Kimataifa

Makardinali wanaotajwa kumrithi Papa Francis

Rome, Italia. Huenda tukamshuhudia Papa wa kwanza mweusi au kutoka bara la Afrika, au huenda akachaguliwa yule Kardinali aliyewahi kusema kuwa ndoa za jinsia moja ni “pigo kwa ubinadamu”… Hawa hapa ni baadhi ya wanaotajwa kumrithi Papa Francis baada ya kufariki dunia akiwa na umri wa miaka 88.

Baada ya kifo cha Baba Mtakatifu Francis kilichotokea leo Jumatatu, Aprili 21, 2025, dunia ipo katika kipindi cha kusubiri kwa hamu na mshikamano, ikitazamia ni nani atakayemrithi katika wadhifa wa juu kabisa wa uongozi wa Kanisa Katoliki. Wakati huu, Makardinali kutoka pembe zote za dunia wanakusanyika mjini Roma kwa ajili ya ‘Konklave’ (baraza la siri la makadinali linalomchagua papa).

Francis alikuwa Baba Mtakatifu wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini, hatua iliyotafsiriwa na wengi kuwa ishara ya mabadiliko makubwa ndani ya Kanisa hilo. Je, uteuzi huo ulikuwa mwanzo wa sura mpya katika historia ya Kanisa Katoliki? Na sasa, je, tuko ukingoni mwa kumshuhudia Papa wa kwanza mweusi kutoka Afrika, au kutoka bara la Asia?

Hawa hapa ni baadhi ya wanaotajwa tajwa na kupewa nafasi ya kuhudumu katika nafasi hiyo ya juu kabisa kwenye kanisa hilo…

Peter Turkson, 76

Aliyekuwa Askofu wa zamani wa Cape Coast, anaweza kuwa Papa mweusi wa kwanza na atakuwa na mvuto kwa Afrika. Alizaliwa nchini Ghana, na alitumwa na Papa Francis kama mjumbe wa amani kwenda Sudan Kusini. Anashikilia msimamo wa kati kuhusu suala gumu la uhusiano wa watu wa jinsia moja, akieleza kuwa sheria katika nchi nyingi za Afrika ni kali mno, lakini maoni ya Waafrika kuhusu suala hilo yanapaswa kuheshimiwa. Turkson alikuwa chaguo la juu kwa wanaombashiria wakati fulani katika kikao cha uchaguzi wa Papa mwaka 2013, ambapo Francis alichaguliwa.

Luis Antonio Tagle, 67

Tagle, aliyekuwa Askofu Mkuu wa Manila, naye ameibuka kwenye kundi la vinara katika kubashiriwa kwamba anaweza kuwa Papa. Atakuwa na mvuto kwa kuwa atakuwa Papa wa kwanza kutoka Bara la Asia, eneo ambalo idadi ya Wakatoliki inakua kwa kasi. Amepinga haki za kutoa mimba nchini Ufilipino, lakini anachukuliwa kuwa miongoni mwa watu wenye msimamo usio mkali sana. Amelalamika kuwa Kanisa Katoliki limekuwa kali kupita kiasi dhidi ya wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja na wanandoa waliotalikiana, jambo ambalo limeathiri kazi yake ya injili.

Pietro Parolin, 70

Yeye ndiye anayehesabiwa kuwa karibu zaidi na mgombea wa ‘mwendelezo’, kutokana na kufanya kazi na Papa Francis akiwa Katibu wa Jimbo la Kardinali. Anaonekana kuwa wa msimamo wa wastani, ingawa si wa karibu sana na mrengo huria kama ambavyo Papa Francis amewahi kuonekana. Wakati Ireland ilipopiga kura mwaka 2015 kuruhusu ndoa za jinsia moja, Parolin aliitaja hatua hiyo kuwa ‘ushindi wa maangamizi kwa ubinadamu’. Hivi karibuni, nyota ya Parolin imepungua kidogo kutokana na mwaka 2018 kusimamia makubaliano kati ya Vatican na China, ambayo baadhi wanayachukulia kuwa ni kujisalimisha kwa Chama cha Kikomunisti cha China.

Peter Erdo, 72

Askofu Mkuu wa Esztergom-Budapest huenda akawa Papa wa pili, baada ya Yohane Paulo wa Pili (John Paul II), kuwa ametumikia katika eneo la zamani la Umoja wa Kisovieti, ambako viongozi wa Kanisa walikuwa wakiteswa mara kwa mara. Aliongoza juhudi za kutaka mtangulizi wake, Jozsef Mindszenty, kuondolewa lawama baada ya kukamatwa kwa kupinga utawala wa kikomunisti wa Hungaria. Erdo ni mhafidhina wa kina ambaye amesema hadharani kupinga Wakatoliki waliotalikiana au kuoa tena kupewa ekaristi takatifu.

Jose Tolentino, 59

Anachanganywa na mchezaji wa besiboli (aina ya mchezo wa mpira wa gongo unaochezwa na timu mbili za watu tisa kila upande) wa Marekani mwenye jina linalofanana na lake, na mara nyingi hutumia kiambishi ‘de Mendonca’ kujitofautisha naye. Akitokea Madeira, Ureno mahali alikozaliwa mchezaji Cristiano Ronaldo, ametumika kama Askofu Mkuu pamoja na kushikilia nyadhifa kadhaa ndani ya Vatican. Kama mbashiriwa kijana kwa kulinganisha, amewahi kushauri  kuwa wataalamu wa masomo ya Biblia wajihusishe na dunia ya kisasa kwa kutazama filamu na kusikiliza muziki.

Matteo Zuppi, 69

Zuppi amekuwa Askofu Mkuu wa Bologna tangu mwaka 2015 na mwaka 2019 aliteuliwa na Papa Francis kuwa Kardinali. Miaka miwili iliyopita, Papa alimteua kuwa mjumbe wa amani wa Vatican huko Ukraine, ambapo alitembelea Moscow, Russia, ili ‘kuchochea hali za ubinadamu’. Ingawa hakufanikiwa kukutana na Rais Vladimir Putin, alikutana na mshirika wake tata, Patriaki Kirill, kiongozi wa Kanisa la Kiorthodoksi la Urusi, lakini bila mafanikio makubwa ya kidiplomasia kuonekana kutokana na juhudi zake.

Mario Grech, 68

Askofu Mario Grech, mzaliwa wa kisiwa cha Malta, ni miongoni mwa viongozi wa Kanisa Katoliki wanaotajwa kwa umaarufu wa kisera na uongozi wa busara. Kabla hajakabidhiwa majukumu makubwa katika ngazi za juu za Kanisa, Grech aliwahi kuhudumu kwa miaka kadhaa kama Askofu wa Jimbo la Gozo, mojawapo ya maeneo ya kidini yaliyo ndani ya Jamhuri ya Malta.

Kwa sasa ndiye Katibu Mkuu wa Sinodi ya Maaskofu, nafasi nyeti na yenye ushawishi mkubwa katika kupanga mwelekeo wa majadiliano ya kanisa kuhusu masuala makubwa yanayoikabili dunia ya leo.

Robert Sarah, 79

Alizaliwa Guinea, Kardinali Robert Sarah ni miongoni mwa majina yanayozungumzwa kwa nafasi ya kuwa Papa mweusi wa kwanza katika historia ya Kanisa Katoliki. Ingawa umri wake wa miaka 79 unaweza kuwa changamoto katika uchaguzi huu, historia yake ya huduma ndani ya kanisa ni ndefu, ya kina na yenye uzito mkubwa.

Kardinali Sarah alianza kulitumikia Kanisa katika nafasi za juu za Vatican tangu enzi za Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, jambo linalomweka katika kundi la viongozi waliokaa kwa muda mrefu na waliotunukiwa heshima ya kipekee ndani ya muktadha wa vuguvugu la kimataifa la Katoliki.

Akitambulika kama mmoja wa viongozi wa msimamo wa kizamani, Sarah amekuwa mstari wa mbele kukemea vikali dhana ya jinsia aliyoielezea kama tishio kwa maadili, utulivu wa kijamii na mfumo wa maisha ya binadamu.

Kadhalika, amewahi kutoa matamko makali dhidi ya misimamo mikali ya Kiislamu, akisisitiza kuwa itikadi kali zinazopandikizwa kwa jina la dini ni hatari si tu kwa imani za watu bali pia kwa amani ya dunia nzima.

Ingawa nafasi yake katika mbio za kumrithi Papa Francis inaweza kuzuiwa na umri, haiepukiki kusema mchango wake katika masuala ya imani, maadili na msimamo wake wa kutetea mafundisho ya jadi ya Kanisa Katoliki unaendelea kumweka katika orodha ya wagombea wenye heshima na ushawishi mkubwa.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi