Kitaifa
Warusha ‘drones’ kusajiliwa kielektroniki
Dar es Salaam. Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imezindua mfumo mpya wa kielektroniki kwa ajili ya kuwarahisishia watu wanaorusha ndege zisizokuwa na rubani (drones), kutuma maombi ya vibali na usajili wa ndege zao ndani ya muda mfupi.
Kuanzishwa kwa mfumo huo sasa kutafanya upatikanaji wa vibali kutumia takribani wiki moja hadi mbili, kutoka mwezi mmoja hadi miwili iliyokuwa ikitumika hapo awali.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mfumo huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Daniel Malanga amesema lengo la kujengwa kwa mfumo huo ni kuondoa kero waliyokuwa wakikutana nayo warushaji wa ndege hizo hapo awali.
Amesema awali mchakato huo ulikuwa ukifanyika kwa njia ya kawaida na ulimlazimu aliyehitaji kibali kupita katika ofisi mbalimbali kushughulikia suala hilo jambo lililochukua muda mrefu.
“Kwa biashara hii ni changamoto ambayo inaathiri mwenendo wa biashara na leo hii utatatuliwa kwa mfumo mpya, hii ni baada ya TCAA kuamua kuwarahisishia watumiaji wa ndege hizi kwa kutekeleza mfumo utakaorahisha mchakato wa upatikanaji vibali kuanzia usajili na matumizi,”
TCAA ilianza usajili wa ndege zisizokuwa na rubani mwaka 2020 ikiwa ni baada ya kuanza kutumika kwa kanuni za ndege zisizokuwa na rubani ya mwaka 2018 ambayo ilimtaka kila mtumiaji wa ndege hizo kujisajili.
Malanga alisema mbali na kusajili, mfumo huo pia utawawezesha watu kuwasilisha maombi mbalimbali ikiwemo ya vibali vya kuingiza ndege hizo, kutoa ndege, na kutumia ndege hizo.
“Sambamba na huduma hizo pia kutakuwapo na urahisi wa utoaji wa taarifa za uendeshaji wa ndege hizo hasa sehemu ambazo mtumiaji anatarajia kwenda kufanya shughuli zake kwa njia rahisi tofauti na awali,” amesema.