Kitaifa

Mradi wa maji Ruvu kukamilika 2025

DAR- ES-SALAAM : WAZIRI  wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) William Lukuvi amesema ujenzi unaoendelea wa tanki kubwa la kuhifadhia maji safi kutoka Ruvu unatarajia kukamilika mapema mwakani.

Waziri  Lukuvi ametoa kauli hiyo alipofanya ziara ya kutembelea na kujionea maendeleo ya mradi na kuzungumza na wananchi wa Banguko katika Jimbo la Ukonga jijini Dar es salaam.

Aidha, ameeleza ujenzi wa bwawa hilo utanufaisha wananchi zaidi ya elfu 40 hasa wa Jimbo la Ukonga na Segerea na mkandarasi ameshalipwa.

“Hivyo tutashuhudia kata saba katika Jimbo la Ukonga zitakazoondokana na adhaa ya upatikanaji wa maji,” amesema  Waziri Lukuvi.

Aidha tunashuhudia fedha nyingi zinatolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji na barabara na tumekubaliana usainishaji wa mikataba ufanyike katika maeneo husika ya ujenzi wa miradi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema Mkoa umejikita sana katika kulinda amani na kuendelea kulinda raia na mali zao, ili wananchi waweze kujikita katika shughuli za uzalishaji.

“Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na kamati za ulinzi kwa kushirikisha na polisi jamiii, hakikisheni madhila ya wananchi kuogopa wahalifu yanadhibitiwa katika maeneo yenu,“ amesema Mkuu wa Mkoa Chalamila.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amesema Serikali imejenga madarasa ya ghorofa zaidi ya 80 na madarasa ya kawaida 465 kwa shule za sekondari, na kwa upande wa shule za msingi madarasa zaidi ya 437 yamejengwa.

“Mafanikio haya yanakuja kutokana na mahusiano tuliyonayao na wawakiishi wa wananchi wanaochagiza kwa kiasi kikubwa maendeleo ya miradi ya maendeleo,” amesema Mpogolo.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi