Kitaifa
Serikali kutumia Sh2 bilioni kujenga stendi ya mabasi Mbagala
Dodoma. Serikali imetenga Sh2 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha mabasi yaendayo mikoa ya Kusini katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam katika mwaka wa fedha 2023/24.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Deogratius Ndejembi leo Mei 29, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbagala (CCM), Abdalah Chaurembo.
Mbunge huyo alihoji ni lini Serikali itajenga stendi ya mabasi yaendayo mikoa ya Kusini katika eneo la Mbagala.
Akijibu swali hilo Ndejembi amesema Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na stendi ya mabasi yaendayo kusini katika eneo la Mbagala.
Amesema katika mwaka wa fedha 2023/24 Serikali kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Temeke imetenga kiasi cha Sh2 bilioni kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kuanza ujenzi wa stendi hiyo.
Amesema Serikali kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Temeke inaendelea na taratibu za kupata eneo la kujenga stendi hiyo katika Kata ya Mbagala na kwamba ujenzi utaanza pindi eneo litakapopatikana.