Kitaifa
Zuio utumiaji wa dola nchini lazua mjadala
Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa mara ya tatu imekumbushia katazo la matumizi ya fedha za kigeni kwa matumizi ndani ya nchi, hatua inayoelezwa na wachumi kuwa inalenga kuondoa athari za kiuchumi zinazoweza kujitokeza.
Taarifa ya BoT iliyotolewa jana imeeleza kwamba tamko la kwanza la kuzuia matumizi ya fedha hizo lilitolewa Agosti 2007, la pili Desemba 2017 na la tatu jana, ikiwa ni mwendelezo wa katazo la ukiukwaji wa Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006.
Juni 8, mwaka huu, wakati akizungumza na wahariri, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba alisema kuna ugumu kwa nchi kuweka kando matumizi ya dola wakati Tanzania ikichukua hatua mbalimbali kukabiliana na upungufu wa sarafu za kigeni.
Tutuba alisema hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa zinaifanya Tanzania kuwa salama dhidi ya changamoto ya upungufu wa sarafu za kigeni ulioathiri nchi nyingi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana, BoT inaukumbusha umma kwamba Serikali ilishatoa tamko kuhusu katazo la matumizi ya fedha za kigeni kwa wakazi wa Tanzania katika kulipia bidhaa na huduma.
“Katika siku za karibuni imebainika kuwepo kwa ukiukwaji wa tamko hilo. Hivyo, Benki Kuu inapenda kuukumbusha umma kwamba maagizo yaliyotolewa hapo awali kuhusu matumizi ya fedha za kigeni yanapaswa kuendelea kuzingatiwa,” alisema Tutuba katika taarifa hiyo.
Akizungumzia suala hilo, mtaalamu wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo alieleza athari za matumizi ya dola kwenye uchumi kuwa ni pamoja na kuongeza mahitaji ya sarafu hiyo, jambo ambalo linaweza kusababisha mfumuko wa bei.
“Kitu chochote ukikihitaji sana, huwa kinaongezeka thamani, kwa hiyo ukiacha kwa muda mrefu hilo lifanyike, kinachokwenda kutokea ni kwamba vile viwango vya kubadilishia fedha vitakuwa juu kwa maana kwamba, kama sasa ni Sh2,300 kwa dola moja, tunaweza kujikuta tunakwenda hadi Sh2,500 au Sh3,000,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Fedha UDSM, Dk Tobias Swai alisema ukiuza bidhaa kwa dola, unaifanya itafutwe zaidi ili watu waweze kulipia bidhaa na huduma kwa wingi, hivyo mahitaji yake yatakuwa ni makubwa kuliko ugavi. “Hali hii iko katika nchi nyingi, hata ukienda Afrika Kusini, huwezi kununua kitu kwa dola. Ni hali ya kawaida kuzuia sarafu hiyo isipate nguvu na kufanya shilingi ya Tanzania kuwa dhaifu,” alisema Dk Swai.