Kitaifa

Serikali kufufua reli bandari nchi za SADC

WAZIRI wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa serikali iko mbioni kufufua reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) ili kuimarisha usafiri wa reli unaounganisha Bandari ya Dar es Salaam na nchi za Kusini mwa Afrika hususan zile za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Pia ameiagiza Shirika la Reli Tanzania (TRC) kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha inaimarika zaidi katika kuleta Mapinduzi kupitia sekta ya usafirishaji.

Profesa Mbarawa ameyasema hayo katika kikao cha 17 cha mkutano wa mapitio ya utendaji kazi cha uchukuzi kwa mwaka 2024 na kuongeza kuwa reli ya TAZARA ni njia muhimu kwa uchumi wa nchi hizi kwani inaunganisha Dar es Salaam na mataifa ya SADC kupitia usafirishaji wa mizigo.

Amesema reli hiyo TAZARA ilianza kujengwa mwaka 1970 na kukamilika mwaka 1975, ikiwa na urefu wa kilomita 1,860 na ilijengwa kwa mfumo wa Cape Gauge, tofauti na reli nyingi ambazo zimejengwa kwa mfumo wa Meter Gauge na Standard Gauge hivuo umaalumu wa reli hiyo unalenga kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na nchi jirani.

Profesa Mbarawa ameongeza kuwa kufufuliwa kwa reli ya TAZARA ni hatua muhimu kwa uchumi wa nchi zote zinazotumia reli hiyo kwani awali reli hiyo ilibuniwa kubeba mizigo yenye uzito wa tani milioni 5.5 kwa mwaka, lakini haijawahi kufikia lengo hilo ambapo mwaka 1986, TAZARA iliweza kusafirisha tani milioni 1.2, ikiwa ni kiwango cha juu zaidi kilichowahi kufikiwa.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi