Kimataifa
Mafao ya Uhuru, Raila yatikisa
Nairobi. Bunge la Kitaifa la Kenya linahitaji kura za walio wengi kusitisha mafao ya kila mwezi na marupurupu mengine ya Rais wa zamani, Uhuru Kenyatta kwa kile kinachoelezwa anajihusisha na siasa baada ya kustaafu.
Mbunge wa Gatundu Kusini, Gabriel Kagombe aliwasilisha hoja katika Bunge la Kitaifa Jumanne iliyopita akitaka Kenyatta anyimwe marupurupu yake ya kustaafu.
Hoja hiyo pia inalenga kusitisha mafao na marupurupu mengine ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga na aliyekuwa Makamu wa Rais, Kalonzo Musyoka.
Hoja hiyo inaungwa mkono kwa kiasi kikubwa na wabunge wanaounga mkono Muungano wa Kenya Kwanza wa Rais William Ruto.
Uamuzi wa kusitisha mafao ya Odinga na Musyoka, utaamuliwa na si chini ya nusu ya wabunge, kwa mujibu wa Sheria ya Mafao ya Kustaafu (Naibu Rais na Maofisa Walioteuliwa).
Kagombe pia anataka Hazina ya Taifa kurejesha Sh844 milioni za Kenya (sawa na Sh14.55 bilioni za Tanzania) ambazo zimelipwa kwa viongozi hao watatu wa zamani baada ya kustaafu.
Mbunge huyo anawatuhumu watatu hao kwa kujihusisha na siasa huku wakiendelea kupokea mafao yao ya kustaafu, jambo ambalo anasema ni kinyume na vifungu vya Sheria ya Mafao ya Kustaafu ya Rais ya mwaka 2003 na Sheria ya Mafao ya Kustaafu (Naibu Rais na Maofisa Wateule) ya mwaka 2015.
Sheria hizo mbili zinawalazimisha viongozi hao wa zamani kuacha siasa ili wawe na sifa za kupata mafao na marupurupu ya baada ya kustaafu. Hata hivyo, iko kimya kama wahusika hao wanaweza kulipwa.
“Bunge linaweza, kwa hoja iliyoungwa mkono na kura za wajumbe wasiopungua theluthi mbili, kuazimia kwamba Rais mstaafu au mwenzi wake, kwa kadiri itakavyokuwa, hastahili mafao yoyote au sehemu ya mafao anayostahili kwa mujibu wa sheria hii,” kinaeleza kifungu cha 4 (1) cha Sheria ya Mafao ya Kustaafu ya Rais ya mwaka 2003.
Sheria hizo mbili zinaweka misingi sawa ya kukomesha marupurupu hayo.
Bunge la Kitaifa lina wabunge 349, maana yake ni kwamba ili mafao ya Kenyatta yasitishwe, hoja hiyo inahitaji kuungwa mkono na angalau theluthi mbili ya wabunge wote, yaani wabunge 233.
Kwa upande wa Odinga na Musyoka, angalau nusu ya wabunge, yaani wabunge 175 wanalazimika kuunga mkono hoja hiyo.
“Endapo Bunge litapitisha azimio, Rais mstaafu au mwenza wake, hatastahili mafao yoyote chini ya Sheria hii au haki yao ya kupata mafao hayo itapunguzwa kwa mujibu wa azimio hilo,” inasomeka sheria hiyo.
Tangu ameondoka madarakani, Kenyatta ameendelea kukumbana na joto la utawala mpya wa Rais Ruto, aliyekuwa makamu wake wakati (Kenyatta) akiwa Rais, ambaye amekuwa akimtuhumu kwa ukwepaji wa kodi na kujificha nyuma ya maandamano yanayofanywa na wapinzani.
Katika maandamano ya Aprili, wahuni wanaodaiwa kuwa mamluki walivamia shamba la Kenyatta na kuiba mifugo yake na kuharibu mali nyingine za kiongozi huyo mstaafu zilizokuwa shambani mwake.
Mapema wiki hii, Kenyatta ameondolewa kwenye nafasi yake kama kiongozi wa chama cha Jubilee kwa kile kilichoelezwa kuwa ni hatua ya kukinusuru chama hicho kutoka kwenye anguko lake.
Kwa sasa, kiongozi wa chama cha Jubilee ni Sabina Chege na anazungumzia ushirikiano wake na serikali ya Kenya Kwanza licha ya kuwa mwanachama wa Azimio la Umoja akisema: “kwa sasa hakuna sheria inayotufunga katika mkataba huu wa kabla ya uchaguzi.”