Kitaifa
Karume ahojiwa kwa saa moja, aeleza hatima yake
Unguja. Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Ali Abeid Karume amesema yuko tayari kupokea uamuzi wowote utakaotolewa na chama hicho kutokana na kauli alizozitoa wiki chache zilizopita.
Katika moja ya mijadala kwenye mitandao ya kijamii, alisema CCM kipo madarakani si kwa sababu kilishinda uchaguzi, bali kwa sababu ya uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Kada huyo, mtoto wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, pia alikosoa uamuzi wa Rais Hussein Mwinyi wa kukodisha visiwa vilivyopo Zanzibar kwa wawekezaji.
Kauli hizo zilisababisha tafrani kwenye chama hicho na Rais Mwinyi aliagiza wanachama wote wanaotoa kauli za kuwagawa na kukiyumbisha chama wasiachwe hadi nyakati za uchaguzi, bali wachukuliwa hatua mapema.
Kutokana na kauli hizo, Balozi Karume ameshahojiwa na chama hicho tawi la Mwera, juzi (Juni 15, 2023) alihojiwa na Kamati ya Maadili ya jimbo la Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja na jana alihojiwa na Kamati ya Maadili Wilaya ya Kati, mkoani humo.
Akizungumza na Mwananchi, Balozi Karume alisema kikao hicho kilidumu kwa saa moja, akidai nusu saa ilikuwa ya mazungumzo maalumu na nusu saa nyingine ilikuwa ya kutaniana na kuwapa hadithi.
Alipoulizwa atahamia chama gani iwapo atafukuzwa CCM, alijibu kuwa hajajiandaa kufukuzwa uanachama na ikitokea hawezi kuhamia chama kingine chochote cha siasa, kwa sababu moyo na mapenzi yake bado yapo ndani ya CCM.
Alisema katika vikao vyote alivyoitwa mazungumzo yalikuwa mazuri na zaidi yalilenga kuhoji masuala ya uchaguzi ndani ya CCM.
Kuhusu taarifa zilizosambaa mtandaoni zikionyesha amesema kadi yake ya American Express na Viza+ ni muhimu kuliko kadi ya CCM, Balozi Ali alisema, “Ndiyo nimesema kwa sababu kadi ya CCM mara ya mwisho nilijaribu kuitumia kwenye ATM lakini haikufanya kazi.” alisema
Kwa mujibu wa Balozi Ali, “Zanzibar kama unafanyika uchaguzi wa haki na wazi mgombea wa CCM hawezi kushinda kwa sababu wagombea huletwa kutoka CCM Taifa na hawafuati ushauri au kuzingatia matakwa ya wanachama wake, hili nililisema na ninaweza kulirejea tena.”
“Pia mtu akiulizia mchakato wa uchaguzi haina maana kwamba anapinga mgombea wa CCM kushindwa, nia yangu ni kujenga tujipange vizuri ili tushinde katika uchaguzi mkuu ujao,”
Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Kati, Omar Moric alisema kada huyo aliitikia wito na alifika kwa wakati katika vikao vyote viwili, cha jimbo na wilaya, akiwa amevaa sare za chama, lakini hakuwa tayari kueleza yaliyojadiliwa.