Kitaifa
Rais Samia amngo’a kigogo, avunja bodi ya TRC
Dar es Salaam. Siku chache baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, kutoa ripoti ya mwaka 2021/22 ikionyesha ubadhirifu, uzembe na matumizi mabaya ya madaraka, Rais Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), Mhandisi John Nzulule na kuivunja Bodi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC).
Taarifa ya Zuhura Yunus, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu aliyoitoa juzi usiku, haikueleza sababu za Rais Samia kumuengua Mhandisi Nzulule, aliyemteua Februari 3, 2022 kushika wadhifa huo.
Pia, taarifa hiyo haikueleza sababu za kuvunja Bodi ya TRC yenye wajumbe tisa iliyokuwa ikiongozwa na Profesa John Kondoro (Mwenyekiti) na Masanja Kadogosa (Katibu) ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo.
Wajumbe wengine ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabir Bakari, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Juma Kijavara, Kondo Kibugula, Benjamini Mbimbi, Lilian Ngilangwa, Joseph Salema na Peter Noni.
Siku chache zilizopita, wakati Rais Samia akipokea ripoti hiyo, alieleza kukerwa na kitendo cha baadhi ya watumishi Serikali kuongeza gharama za bei ya ndege ya mizigo ambayo Tanzania imeagiza kutoka dola milioni 37 hadi dola milioni 86.
“Ukitizama kwa undani, hili ongezeko limeanzia huku ndani, sasa hatuwezi kwenda hivyo na nadhani hao wanaopokea hizo invoice na kuzileta kwa raha zao serikalini watupishe, hawafai kuwa katika nafasi hizi,” alisema
Tangu kutolewa kwa ripoti ya CAG kumekuwa na mijadala mikali ndani na nje ya Bunge, juu ya kuwajibishwa kwa waliotajwa kwenye ripoti hiyo kwa kuitia hasara Serikali, kuzembea, ubadhirifu na kutumia mamlaka vibaya.
Kulingana na ripoti hiyo ya CAG ya 2021/22, TRC katika mwaka wa fedha 2020/2021, lilipata hasara ya Sh22.8 bilioni huku mwaka 2021/2022 ikipata hasara ya Sh31.29.
Kwa upande wa Shirika la Ndege (ATCL), ripoti hiyo inabainisha hasara ya Sh36.1 bilioni iliyoipata katika mwaka wa fedha 2020/2021, hali hiyo ikajirudia mwaka ulioishia Juni 2022 likipata hasara ya Sh35 bilioni.
Taarifa ya Ikulu, ilieleza kuwa Rais Samia ametoa maagizo kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka kuhakikisha Makatibu wakuu na watendaji wakuu wote wa taasisi za Serikali wanapitia kwa kina taarifa ya CAG ya mwaka 2021/22 iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita ili waweze kujibu na kuzifanyia kazi kwa haraka hoja zote zinazogusa maeneo hayo huku mkuu huyo wa nchi akielekeza watendaji wote watakaobainika kuhusika na uzembe au ubadhirifu wachukuliwe hatua za kisheria.
Katika ripoti hiyo ya CAG, Kichere ameonyesha ubadhirifu.
wa fedha kwenye maeneo tofauti huku wadau mbalimbali ikiwemo Chama cha Mapinduzi (CCM), Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) kutaka hatua zichukuliwe kwa waliotajwa kwenye ripoti hiyo.
Jana Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohammed Kawaida, alitaka “Serikali irejeshe kanuni ya utumishi bungeni ili itungwe sheria kali zitakazowabana wabadhirifu wasio na nia njema ya Tanzania kwa kuwa na wanachofanya ni kuhujumu Taifa na hatupo tayari kuona hili linaendelea” kutokea,” alisema Kawaida
Alisema jumuiya hiyo inawajibu wa kuwasemea vijana na kwamba katika ripoti hiyo ya CAG imeonyesha kutokurejeshwa Sh88.4 bilioni zilizotolewa mkopo kwenye vikundi vya vijana huku kukiwa na vikundi hewa vya vijana vilivyopewa Sh895.9 milioni.
Pia, kuna mikopo inayodaiwa kwenye vikundi vilivyositisha shughuli za biashara Sh2.2 bilioni huku mamlaka za Serikali za mtaa zikionyesha kutochangia Sh5 bilioni kwenye mfuko wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Sambamba na hilo, kwa mujibu wa Kawaida aliyedai kaisoma ripoti yote yenye kurasa zaidi ya 250, kuna mikopo ya Sh147.2 milioni imetolewa kwa watu wenye ajira rasmi ilhali hawakupasawa kupewa mikopo hiyo.
Pia, alisema kumebainika kasoro za kutoshirikishwa kwa wataalamu katika utoaji na urejeshaji wa mikopo “Tunaunga mkono kwamba fedha za vijana zianze kutolewa katika benki kuepusha mianya ya upigaji” alisema.
UVCCM inatoa kauli hiyo siku chache kupita tangu Kamati Kuu ya CCM chini ya uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan, kutaka waliohusika na ubadhirifu kuchukuliwa hatua kali. Mbali ya UVCCM na CCM yenyewe, baadhi ya wabunge nao wamekwisha paza sauti zao kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Katika mkutano wake wa jana, Kawaida, alizungumzia maadili ndani ya chama hicho, akisema wapo baadhi ya wanachama wanaokengeuka na kwenda kinyume na katiba ya chama.
“Tunapaswa kuilinda nchi yetu, kuwatetetea na kuwasemea viongozi wetu,” alisema Kawaida
Alitumia fursa hiyo kuwataka vijana wanaojiingiza kwenye vitendo vya ukosefu wa maadili
“Taifa lolote linakuwa na maadili, mila na desturi na sheria zake, niwaombe hususani vijana wale wote wenye vitendo vya ukosefu wa maadili waache mara moja vitendo hivyo” alisema.