Kitaifa
Bei ya petroli na dizeli yaongezeka Dar es Salaam
Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei mpya za mafuta zitakazotumika kuanzia leo Jumatano Mei 3, 2023 huku bei ya mafuta ya petrol na dizeli zikipaa kwa yale yanayoingia kupitia bandari ya Dar es Salaam ikilinganishwa na Aprili.
Katika taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Mwainyekule imeonyesha kwa mafuta yanayoingia kupitia bandari ya Dar es Salaam bei ya petroli itauzwa Sh2,871 mwezi huu ikilinganishwa na Sh2,781 ya Aprii.
Hali kadhalika, bei ya dizeli imeongezeka kidogo kutoka Sh2,847 Aprili hadi Sh2,871 mwezi huu sawa na ongezeko la Sh24.
Wakati bei hizo zikipaa kwa mafuta yanayoingia kwa bandari ya Dar es Salaam, hali ni tofauti mikoa ya kaskazini ikijumuisha Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara ambao bei za mafuta ya petrol na dizeli zitasalia kama ilivyokuwa Aprili Sh2,756 na Sh2,900 mtawalia
Utofauti wa bei katika mikoa inasababishwa na umbali wa usafirishaji wa mafuta kutoka bandarini na bandari ambayo mkoa husika unachukua mafuta hayo.
Kwa upande wa mafuta yanayoingia kupitia bandari ya Mtwara ambayo inahusisha mikoa ya kusini (Mtwara, Lindi na Ruvuma) bei ya mafuta ya petroli na dizeli ya rejareja itabaki kama ilivyokuwa Aprili kwasababu hakuna shehena mpya ya mafuta iliyopokelewa.
Kwa mwezi huu bei ya mafuta itakuwa juu zaidi katika Wilaya ya Kyerwa ambapo petroli inauzwa Sh3,109 na dizeli inauzwa Sh3,109 hii inasababishwa na umbali uliopo kutoka bandarini.
Dk Mwainyakule amesema ongezeko na mabadiliko hayo ya bei ya mafuta nchini yamesababishwa na mabadiliko katika soko la dunia na sababu nyingine.
“Mabadiliko haya ya bei yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia, gharama za usafirishaji (BPS Premium) na thamani ya shilingi ikilinganisha na dola ya Marekani,”amesema.
Bei hii inakuja baada ya Serikali kuondoa ruzuku ya mafuta ambayo ilikuwa inapunguza ukali wa bei hizo takribani miezi minne iliyopita.