Imesema katika utafiti wake mpya umebaini unywaji wa vinywaji hivyo kwa wingi unaweza kuleta madhara kwenye mishipa ya moyo ya kuziba ghafla na hata kusababisha vifo vya ghafla.
Hivyo, imeonya kuwa mtu asinywe zaidi ya kopo moja lenye ujazo wa mililita 250 ndani ya saa 24, huku ikisisitiza kama kuna uwezekano wa kuviepukwa, ifanyike hivyo kulinda afya ya mhusika.
Baadhi ya vinywaji hivyo ndani yake kuna maji, sukari, ladha, caffein, mitishamba, tauline (amino acid), protini, vitamini, madini. Inaelezwa kuwa caffeine pamoja na mambo mengine, inafanya kazi ya kuzuia uzalishwaji wa kichocheo cha mwili kinachohusika na kulala ama kuhisi uchovu.
Utafiti huo wa kisayansi umehusisha unywaji wake na matatizo ya moyo na mishipa kuziba ghafla inayowakumba watu wa rika zote wanaovitumia hivi sasa.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo JKCI, Pedro Palangyo alisema utafiti huo uliochapishwa juzi katika jarida moja maarufu la kisayansi nchini Marekani, unamhusisha kijana wa Kitanzania ambaye mshipa wake mkubwa wa moyo uliziba ghafla.
Hata hivyo, alisema miezi ya hivi karibuni JKCI imekuwa ikipokea vijana wengi hospitalini hapo wanaofika kutibiwa wakikabiliwa na changamoto mfanano na hizo, huku wakiwa na historia ya kutumia vinywaji hivyo.
“Unapokunywa kinywaji hiki huchukua muda wa dakika kumi hivi caffeine kuingia kwenye mzunguko wa damu na matokeo yake mapigo ya moyo na shinikizo la damu huongezeka hivyo kumuondolea mtu uchovu. Lakini, ukizidisha hiki kinywaji inaleta athari kwenye mishipa.
“Tulimpokea kijana wa Kitanzania mwenye umri wa miaka 28, ambaye alikuja na historia ya maumivu makali kifuani upande wa kushoto.
Katika hali ya kawaida magonjwa ya mishipa kuziba huwa zaidi kwa watu wazima na mara nyingi wanakuwa pia na magonjwa mengine, hususani presha na kisukari, kwa hiyo ukiona picha hii kwa kijana wa miaka 28 ni jambo sio la kawaida,” alisema.
Dk Pedro alisema baada ya kufika na hiyo historia ya kichomi kikali, walimfanyia vipimo viwili vya ECO na ECG ambavyo vilidhihirisha dalili za mishipa ya moyo upande wa kushoto kuziba.
“Katika historia yake hakuwa na vile visababishi vitano vyote hatarishi, hakuwa na magonjwa yasiyoambukiza, hakuwa anavuta sigara wala kunywa pombe, hakuwa na uzito mkubwa, ulaji wake haukuwa mbaya na pia alikuwa anafanya mazoezi.
Alikuwa ni wa kujitosheleza kiafya, pia kwa upande wa familia, hakukuwa na yeyote mwenye magonjwa ya moyo au vifo vya ghafla.
“Kitu pekee kwenye historia yake tulichokibaini alikuwa anapendelea kunywa energy drinks na alikuwa anakunywa makopo yale mawili hadi matano kwa siku…
“Na siku husika alikuwa ametoka kunywa makopo matano ndani ya saa nne. Baada ya kumaliza lile kopo la tano, ndipo alipoanza kupata kichomi kwenye moyo, kiliendelea kuwa kikali pamoja na kwamba alimeza dawa za maumivu hakikutulia mpaka ikabidi aletwe kwetu.
Kwa hiyo aliingizwa kwenye chumba cha dharura cha cathlab ambacho lengo lake ni kuchunguza mishipa ya moyo ambako wakibaini tatizo hilo wanaweza kutibu kwa kuizibua.”
Dk Pedro alisema uchunguzi ulionyesha mshipa mmoja mkubwa wa moyo upande wa kushoto ulikuwa umeziba kwa asilimia 100, tofauti na watu wazima ambao kuziba kwake mara nyingi husababishwa na mafuta; yeye damu ilikutwa imeganda mpaka kuzuia kabisa nyingine kupita katika huo mshipa.
“Bahati nzuri aliwahishwa chumba cha cathlab madaktari wetu bingwa waliweza kuuzibua huo mshipa na hatimaye damu kuendelea kupita, katika hali ya kawaida na huyu mgonjwa alirudishwa wodini, baadaye alipona na kuruhusiwa,” alieleza Dk Pedro.
Alisema mgonjwa huyo ataendelea kutumia dawa mbalimbali katika maisha yake yote kwa kuwa aliwekewa kifaa kinaitwa ‘stant’ wakati wa kuzibua ule mshipa ili kuhakikisha hauzibi tena.
Ongezeko la matumizi
Dk Pedro alisema matumizi ya vinywaji vya kuongeza nguvu yamekuwa makubwa katika jamii na yanaongezeka huku vijana wengi wakivitumia si kwa sababu ya kujipa nguvu, bali kwa kupenda ladha yake.
“Kumekuwa na wimbi la watu wanakaa wanakunywa makopo matano, sita kwa sababu hataki kutumia kilevi lakini kuna madhara makubwa kwa wanaotumia, ukiacha kuumwa kichwa na mapigo ya moyo kwenda kasi, vinywaji hivyo vinachochea damu ya mtu kuganda.
“Energy drinks husababisha damu kuwa nzito kuliko inavyopaswa na ikiwa nzito inaweza kusababisha damu kuganda kama ilivyokuwa katika kisa hiki, kwa hiyo ni muhimu kuendelea kupaza sauti kwa jamii zetu na kwa wale wanaviotumia ni vizuri wakaacha kabisa,” alisema Dk Pedro.
Alisema takwimu za hivi karibuni za taasisi hiyo zinaonyesha wanapata wagonjwa wengi wa mishipa kuziba kwa watu wenye umri mdogo ambao katika hali ya kawaida ya ugonjwa huo umri mdogo ni mtu yeyote chini ya miaka 45.
Ukubwa wa tatizo
Wanamichezo, wanafunzi na watu wanaofanyakazi ngumu ndiyo wanaotajwa zaidi kutumia vinywaji hivyo wakiamini huwaondolea usingizi, uchovu na kuwapa nguvu zaidi.
Wapo wanamichezo ambao hutumia saa chache kabla ya kuingia kuingia mchezoni au mara baada ya kucheza wakiamini itawafanya kupata nguvu za ziada na kucheza kwa kiwango.
Huku wanafunzi na madereva wakivitumia siku za mitihani ili kuuondoa usingizi na wanywaji wa pombe kali aina ya spiriti na whiskey hutumia kuchanganyia.
“Nimekua nikitumia energy drinks hasa ninapohisi usingizi na ikifika jioni saa mbili hivi ndiyo huwa naanza kunywa, hapo naweza kunywa hata tatu mpaka ninapoenda kulala muda ninaoona nimekusanya pesa ya kutosha,” alisema dereva daladala inayofanya safari zake Segerea kwenda Kawe.
Mmoja wa dereva bodaboda alisema: “Nakunywa sana hiki kinywaji na mara nyingi huwa tunachanganya hata na K-Vant inaondoa usingizi halafu unapata nguvu hata kama ulikuwa umechoka.”
Hata hivyo, wataalamu walisema iwapo mwili umechoka na unaulazimisha kwa kutumia visaidizi ina madhara.
“Ni kweli caffein husisimua mfumo wa fahamu na kumfanya mtumiaji kuhisi kuchangamka na kuondoa uchovu. Caffein huainishwa kisayansi kama kundi la opiod yaani dawa ya kulevya aina ya kichangamshi kiwango chake katika vinywaji hivi kinakubalika ni salama kwa matumizi ya binadamu lakini unapoulazimisha mwili unauchosha zaidi na unapozidisha lazima upate madhara na hatushauri kuchanganya na pombe kali ina madhara makubwa,” anasema daktari wa bingwa wa magonjwa ya moyo, Enock Erick.