Kitaifa
Wizi mpya Kariakoo unavyowatisha wafanyabiashara, wananchi
Dar es Salaam. Mbinu mpya ya uhalifu imezuka katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam kwa wahalifu kutumia ugomvi bandia kuwaibia wafanyabiashara na watu wengine wanaofika eneo hilo la kibiashara.
Mbinu hiyo ya kihalifu inatekelezwa na makundi ya vijana, ambapo mmojawapo humsogelea mtu ambaye ni mgeni wa mitaa husika kisha kuanza kumtuhumu kwa sauti, kwamba ameibiwa na anadai mali yake.
Hayo yakiendelea, watu wengi wanaokuwa eneo hilo, hudhani kuwa vijana hao wanagombana wenyewe kwa wenyewe, muda mwingine kuingilia kati kuwaamulia au kupotezea wakiendelea na shughuli zao.
Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Renatus Mlelwa alipoulizwa kuhusu hali hiyo, amesema wateja wao wamekuwa wakiibiwa mara kwa mara na ndiyo maana wamekuwa wakiliomba Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi.
“Kutokana na umati uliopo Kariakoo kuzongwa na watu na kuibiwa kesi hizi tumekutana nazo, wengine wanaibiwa kwa kuchaniwa pochi zao, hususan wakijua mtu huyo ametoka kuchukua pesa benki,” amesema Mlelwa.
Amesema jambo kama hilo lilimkuta mteja wake ambaye alitoka kuchukua pesa kwa ajili ya kufunga mzigo, walimwibia Sh10 milioni baada ya kumchania mkoba na hakujua nani amezichukua kwa sababu alipishana na watu wengi.
Mlelwa amesema wezi wa Kariakoo kila siku wanabuni njia mpya ya kuibia watu, hivyo ulinzi unahitajika ili wateja wanaofika eneo hilo wawe salama.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kariakoo Magharibi, Said Omary amekiri kuwepo kwa mbinu hiyo inayotumiwa na wahalifu.
“Tatizo ni kwamba kila ukija na mbinu ya kukabiliana nao, wao wanakuja na mpya. Lakini sasa inabidi tushirikiane na Jeshi la Polisi kwa ukaribu ili kuzuia hali hii ambayo inawaathiri watu wengi,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi Mei 21, 2025 Kaimu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Faustine Mafwele amesema watafanya operesheni ya kuwakamata wote wanaokutwa na makosa hayo.
Amesema operesheni hiyo itahusisha pia wizi wa mifuniko ya vioo vya pembeni vya magari (Side mirror) katika Barabra ya Uhuru, Karume, Msimbazi na Uhuru.
“Jeshi la Polisi tumejipanga kwa ajili ya operesheni hiyo kuanzia wiki hii,” amesema.
Kamanda huyo amesema operesheni hiyo inatokana na malalamiko ya wananchi kuwa wanapokuwa kwenye foleni wezi wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kung’oa vifuniko vya side mirror za magari.
Ushuhuda wa tukio
Mei 16, 2025 majira ya saa sita mchana, Mwananchi ilishuhudia tukio mojawapo katika Mtaa wa Mchikichi, ambapo mwanamke mmoja alivamiwa na vijana wawili waliodai kwamba wanamtafuta muda mrefu, baada ya kuwakopa na kutoweka.
“Nimeshangaa nimevamiwa na watu wawili wakisema nimekopa kwao. Wakanisukuma, wakaninyang’anya simu. Siwajui, sijawahi kuwaona,” alieleza dada huyo huku akiwa na hofu na mshangao.
Mfanyabiashara Jamali Shamte wa Mtaa wa Congo amesema visa hivyo ni vya kawaida, hasa katika maeneo ya msongamano.
“Siku hizi wezi wamekuja na mbinu mpya wanaweza kukufuatilia kila duka unaloingia, wakiona unaelekea kupanda gari wanaanzisha mzozo wa kudai kuwa umeiba kitu wanachokihitaji, wanataja na duka ulilotoka,” anasema.
Zamda Shedrack, machinga anayefanya biashara pembezoni mwa mtaa huo, amesema wezi hao wamekuwa na hiyo tabia na ukiingilia wanasema waachwe wanajuana, kwa hiyo asilimia kubwa wanaoshuhudia wanaendelea na majukumu yao bila kuwaingilia.
“Wakikutana na mtu anayejaribu kusaidia wanajibu kuwa wanajuana na wanayemtendea uhalifu, au kwamba ni mzozo wa kifamilia. Watu wamezoea, sasa kila mtu anaendelea na shughuli zake,”amesema Zamda,
Mashaka Mchome, dereva wa bodaboda, amesema alishuhudia vijana hao wanataka kumwibia mtu pikipiki yake wakisingizia amechelewesha malipo ya mkataba, lakini aliokolewa baada ya madereva wenzake kuingilia kati.
“Kwa sababu bodaboda tuna ushirikiano, tulifika na kuuliza kulikoni wakawa wanatuelezea kuwa pikipiki ni ya mkataba na mshikaji hakuwa anapeleka pesa na amekuwa akiwakimbia na simu hapokei,” amesema Mchome.
Amesema kilichosaidia dereva wa bodaboda alijitetea kuwa hawajui na kama hawaamini wampigie simu kuhakikisha kama wanafahamiana na walipotakiwa kufanya hivyo, wakadai kuwa kabadilisha namba, kisha wakakimbia.
Athari kiuchumi
Mtaalamu wa uchumi, Sheila Mussa amesema matukio kama hayo yanaweza kuathiri ukuaji wa biashara ndogo na za kati ambazo ni msingi wa uchumi wa Kariakoo.
Amesema mteja anapojua kwamba anaweza kuporwa baada ya kununua anapata hofu na ataacha kwenda, na mfanyabiashara atakosa wateja.
“Hii inaweza kudhoofisha biashara ya mamilioni kutokana na yanayofanyika, maana wezi hawachagui wanaweza kuibia hata wageni,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, wadau wa biashara na wananchi wameiomba Serikali na vyombo vya usalama kuimarisha doria, wasisubiri matukio hayo yatokee ndipo wachukue hatua.
“Kariakoo ni moyo wa uchumi wa Dar es Salaam ukiacha wahalifu waendelee hivi, itawatia hofu wateja,” amesema Jamali Shamte, mmoja wa wafanyabiashara.