatoza wanaotaka maeneo kuanzia Sh50,000 hadi Sh200,000 akijipatia kipato kwa njia hiyo.

Anasema wakati wa sikukuu maeneo hupanda bei kwa kuwa mtu ana uhakika wa kuuza bidhaa kwa wingi.

Salma Chaurembo, anayefanya biashara Kigamboni anasema hupanga bidhaa maeneo yasiyo rasmi kwa kuwa hupata wateja wengi wanaoshuka kutoka kwenye vivuko.

Licha ya kufukuzwa mara kwa mara, Erasto Fanuel, anayefanya biashara katika stendi ya Mbezi Mwisho anasema eneo hilo ni kimbilio kwa kuwa lina wateja wengi.

Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Dar es Salaam, Yusufu Namoto anasema imeshindikana kuzuia wafanyabiashara kurejea barabarani. Anasema kutokana na mahitaji, baadhi ya watu hukodisha meza kwa wengine.

“Suala la meza kuuzwa nakiri lipo, kwani kuna baadhi huziuza kwa lengo la kwenda kufanya mambo mengine,” alisema.

Kutokana na hilo, anasema wamejikuta wakiongezeka kutoka wafanyabiashara 5,245 hadi kufika 7,628 katika maeneo hayo. Alisema Dar es Salaam pekee kuna machinga 360,000.

Wanasiasa watajwa

Namoto alisema viongozi wa kisiasa wamekuwa kikwazo katika kulidhibiti hilo.

“Baada ya Serikali kutaka sisi ndiyo tuhusike kupanga kwa kuwa tunajuana, wakati mwingine viongozi wa kisiasa wamekuwa wakiingilia na kuwataka wenzetu hao wasiondoke,” anasema Namoto.

Alisema maeneo mengine machinga waliyokatazwa wasiwepo wao hawawezi kuyalinda kwa kuwa hawana mgambo.

Ili kukabiliana na tatizo hilo, Namoto anashauri kutengwe mitaa ambayo kutakuwa na mnada kwa siku maalumu.

Kwa masoko ambayo Serikali inatarajia kuyajenga aliomba washirikishwe tangu hatua za awali ili yawe rafiki kwao wasirejee barabarani.

Kauli ya mgambo

Msimamizi wa mgambo wilayani Ilala, Nsajigwa Mwakyoma hakukubali au kukataa kuhusu madai ya mgambo kupokea fedha, akisema kila mmoja ana hulka yake. Hata hivyo, anasema ni jambo linalohitaji ushahidi zaidi kuliko hisia.

Anasema wanapata ugumu kutekeleza kazi kutokana na idadi ya mgambo kuwa ndogo, huku Jiji likiwa na machinga wengi.

“Tunafanya kazi kwa kadiri ya uwezo wetu, mpaka sasa tupo mgambo 2,000, hawa hawawezi kusimamia kila eneo na kila wakati,” anasema.

Chalamila atoa wiki moja

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametoa wiki moja kwa machinga kurudi kwenye maeneo walikohamishiwa badala ya kupanga bidhaa barabarani.

Chalamila ametoa agizo hilo jana, baada ya kupokea malalamiko ya wafanyabiashara wa soko la Coca Cola lilipo Mwenge kuhusu kurejea kwa machinga kwenye maeneo waliyoondolewa.

Alisema juhudi za Serikali kuwahamisha kwenye maeneo hayo ilikuwa na nia njema, lakini wapo baadhi wameonyesha utii na wengine wamekaidi.

“Huwa sitetereki, napenda kutumia diplomasia, kama kuna jambo la kushauri njooni au nitakuja tushauriane, lakini si kutumia nguvu, nadhani mnanifahamu,” alisema.

Mkakati wa kodi

Mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo anasema sheria ya mapato inasema mfanyabiashara anayeuza zaidi ya Sh4 milioni kwa mwaka anapaswa kulipa kodi.

Wakati TRA ikisema hayo, mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Abel Kiyondo anasema haoni kama utaratibu wa kuwasajili machinga kulipa kodi ni sahihi.

“Ni vema TRA ifanye utafiti wa kina kujua kwa nini wafanyabishara wakubwa hawaweki bidhaa zao madukani na kuziweka kwa machinga,” anasema.

“Kama kitambulisho kile kingekuwa na picha na namba isingekuwa rahisi leo kukuta meza ya fulani kapewa mwingine kwa kuwa hata angekubali mhusika ingekula kwake,” anasema.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi