Kitaifa
Mfahamu Wasira anayevaa viatu vya Kinana CCM

Dar es Salaam. Stephen Wasira ni mmoja wa wanasiasa mashuhuri wa Tanzania. Amejitokeza katika medani za siasa na maendeleo ya Taifa kwa zaidi ya miongo minne.
Alizaliwa Jumapili ya Julai Mosi, 1945 katika Wilaya ya Bunda, mkoani Mara. Maisha yake yamejikita katika siasa, uchumi na uongozi wa umma.
Akiwa mwanasiasa mwenye msimamo thabiti, Wasira ameshikilia nyadhifa nyingi za uwaziri, usimamizi wa chama na nafasi nyingine muhimu ambazo zimeacha alama isiyofutika katika historia ya Tanzania.
Wasira alipata elimu ya juu nchini Marekani katika Chuo Kikuu cha American, Washington, DC nchini Marekani. Alitunukiwa Shahada ya Kwanza katika Uchumi na Masuala ya Kimataifa, Shahada ya Uzamili katika Uchumi na Shahada ya Uzamili katika Utawala wa Umma.
Elimu ilimwandaa vyema kushughulikia changamoto za kiuchumi na kiutawala ambazo alikabiliana nazo baadaye katika maisha yake ya kisiasa na kiutendaji.
Safari ya kisiasa
Wasira alianza siasa akiwa na miaka 25, alipoteuliwa kuwa mbunge wa Mwibara mwaka 1970.
Katika kipindi hicho, aliteuliwa na Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, kuwa Naibu Waziri wa Kilimo (1972–1975) na baadaye Mkuu wa Mkoa wa Mara (1975–1982).
Nyadhifa hizi zilimpa uzoefu wa kipekee wa kiutawala na uwezo wa kushughulikia masuala ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kati ya mwaka 1982 na 1985, Wasira alihamishiwa ubalozi wa Tanzania nchini Marekani kama ofisa mwandamizi. Alirejea nchini mwaka 1985 na kushinda tena ubunge jimbo la Bunda, nafasi ambayo ilimruhusu kushiriki katika maamuzi muhimu ya kitaifa.
Nyadhifa za uwaziri
Wasira alishika nafasi mbalimbali za uwaziri. Chini ya utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Serikali za Mitaa na Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo (1989–1990).
Katika awamu ya nne ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, alihudumu kama Waziri wa Maji (2006), Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika (2006–2008) na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) kati ya 2008 na 2010.
Kati ya mwaka 2010 na 2014 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu wa Masuala ya Jamii).
Katika nafasi hizi, Wasira alisimamia miradi ya maendeleo, hasa katika sekta za kilimo, maji na usimamizi wa serikali za mitaa. Jitihada zake zililenga kuhakikisha wananchi wa vijijini na mijini wananufaika na rasilimali za Taifa.
Msimamo, ushupavu
Wasira anajulikana kwa ushupavu wa kisiasa na uwezo wa kushindana na wapinzani wake kwa hoja. Sifa hii imemjengea heshima kubwa katika siasa za Tanzania.
Mwaka 1995, aligombea ubunge kupitia Chama cha NCCR-Mageuzi baada ya kutofautiana na CCM, lakini ushindi wake ulifutwa na mahakama. Alirejea CCM mwaka 2005, akashinda tena ubunge wa Bunda. Aliendelea kushika nafasi za uongozi wa juu serikalini.
Safari ya kisiasa ya Wasira haijakosa changamoto. Mwaka 2015, alipoteza kiti cha ubunge wa Bunda Mjini aliposhindwa na Esther Bulaya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), hali iliyokuwa pigo kubwa kwake kisiasa.
Katika nyakati tofauti, Wasira amekuwa mstari wa mbele kupinga rushwa na ufisadi.
Amenukuliwa mara kadhaa akisistiza haja ya viongozi wa umma kuwa na maadili na kuwajibika kwa wananchi. Katika kampeni za kuwania urais mwaka 2015, aliahidi kuimarisha taasisi za umma na kuhakikisha zinatumika ipasavyo kupambana na ufisadi.
Msimamo ndani ya CCM
Wasira amekuwa kada wa muda mrefu wa CCM, akishikilia nyadhifa za mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Kamati Kuu (CC).
Katika uchaguzi wa ndani wa CCM mwaka 2012, alichaguliwa tena kwa kura nyingi kuwa mjumbe wa NEC, jambo lililoonyesha imani kubwa ya wanachama kwake.
Aliwahi kutangaza kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kama mgombea wa urais wa CCM mwaka 2025, akisisitiza ni utamaduni wa chama kumuunga mkono rais aliyepo madarakani kumaliza mihula yake miwili.
Wasira amezungumzia kwa kina kuhusu masuala ya uwekezaji, akisisitiza umuhimu wa kulinda rasilimali za taifa dhidi ya propaganda za upotoshaji.
Julai 29, 2023 alisema: “CCM haiwezi kuuza nchi yetu; sisi ndio tuna mikoba ya TANU na Afro Shiraz waliotukabidhi nchi hii.”
Kauli zake zimeonyesha ujasiri wa kukemea uongozi usio wa uwajibikaji na kuhimiza umoja miongoni mwa Watanzania.
Pamoja na changamoto za kisiasa alizokabiliana nazo, mchango wake katika maendeleo ya Taifa, hasa katika sekta za kilimo, maji na siasa za amani ni wa kutilia mfano.
