Kimataifa
Camilla Kutoka kuwa ‘mchepuko’ hadi Malkia wa Uingereza
Dar es Salaam. Historia inaonyesha mke wa sasa wa Mfalme Charles III wa Uingereza ambaye pia ni Malkia wa nchi hiyo, Camilla Rosemary Shand alikuwa kwenye mahusiano ya siri ya kimapenzi na mfalme huyo kwa kipindi cha miaka 15 huku wote wakiwa katika ndoa zao.
Historia ya mahusiano ya Mfalme Charles na Malkia Camilla ilianza mwanzoni mwa miaka ya 1970 walipokutana katika uwanja wa mchezo wa kukimbiza farasi na kuanzisha mahusiano pasi na kuwa na lengo la kufunga ndoa.
Hata hivyo katika kipindi hicho mwanamfalme Charles (kwasasa Mfalme Charles III) alikuwa na umri mdogo hivyo dola hiyo ya klifalme ikaona hafai kumuoa Camilla.
Hata hivyo, ripoti mbalimbali zinaonyesha Camilla alikuwa anampenda zaidi rafiki wa Mfalme Charles III aliyekuwa Afisa katika jeshi la Uingereza aliyejulikana kwa jina la Andrew Parker Bowles na mwaka 1973 alifanikiwa kufunga nae ndoa.
Camilla na Bowles walipata watoto wawili Tom (mwaka 1974) na Laura (mwaka 1978), wakati hayo yanaendelea Mfalme Charles na yeye kipindi hicho alifunga ndoa na mchumba wake Diana Spencer mwaka 1981.
Miaka mitano mbele yaani 1986, taarifa za kuwa na mahusiano ya siri kati ya Mfalme Charles na Camilla zilianza kusambaa, huku nwawili hao wote wakiwa ndani ya ndoa zao, jambo ambalo lilizua mtikisiko katika ndoa zao.
Ndoa ya kwanza kwenda kombo ilikuwa ya Mfalme Charles mwaka 1992 ambapo taarifa za kutengana na mke wake wa wakati huo Diana zilienea, huku taarifa rasmi kutoka familia ya kifalme ikionyesha wawili hao wataendelea kuwa pamoja kwa ajili ya malezi ya watoto wao na kuwa viongozi wa Wales.
Miaka mitatu mbele (mwaka 1995) ndoa ya Camilla na rafiki wa Mfalme Charles (Bowles) nayo ilivunjika rasmi kwa talaka baada ya Mfalme Charles (Mwanamfalme kwa kipindi hicho) mwaka 1994 kupitia kipindi cha runinga kuweka wazi kwamba ana mahusiano ya kimapenzi na Camilla kwa muda mrefu.
Rasmi mwaka 1996, ndoa ya Mfalme Charles na Diana ilivunjika kwa talaka na mwaka mmoja baadae Diana alifariki katika ajali tata ya gari ambayo ilizua sintofahamu duniani.
Wawili hao waliendelea na mahusiano ya kimapenzi hadi mwaka 2005 walipoamua kufunga ndoa katika kanisa la Mtakatifu George, Uingereza. Na hapo Camilla akaingia rasmi katika familia ya kifalme.
Kwa sasa Camilla ni Malkia Konsoti wa nchi hiyo.