Kitaifa

Tatizo la ajira lamulikwa, wanafunzi CBE kupatiwa mbinu

Dodoma. Katika kukabiliana na tatizo la ajira nchini, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kimenzisha mpango atamizi wa mawazo ya biashara yanayobuniwa na wanafunzi ili kuwasaidia kusajili biashara na kujiajiri wenyewe.

Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Edda Lwoga amesema hayo leo Novemba 20, 2024 jijini Dodoma wakati akizungumza kwenye kongamano la wanataaluma wa chuo hicho kuelekea mahafali ya 59.

Lwoga amesema katika kutaka changamoto hiyo wanaendelea kuboresha mitalaa ya elimu ili kuwajengea uwezo wahitimu kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri kuajiriwa.

“Sasa hivi tunajua ajira ni ngumu sana, kwa hiyo matumaini yetu ni kuona wahitimu wetu wasiwe wa kuandika barua ya kwanza, barua ya pili na kufikia zinakuwa chakavu bila kupata nafasi za kazi,” amesema Lwoga

Amesema wanachokitaka ni kuhakikisha wahitimu wakitoka chuoni wanajiajiri na kuajiri vijana wengine.

“Huu mpango wa chuo kuatamia mawazo ya biashara yanayobuniwa na vijana tangu 2022 mpaka sasa hivi tumewalea vijana 412 ambao wako katika hatua tatu tofauti za mawazo yao kuatamiwa,”ameongeza Lwoga.

Mgeni rasmi wa kongamano hilo, Ofisa Mahusiano Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Elisipher Mollel ameutaka uongozi wa chuo hicho kuboresha mitaala kwa kila kada ili kuendana na soko la ajira katika kipindi hiki cha ukuaji wa teknolojia.

“Kama tunavyojua Kuna changamoto ya ajira hivyo ninaushauri uongozi wa chuo kutekeleza mpango huu ili kuwapa fursa wahitimu wetu”.

Kwa upande wao,  wanafunzi wa chuo hicho wameiomba Serikali kuwasaidia kwenye bunifu zao ili wasaidie kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii ikiwemo uharibifu wa mazingira.

“Kama serikali ikisapoti wabunifu watasaidia kupata nishati bora kwani hapa chuoni tunatoa watu ambao wanaubunifu mkubwa ambao wanaweza kusaidia kwenye kukabiliana na uharibifu wa mazingira,” amesema Mwamini Issa ambaye ni mwanafunzi wa chuo hicho.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi