Connect with us

Kitaifa

18,449 wapata ajira Tamisemi

Dodoma. Kati ya waombaji 171,916 walioomba nafasi za kazi katika kada ya ualimu na afya kupitia Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, 18,449 wamechaguliwa na kupangiwa vituo vya kazi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma, Waziri wa Tamisemi, Angellah Kairuki alisema waliochaguliwa na kupangiwa vituo vya kazi katika kada ya afya ni 5,319 na ualimu ni 13,130 na kati yao, wenye mahitaji maalumu ni 111, sawa na asilimia 0.84.

Kairuki alisema kati ya waombaji waliochaguliwa kwenye kada ya ualimu, 7,801 wanatakiwa kufundisha shule za msingi, 5,329 kwa shule za sekondari.

Hata hivyo, katika kada ya afya kwenye nafasi 8,070 zilizotangazwa, waliopatikana na kukidhi vigezo ni 5,319 na kufanya nafasi 2,751 kuendelea na mchakato wa kutafuta watu wengine kuzijaza.

Aidha, Kairuki alisema baada ya uhakiki, kati ya waombaji waliojitokeza, 122,827 walikamilisha vigezo na kupata nafasi ya kuhakikiwa.

Alisema baada ya uhakiki, waombaji 86,448 walibaki kwenye mfumo na waombaji 49,089 waliondolewa kutokana na kuhitimu kabla ya mwaka 2015 na 47,633 waliomba masomo ambayo hayakutangazwa.

Mchakato huo, Kairuki alisema ulihusisha uhakiki wa nyaraka na kubaini kati ya watu 64 waliodai ni walemavu wa ngozi, 24 tu ndiyo walibainika kuwa na ulemavu huo.

Pia mchakato huo ulibaini uwepo wa vyeti vya kughushi 56 na 50 vinatumiwa na waajiriwa wengine.

Akizungumzia kutokukamilika kwa waombaji wa kada za afya, Mkurugenzi wa Idara ya Afya, ustawi wa jamii na lishe, Dk Ntuli Kapologwe alisema nafasi za ofisa fiziotherapia, radiolojia na tabibu wasaidizi, zimetangazwa upya.

Alisema ni kutokana na uzalishaji wa kada hizo kuwa mdogo Serikali imefanya uwekezaji wa ununuzi wa mitambo.

“Kwa upande wa kada za maofisa tabibu wasaidizi hiyo ilikuwa kwa ngazi ya astashahada lakini uzalishaji wake umekuwa mdogo na vyuo vingine vimeacha kuzitoa, kwa hiyo kada za aina hiyo ndio zimesababisha kutangazwa upya,” alisema.

Mgawanyo wenyewe

Waziri Kairuki alisema waombaji 86,448 waliokidhi vigezo vyote kwa kada ya afya walikuwa 21,273, wanaume 10,655 na wanawake 10,618 huku kwenye ualimu wakiwa 65,175, wanaume wakiwa 38,584 na wanawake 26,591.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi