Kitaifa

Ujumuishi wa kifedha kidijitali kuwafikia wakulima

KATIKA jitihada za kuboresha sekta ya kilimo nchini, Benki ya CRDB imejipanga kushiriki utekelezaji Mpango wa Uwezeshaji Wakulima Kidijitali nchini kupitia programu ya ‘MADE Alliance: Afrika’.

Akizungumza katika Makao Makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema ushiriki wao katika programu hiyo unalenga kuwaunganisha mamilioni ya wakulima wa Kitanzania na huduma za kifedha kidijitali.

Ushiriki wa benki hiyo katika programu ya ‘MADE Alliance’ upande wa Tanzania ulitangazwa rasmi wakati wa Mkutano Mkuu wa 79 wa Umoja wa Mataifa (UNGA) uliofanyika hivi karibuni jijini New York, Marekani.

Kupitia akaunti yake ya FahariKilimo ambayo ni mahsusi kwa ajili ya wakulima, benki hiyo imekuwa inawaunganisha wakulima na huduma bunifu za kifedha kama vile malipo ya kidijitali, utunzaji akiba, huduma za bima na upatikanaji wa mikopo, jambo ambalo limesaidia kuwapa uwezo wa kuboresha shughuli zao za kilimo.

Kwa sasa, Benki ya CRDB inaongoza kwa ufadhili wa sekta hiyo muhimu, ikiwa imetoa takribani asilimia 60 ya mikopo yote iliyotolewa na taasisi za fedha.

“Ushiriki wetu katika MADE Afrika unaendana na dhamira yetu ya kuwawezesha wakulima kupitia majukwaa ya kidijitali.

“Tumejizatiti kuwapatia wakulima zana wanazohitaji ili kuboresha mbinu zao, kupata mikopo nafuu, na kujenga uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Suluhisho zetu za kidijitali kama SimBanking na mtandao mpana wa CRDB Wakala zinaleta huduma za kifedha karibu na wakulima, zikiwawezesha kuweka akiba, kukopa na kukata bima ya mazao yao kwa urahisi,” alisema.

Akielezea kuhusu huduma mahsusi zinazotolewa na benki hiyo kwa ajili ya wakulima, Nsekela alisema huduma zinazotolewa ni pamoja na mikopo ya pembejeo za kilimo, mikopo ya zana za kilimo, mikopo ya ujenzi wa maghala na uwezeshaji kupitia stakabadhi ghalani.

Vilevile, Nsekela alisema benki yao inashirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutoa bima ya afya kwa wakulima na kupitia kampuni tanzu ya CRDB Bank Insurance, inatoa bima ya mazao dhidi ya majanga kama ukame na mafuriko, kuhakikisha wakulima wanajilinda na majanga yanayoweza kujitokeza.

Katika jitihada zake za kukuza ujumuishi wa kifedha, Benki ya CRDB imeendelea kuboresha jitihada zake za kuwafikia wakulima wengi zaidi kupitia programu ya IMBEJU Kilimo inayoendeshwa chini ya taasisi yake ya CRDB Bank Foundation.

“Kubadilisha mfumo wa kifedha wa kilimo kuwa wa kidijitali ni msingi wa kuendeleza kilimo cha kisasa nchini.

“Kupitia mpango wa IMBEJU Kilimo, tunawawezesha wakulima wadogo kwa elimu ya kifedha, suluhisho za kifedha za kidijitali, pamoja na kuwapatia mtaji wezeshi.

“Programu hii inawapa mbinu za kisasa za kilimo huku ikiimarisha ushiriki wao katika huduma za kifedha za kidijitali, kuhakikisha hakuna mkulima anayebaki nyuma,” alisema.

CRDB ni benki pekee nchini iliyoweka jukwaa maalum la kujitolea kwa ukamilifu kuwawezesha wakulima kupitia programu za mafunzo.

Kupitia CRDB Bank Foundation, benki hiyo inawapatia wakulima mafunzo muhimu kuhusu ujuzi wa kidijitali, usimamizi wa kifedha na mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa – kuhakikisha wanakuwa na maarifa na zana muhimu kwa mafanikio katika uchumi wa kisasa.

 

Kama mshirika aliyeidhinishwa wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (UNGCF), benki hiyo pia inawasaidia wakulima kuanza kutumia mbinu na teknolojia zinazozuia madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Kupitia miradi kama TACATDP, benki hiyo inahimiza na kufadhili matumizi ya suluhisho za kisasa kama mifumo ya umwagiliaji, kilimo cha usahihi na mitambo ya nishati ya jua, ambayo inapunguza hatari za tabianchi na kuongeza uzalishaji.

Akizungumza kwa njia ya mtandao, Jon Hauntsaman, Makamu Mwenyekiti na Rais wa Mastercard, alieleza furaha yake juu ya ushirikiano na Benki ya CRDB katika MADE Afrika, akisema:

“Uzoefu mkubwa wa Benki ya CRDB na kujitolea kwao kwa ufadhili wa kilimo kunawafanya kuwa mshirika muhimu katika programu hii.

“Tunafurahia kushirikiana nao katika kuendeleza na kupeleka suluhisho za kidijitali zitakazowawezesha mamilioni ya wakulima kote Tanzania. Utaalamu wao wa kuunganisha huduma za kifedha na teknolojia ya kisasa, pamoja na uhusiano wao wa karibu na jamii za wakulima, unaendana kikamilifu na malengo ya programu hii.”

Ushiriki wa Benki ya CRDB katika programu ya MADE Afrika unazidi kuimarisha nafasi yake kama benki kiongozi katika kuboresha sekta ya kilimo nchini Tanzania. Kwa kuwapatia wakulima zana na msaada wanaohitaji ili kufanikiwa, benki ya hiyo inajenga mustakabali mzuri kwa wakulima wa Tanzania na kukuza mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa taifa.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi